Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Abdulla Ally Saleh
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Malindi
Primary Question
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Tanzania imesajili michezo kadhaa ambayo huingia kwenye medani ya Taifa kiushindani lakini kote huwa ni mashamba yanayozaa visingizio. (a) Je, Serikali haioni haja sasa ya kujipinda katika michezo michache kiushindani Kimataifa? (b) Je, kama kukiwa na uamuzi huo inaweza kuwa michezo ipi?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwamba katika hali halisi inavyoonesha kwamba Tanzania haijawahi kuwakilishwa nje ya michezo ya kuogelea, mpira wa miguu, riadha, ngumi katika ile michezo ambayo huwa inataka qualifications, lakini moja ya tatizo kubwa ni choice ya michezo yenyewe na pili ni ufadhili wa michezo yenyewe. Mimi siamini kwamba Serikali ndiyo isimamie kufadhili michezo kwa sababu ina-priority nyingi.
Je, Waziri haoni kwamba wakati umefika sasa kuja na mwongozo au sera ya namna ya corporate Tanzania kuchangia katika michezo? Kwa mfano Uingereza British lottery ndiyo inayodhamini Olympic system nzima ya Uingereza. (Makofi)
Swali la pili, ipo michezo ambayo kwa gharama zake
na kwa uenezi wake ni rahisi sana kuenea, mchezo chess investment kubwa wanayotaka ni chess board ambayo in-cost labda dola sita au dola saba, baada ya hapo ni kuwa-train tu watoto au vijana.
Je, Serikali inaweza kushaurika kwamba huu ni mmoja kati ya mchezo ambao unaweza kuwa kipaumbele katika Taifa, kwa sababu hauna gharama na kwa sababu unaweza ukaenea katika hali ya haraka katika nchi?
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ally Saleh Ally kwa jinsi alivyo mdau mkubwa katika maendeleo ya michezo na amekuwa akichangia sana sana masuala ya michezo katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la kwamba kuna michezo ambayo haijawahi kuwakilishwa Kimataifa, nitoe mfano tu kwamba kwa mchezo wa kuogelea nchi yetu imeshawahi kuwakilishwa, kuna vijana ambao walishawahi kwenda Canada na wakaiwakilisha nchi yetu, tuliwapa bendera na mmoja alishika namba nne, lakini pia hata riadha, walishawahi kuwakilisha nchi yetu kimataifa na mmojawapo ni Simbu na anamfahamu. Ndugu Simbu ameshawahi kutuwakilisha Kimataifa na Serikali huwa inatenga bajeti kwa ajili ya hawa, lakini hatua za awali huwa zinafanywa na Tanzania Olympic Committee ambapo inawaandaa wale wachezaji na fedha zinatoka Olympic Kimataifa na wanapofuzu sasa kushiriki mashindano yale Kimataifa ndipo Serikali inapowawezesha. Mwaka 2016/2017 Serikali ilitenga fedha na wanariadha wetu waliweza kuiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olympic.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mwongozo wa ushiriki wa sekta binafsi tunakubaliana na hilo lakini tunakwenda hasa na sera kwa sababu, sera yetu inatutaka kusimamia michezo sio tu kwa kuegemea kutambulika Kimataifa, tunasimamia michezo kwa madhumini mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuimarisha afya, afya ya Watanzania kwa ujumla, pia kudumisha amani, umoja, mshikamano na upendo, vilevile kuhakikisha kwamba tunatambulika kimataifa kama anavyosema na kumjenga Mtanzania kuwa jasiri, kukabiliana na matatizo mbalimbali. Kwa hiyo, yako masuala ya msingi ambayo yanatupelekea Serikali kusimamia michezo.
Kwa upande wa mchezo anaoupendekeza wa chess katika swali lake la pili, tunapenda sana kutoa wito kwa wananchi wote kwa wananchi wote kwamba pale ambapo kuna michezo wanayoiona ni mipya na inafaa kuingizwa katika sekta ya michezo na hasa katika shule za msingi na sekondari, ili wanafunzi wetu waweze kujifunza, tunahimiza kwamba wananchi kama hao, Walimu ambao wanaweza kufundisha michezo hiyo wajitokeze ili waweze kufundisha kwa sababu, Azimio la Michezo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1978 linahimiza wananchi wafanye ile michezo wanayoiweza, michezo wanayoipenda, michezo ambayo wana amani nayo. Ahsante. (Makofi)
Name
Grace Sindato Kiwelu
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Tanzania imesajili michezo kadhaa ambayo huingia kwenye medani ya Taifa kiushindani lakini kote huwa ni mashamba yanayozaa visingizio. (a) Je, Serikali haioni haja sasa ya kujipinda katika michezo michache kiushindani Kimataifa? (b) Je, kama kukiwa na uamuzi huo inaweza kuwa michezo ipi?
