Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:- Kumekuwa na usumbufu na uharibifu unaosababishwa na ongezeko la nyani ambao wanavamia mashamba ya wananchi na kula mazao kama mahindi, ndizi na sasa wanaingia katika majumba ya watu na kubeba chakula katika Kata za Ushiiri, Mrao – Keryo, Kirua – Kei, Katangera – Mrere, Kirongo – Samanga na Olele. (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapunguza au kuwahamisha nyani kwenye maeneo hayo? (b) Je, kuna utaratibu gani wa kuwafidia wananchi hasara waliyoipata kutokana na uharibifu wa nyani hao?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Waswahili wana msemo kwamba ukitaka kujua utamu wa ngoma uingie ucheze. Tatizo hili ni kubwa sana na binafsi nilikwishaongea na Naibu Waziri akawa ameniahidi atanipelekea mtaalam kutoka Arusha, hili siyo tatizo la mwaka huu nashangaa jibu linasema kwamba wanaanza kufanya utafiti. Wale wanyama wanaendelea kuzaliana, wanaendelea kuleta usumbufu, sasa hivi wanaingia hata ndani wanaepua chakula kikiwa jikoni na ni hatari sana kwa akina mama na nikisema ni hatari kwa akina mama nadhani kila mtu anaelewa. Sasa nataka nijue huu utafiti utakwisha lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, miaka ya nyuma nyani hawa walikuwa wanadhibitiwa na wananchi wenyewe kwa kuwaua kwa risasi ambazo zilikuwa zinagawiwa kutoka kwenye Ofisi ya Maliasili lakini sasa hivi wamekatazwa kufanya hivyo na Maliasili hawa hawa. Sasa naomba niulize Wizara, kwa kuwa imetamka kwamba inakusudia kuwashirikisha wananchi kwa kutumia silaha za jadi, je, Wizara iko tayari wananchi wenye silaha kama magobole na kadhalika watumie risasi kama utaratibu wa zamani?Mimi Mbunge wao niko tayari kuwanunulia risasi ili tupambane na hawa wanyama vinginevyo watuletee Wa-Congoman waje wawale kule na siyo kutuambia utafiti wakati wanaharibu watu. (Makofi)

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza Wizara kwa niaba ya Serikali inawapa pole wananchi wa maeneo ya kata zilizotajwa kutokana na usumbufu huo wa wanyama hawa nyani na ngedere na uharibifu wanaosababisha kwenye mashamba yao. Kwenye swali lake la kwanza la nyongeza anauliza utafiti utaisha lini, kwenye jibu la msingi nimesema utafiti huo unakamilika mwezi Disemba, 2017.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa nini tunafanya utafiti wakati ni dhahiri kwamba wanyama wapo na wanasumbua na wanaharibu. Mimi nafikiri utafiti ndiyo njia nzuri ya kuweza kufika mahali kupata jibu au suluhisho. Ni sawasawa na mtu anayeumwa malaria ambaye hataki damu itolewe iende kwanza ikapimwe, nafikiri hiyo haitakuwa njia sahihi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumedhamiria na tunakusudia na mimi na wewe tunaweza tukapata nafasi kabisa kupeana taarifa ya mara kwa mara katika kipindi hiki kabla ya hiyo Disemba ili tuweze kuona tunasonga mbele namna gani.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya silaha, matumizi haya yapo kwa mujibu wa sheria na kama ni matumizi ya risasi za moto sheria zinakuwa kali zaidi. Katika eneo hilo hao Serikali inashughulikia masuala hayo kwa kushirikisha Wizara zaidi ya moja, si suala la Wizara ya Maliasili na Utalii tu.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kwamba utafiti sasa ndiyo unaweza ukatuwezesha tuone ukubwa wa tatizo, uzito wake, kama utaainisha kwamba matumizi ya silaha za moto ni lazima basi labda tunaweza tukaenda huko kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo lakini kama kwenye utafiti tukiona tunaweza kutumia njia nyingine ambayo siyo silaha za moto basi itakuwa ni vema tutumie njia hizo ambazo tutazipata.