Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Daniel Nicodemus Nsanzugwako
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Mjini
Primary Question
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:- Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuwa na vijana wengi wanamichezo na wasanii mfano Shaaban Robert, Diamond, Ali Kiba, Banana Zoro, Linex, Mrisho Mpoto na kadhalika:- (a) Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wa Kigoma kwa kujenga Jumba la Sanaa (Theater Centre) ili vijana wa aina hii wawe na sehemu nzuri ya kuendesha shughuli zao? (b) Kama Serikali inakubaliana na hoja hiyo, kituo hicho kitaanza kujengwa lini?
Supplementary Question 1
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nipende kumkumbusha kwamba tunasema wasanii na wanamichezo wenye asili ya Kigoma, siyo wakazi wa Kigoma. Mrisho Mpoto mimi nazungumza naye, asili yake ni Kigoma ila amehamia Songea. Hata akina Diamond nao ni watu wa Kigoma lakini wanaishi Dar es Salaam. Nilitaka tuweke rekodi sawasawa maana huwezi kuwa msanii mzuri kama asili yako siyo Kigoma.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, hii Sera ya mwaka 1999 ambayo inatamka dhahiri kwamba hizi Theater Centers zitajengwa Makao Makuu ya nchi, je, Mheshimiwa Waziri huoni kwamba sera hiyo imepitwa na wakati kwamba vijana wengi wako kwenye Majiji, Halmashauri na Manispaa zetu? Ni lini Serikali itaiangalia upya sera hiyo ambayo kusema kweli imepitwa na wakati kabisa hasa Sura ile ya Nne ambayo inasisitiza kwamba hizi Theater Centers zitajengwa katika Makao Makuu ya nchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, niendelee kushukuru kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri Kigoma imetoa mchango mkubwa na kwa kweli wasanii wale wengi wao wanatoka Kigoma, Kibondo na Uvinza. Napenda kujua ni kwa nini basi Wizara isitoe mwongozo technical kwa Wakuu wetu wa Mikoa na Ma-RAS wetu ili wajue kwamba sasa wakati umefika hizi Theater Centers zijengwe katika Halmashauri na Manispaa zetu zote katika nchi yetu?
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa jinsi anavyoshirikiana vizuri na wasanii. Vile vile tunathamini mchango mkubwa wa Waheshimiwa Wabunge wote katika kuitetea na kuwa mstari wa mbele kuboresha tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ambalo linasema kwamba sera hii imepitwa na wakati, ni kweli tunakubali kabisa kwamba sera hii kwa namna moja au nyingine imepitwa na wakati. Kwa hiyo, kwa hivi sasa napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imeshaandaa Rasimu ya Utamaduni na imeshaiwasilisha katika ngazi za juu za maamuzi.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inapongeza sana kazi za wasanii na hasa kwa jinsi wanavyojishughulisha na masuala ya kijamii. Tumekuwa tukiwaona wasanii kama Mrisho Mpoto na wenzake wakijishughulisha na kampeni za kuhamasisha usafi katika Majiji yetu. Kwa sababu hiyo basi tumeona pia kuna umuhimu wa kufanya maandalizi ya Sera ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ambalo linataka Serikali itoe mwongozo kwa mikoa, tunakubaliana nalo kabisa kwamba tutatoa mwongozo huu. Pia napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kupitia Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Wizara inaendelea kutoa wataalam waliokamilika katika fani za sanaa na utamaduni ikiwemo utaalam wa uandaaji wa Majumba ya Sanaa. Hata hivyo, Wizara hii pia ipo katika mazungumzo na TaSUBa ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza kutoa mafunzo nje ya kituo hiki.
Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kuziomba Halmashauri zote ziajiri Maafisa Utamaduni. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved