Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Primary Question

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:- Je, nini mkakati na sera ya Serikali kwa wafanyakazi hususani walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri kwanza naishukuru sana Serikali yangu kwa maana ya kwamba iliweza kutatua tatizo la walimu waliokuwa wanapandishwa madaraja lakini hawapati mshahara. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa taarifa ya uhakiki wa vyeti imeshatolewa na katika Jiji la Mbeya kuna walimu zaidi ya 200 waliobaki. Je, ni lini sasa Serikali itaruhusu marekebisho ya mishahara kwa walimu hao waliokwishapandishwa vyeo vyao kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kumekuwa na tatizo la watumishi kukaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu sana na hivyo kushindwa kuleta changamoto mpya katika kipindi hiki cha Hapa Kazi Tu na kufanya kazi zao kwa mazoea. Nilitaka kujua nini mkakati wa Serikali katika hilo?Ahsante.

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alichosema Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, alitaka time frame ni kwamba katika mwaka ujao wa fedha zoezi hili litaanza. Mheshimiwa Mwanjelwa asihofu watumishi wake watapata hiyo stahiki yao inayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la watumishi wengi kukaa kituo kimoja muda mrefu, ni kweli tunafahamu kwamba mtumishi anapokaa miaka 15, 20 hana changamoto mpya ambayo anaweza akaileta katika eneo hilo. Ndiyo maana Ofisi yetu kila mwaka tumekuwa tukifanya utaratibu huo katika maeneo mbalimbali, lengo kubwa ikiwa ni kuleta hii changamoto mpya na tunaendelea kufanya zoezi hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tuko makini
sana katika kuhamisha watumishi. Kwa mfano, tumetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wetu kwamba waangalie jambo hilo, lakini wasihamishe watumishi hivi hivi bila kuwa na pesa yao kuweza kuwalipa. Jambo hili tumelielekeza na bahati nzuri Mheshimiwa Rais siku ya Mei Mosi alilitolea maelekezo maalum kwamba sasa hakuna utaratibu wa kumhamisha mtu kabla ya pesa yake kuwa tayari.
Naomba nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutahakikisha tunakuza utendaji wa kazi na kuangalia mtu kama ame-over stay kwa muda mrefu tutaona namna ya kumhamishia sehemu nyingine ili kuleta changamoto mpya.

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:- Je, nini mkakati na sera ya Serikali kwa wafanyakazi hususani walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo linatusikitisha ni kwamba pamoja na kupandishwa madaraja walimu hawa hawalipwi pesa zao suala ambalo linapelekea kila mwaka walimu hao kudai takribani shilingi bilioni 21. Je, Serikali haioni kutokuwapandisha madaraja na kutokuwalipa kunasababisha kulimbikiza madeni yao na ndiyo sababu inafanya walimu kutokuwa na motisha wa kazi? Ni lini sasa Serikali itawalipa fedha zao wanapopandishwa madaraja?(Makofi)

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu tumekuwa tukitoa taarifa mbalimbali ya madeni ya walimu ambayo tumekuwa tukiyalipa na tulisimama kwa ajili ya zoezi la uhakiki. Kwa hili naomba niwaambie, tumezungumza na hapa nilisema katika eneo langu la kwanza kwamba suala la malipo haya yote mwaka huu wa fedha unapokuja kila mtu atapata stahiki yake.
Serikali hii ya Awamu ya Tano lengo lake kubwa ni kuondoa hizi changamoto ndogo ndogo tulizokuwa nazo kwani tunataka tupate wafanyakazi wenye ari ya kutosha. Sisi ambao ni beneficiaries wa utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi lazima tuitekeleze, naomba nimhakikishie jambo hilo halina mashaka tutalitekeleza.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:- Je, nini mkakati na sera ya Serikali kwa wafanyakazi hususani walimu wanaojiendeleza katika kuwapandisha madaraja na kuwaongezea mishahara?

Supplementary Question 3

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya walimu wamekuwa wakijiendeleza wao wenyewe katika vyuo mbalimbali na kupata vyeti lakini kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikivikataa vyeti hivyo, imekuwa haivitambui. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvitambua hivyo vyeti ili waweze kupandishwa madaraja zaidi?

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kujiendeleza ni kujiendeleza tu aidha Serikali imekusomesha ama umejiendeleza mwenyewe kinachotakiwa ni kujiendeleza. Ndiyo maana katika jibu la msingi mwanzo nimesema mtu akijiendeleza maana yake ana-submit cheti chake, kinapitiwa na kuhakikiwa na Afisa Utumishi mtu huyo anastahili kupanda daraja na kuwekwa katika nafasi yake anayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna kesi kama hiyo, maana wakati mwingine hatuwezi tukajibu kesi hapa zote kwa ujumla, inawezekana kuna case by case, kama likiwa hilo basi tunaomba tujulishane hiyo kesi imejitokeza wapi tuweze kuifanyia kazi. Mtu yeyote aliyesoma provided kwamba amesoma na ana cheti halali jambo hilo halina mashaka la kuwekwa katika muundo anaostahili. (Makofi)