Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Asha Abdullah Juma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:- Watanzania wengi hasa wanawake wanaokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za kiarabu kama Oman na nyinginezo wamekuwa wakifanyiwa ukatili mkubwa sana unaosababisha wengine kufariki na wengine kujeruhiwa vikali. (a) Je, Serikali ina utaratibu gani madhubuti wa kudhibiti safari za Watanzania hao wanaokwenda katika nchi za Kiarabu na pia kuwabana Mawakala na kuwawajibisha inapobidi? (b)Je, ni wanawake wangapi wa Kitanzania wameuawa katika Nchi za Kiarabu na fidia kutolewa katika familia zao?
Supplementary Question 1
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nashukuru kwa majibu, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa pamoja na mikataba na vipengele vingi vilivyoratibiwa vizuri hali bado kwenye eneo hili siyo nzuri. Bado wananchi wetu wengi wanaendelea kupata matatizo hasa wanawake wanaokwenda kufanya kazi nchi za Urabuni. Serikali kupitia Ubalozi wetu inalazimika kutumia gharama nyingi za kifedha ambazo zingeweza kutumika katika shughuli za maendeleo, kwa mfano, miundombinu, standard gauge na kutununulia ndege nyingine ya Bombadier. Je, Serikali haijaona kwamba sasa wakati umefika wa kuwakatibisha hawa ma-agent, wafanya mikataba ili kuweza kuweka deposit ya fedha ambazo zitatumika kuwashughulikia wananchi wetu hawa inapobidi kurudishwa wanapokuwa wagonjwa wakati wanapokuwa wametelekezwa na waajiri wao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa zipo taarifa na malalamiko kwamba baadhi ya wananchi wetu hawa wanaokwenda kufanya kazi huko huambiwa, kwa mfano, wanakwenda kuuza duka wakafika kule wakafanyishwa kazi nyingine kinyume na hilo duka na kinyume na ridhaa yao na pengine kusababisha hatari kwenye afya zao. Je, Serikali inalisaidiaje jambo hili katika kudhibiti na kuhakikisha kama wananchi wetu hawaendi kuongezewa udhalilishaji huko nchi za Kiarabu? Ahsante. (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Spika, la kwanza, Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua namna ambavyo Serikali tutaweka mfumo mzuri wa kuweza kuwabana mawakala hawa. Kazi hii ya kuwapeleka Watanzania kufanya kazi nje ya nchi inaratibiwa kwa mujibu wa sheria zetu na mawakala hawa wanasajiliwa katika utaratibu ambao umewekwa. Wakala yeyote ambaye anavunja masharti na matakwa ya sheria hizi tumekuwa tukimchukulia hatua kwa kufuta pia usajili wake ili kumtaka ufuate taratibu za nchi ambazo tumeziweka katika kupeleka wafanyakazi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika eneo hili nitoe rai tu kwa wafanyakazi wote ambao wanafanya kazi nje ya Tanzania hasa katika nchi za Kiarabu hususani Oman kufuata taratibu tulizoziweka kupitia Ofisi ya Wakala wetu wa Huduma za Ajira (TAESA) ambapo tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kabla ya mfanyakazi wa Tanzania hajatoka nje ya nchi tunafanya kwanza mawasiliano kufahamu kazi anayokwenda kufanya lakini na mkataba na malipo yake. Matatizo mengi yanakuja kwa sababu asilimia kubwa ya wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi hawapitii katika utaratibu ambao tumeuweka na ndiyo maana wakipata matatizo huwa inakuwa ngumu sana kuweza kushughulikia kwa sababu hawajapitia katika mfumo wetu na hawapo katika kanzidata yetu ya watumishi ambao wanafanyakazi nje ya nchi. Nitoe rai kwa Watanzania wote wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kufuata taratibu ili wapatapo matatizo iwe rahisi kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumza kuhusu kwenda kufanyishwa kazi kinyume na utaratibu uliowekwa, haya yote yanatokana na iwapo tu wafanyakazi hawa hawatakuwa wamepitia katika ofisi zetu. Sisi tunawabana mawakala ili waje na mikataba ambayo tutaipitia wote kwa pamoja na Ubalozi utabaki na nakala yake ili kuweza kufuatilia. Inapotokea Mtanzania anafanya kazi tofauti na ile ambayo ilisemwa katika mkataba ni rahisi kwenda kuripoti katika Balozi zetu na sisi kuweza kuchukua hatua.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved