Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ussi Salum Pondeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chumbuni

Primary Question

MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:- Askari Polisi Zanzibar kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kutumia fedha zao za mfukoni kuwahudumia chakula mahabusu wanoshikiliwa katika Vituo vya Polisi Unguja wakati jukumu hilo ni la Serikali. (a) Je, Serikali imechukua hatua gani za kuondoa tatizo hilo tangu kulalamikiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora baada ya kufanya ziara ya ukaguzi na kugundua tatizo hilo? (b) Je, ni sababu gani zimepelekea chakula kutopelekwa katika Vituo vya Polisi wakati Bunge limekuwa likiridhia matumizi ya Wizara kila mwaka zikiwemo gharama za chakula kwa mahabusu? (c) Je, haki za binadamu zinazingatiwa vipi inapotokea askari hawana fedha za kununua chakula cha mahabusu na kulazimika kulala na njaa wakati Serikali ndiyo yenye jukumu la kuwapatia huduma ya chakula?

Supplementary Question 1

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri japo hayakidhi ukweli halisi wa mahabusu.
Je, Waziri yuko tayari apewe ushahidi wa raia ambao wanawapelekea chakula raia ambao wanakuwa mahabusu Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu haki za binadamu, kila mara kumekuwa na taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya ukosefu wa hali ya amani katika vyuo vya mafunzo Zanzibar. Je, Serikali imeshatolea ufafanuzi kuhusu chombo hicho? (Makofi)

Name

Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake lakini niseme tu kitu kimoja amekichanganya kwamba, sijakataa watu kupeleka chakula kwa mahabusu na hiyo ni hospitality ya Kitanzania. Mtu kama ana mtu wake yuko mahabusu akaamua kumpelekea chakula, Magereza ama Polisi hawazuii ndugu kuwapelekea ndugu zao chakula wanapokuwa wako mahabusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ndugu zao kuwapelekea chakula mahabusu haimaanishi kwamba Serikali haikupeleka chakula. Wakati mwingine hata mahabusu wenyewe wanakuwa na chaguo lao la chakula anachokula, wengine wana diet zao wanazotaka kula, kwa maana hiyo haingekuwa vyema sana kwa Serikali kusema lazima mtu akiwa mahabusu ale chakula cha Serikali na nadhani hata ninyi msingekubaliana na utaratibu wa aina hiyo. Sisi tunachosisitiza ni kwamba Serikali inaweka bajeti na huo ndiyo umekuwa utaratibu lakini haizuii watu kupelekewa chakula kufuatana na mahitaji yao ama ndugu wanapokuwa wamepeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lile la pili la uvunjifu wa amani, tumelisisitiza na tumeendelea kulisisitiza kwamba vyombo vya dola vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na inapotokea kesi moja moja tunazishughulikia kama kesi moja moja na hatua huchukuliwa inapotokea makosa yamejitokeza.