Supplementary Question 2
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Timu yetu ya Serengeti imeendelea kufanya vizuri huko ilipo, ningependa kujua Serikali imetenga kiasi gani, kwa ajili ya kuisaidia timu yetu hii ili iweze kufanya vizuri na kurudi na kombe hapa nchini? (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza sana Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana. Ninataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu hii ya Serengeti haijaibuka tu, tumeanza nayo miaka mitatu iliyopita, kwa kushindanisha vijana wa chini ya umri wa miaka kumi na tano, tukapata timu bora, tumeilea hiyo timu na kuhakikisha kwamba inashiriki kwenye mashindano ya kimataifa kabla ya hizi mechi 22 ambayo haijapata kutokea toka historia ya nchi hii, yote hii huu ni uwezeshaji na uwekezaji wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nisisitize kwamba figure kamili yaani ni kiasi gani tumetumia kama Serikali tutaiandaa tumpe Mheshimiwa Mbunge, lakini Serikali imejitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba timu hii inatuletea ushindi katika mashindano haya. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Tanzania imesajili michezo kadhaa ambayo huingia kwenye medani ya Taifa kiushindani lakini kote huwa ni mashamba yanayozaa visingizio. (a) Je, Serikali haioni haja sasa ya kujipinda katika michezo michache kiushindani Kimataifa? (b) Je, kama kukiwa na uamuzi huo inaweza kuwa michezo ipi?
Supplementary Question 3
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii niulize swali la nyongeza.
Kwa niaba ya vijana wote wa Tanzania ambao wanaweza kuwa wanufaika wakubwa sana wa michezo naomba kuuliza swali la nyongeza lifuatalo:
Je, Serikali haioni umuhimu wa kwamba ni wakati muafaka wa kuwa na shule maalum kwa ajili ya kukuza vipaji katika michezo kama sports academy? (Makofi)
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninampongeza kwa kuwatetea vijana kimichenzo, kama alisikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ni kwamba tumedhamiria. Serikali sasa hivi imekwishatenga shule takribani 55 ambazo ziko katika Mikoa yote ya Tanzania, hizi ndizo ambazo tutazichukulia kama ndizo academy zetu. Vilevile michezo ya UMISETA, michezo ya UMITASHUMTA itasaidia sana kuibua vipaji, hata hivyo tunashirikiana sana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba michezo inafundishwa katika ngazi zote za elimu tangu awali, sekondari na vyuoni. Ahsante. (Makofi)
Name
Maria Ndilla Kangoye
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Tanzania imesajili michezo kadhaa ambayo huingia kwenye medani ya Taifa kiushindani lakini kote huwa ni mashamba yanayozaa visingizio. (a) Je, Serikali haioni haja sasa ya kujipinda katika michezo michache kiushindani Kimataifa? (b) Je, kama kukiwa na uamuzi huo inaweza kuwa michezo ipi?
Supplementary Question 4
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na kwa niaba ya vijana wa Kitanzania ningependa kujua ni lini Serikali itarudisha programu ya michezo katika shule zetu za sekondari na msingi? (Makofi)
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyozungumza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza katika suala zima la shule hizi, juzi tumezindua michezo ya UMISETA hapa rasmi, bahati nzuri Kitaifa tumezindulia hapa Dodoma, tuna shule zipatazo 55.
Hata hivyo, tumetoa maelekezo maalum kwa Ofisi
za Mikoa yote sasa programu ya michezo sasa imeishaanza kurudi mashuleni na tumetoa maelekezo kwamba Maafisa Michezo wote waweze kuwezeshwa katika Mikoa yote na katika Halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba tunaibua vipaji katika michezo ya watoto wa shule za msingi na watoto wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba Serikali imeshalichukua suala hili na sasa liko katika utekelezaji. Tunawashukuru sana wenzetu wa CocaCola ambao mwaka huu wanafadhili michezo hii ya UMISETA hapa Tanzania, nayo imeishaanza vizuri na tunashukuru sana kwa kweli. (Makofi)
Name
Atupele Fredy Mwakibete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Primary Question
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Tanzania imesajili michezo kadhaa ambayo huingia kwenye medani ya Taifa kiushindani lakini kote huwa ni mashamba yanayozaa visingizio. (a) Je, Serikali haioni haja sasa ya kujipinda katika michezo michache kiushindani Kimataifa? (b) Je, kama kukiwa na uamuzi huo inaweza kuwa michezo ipi?
Supplementary Question 5
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni miongoni mwa
watu ambao ni washabiki na wapenzi wa ngoma za asili, pamoja na kwamba wewe ni mpenzi wa ngoma za asili, hata huku Dodoma kuna ngoma za asili zinaitwa Chigogo.
Je, Serikali imejipangaje kuwezesha wale wote ambao wanaanzisha ngoma za asili katika mashindano hayo? (Makofi)
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali lake liko nje ya michezo, lakini liko ndani ya Wizara yetu ni ngoma za asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi wote waendelee kuenzi ngoma za asili, hata vyombo vya habari tunavihamasisha ili viweze kupiga ngoma za asili katika vipindi vyake kwa zile asilimia 60 za local content ambazo zimepewa. Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri hilo swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa ubunifu, ujasiri na uthubutu kuanzisha mashindano ya ngoma zetu za utamaduni katika Ukanda wa Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lilivyoanza hili Waheshimiwa Wabunge ilikuwa kwa Wilaya mbili tu, Wilaya ya Rungwe na Kyela sasa imepanuliwa zaidi kuhusisha Mkoa mzima na Mikoa ya jirani. Ninatoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote katika maeneo yenu tusisubiri Serikali ianzishe hayo, hebu tufuate mfano alioutoa Naibu Spika, wote tuanzishe hayo mashindano. Sisi kama Serikali tutasaidia kuboresha hizo ngoma zetu za utamaduni. (Makofi)