Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Primary Question

MHE. SAADA MKUYA SALUM aliuliza:- Vituo vya Afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Wananchi vimekuwa vikitoa huduma za afya kwa wananchi wengi na kutokana na umadhubuti na umakini wa watendaji, wananchi wamejenga imani kubwa juu ya huduma zinazotolewa katika vituo hivyo; hata hivyo huduma hizo zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo mbalimbali vikiwemo uhaba wa dawa, Madaktari na vitendea kazi:- Je, Serikali imeweka mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kuwa vifaa tiba, dawa na Madaktari vinapatikana ili kutoa huduma bora?

Supplementary Question 1

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; katika mikakati ambayo imeorodheshwa ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo cha Afya cha Jeshi kilichopo Welezo ambacho kinahudumia wananchi wengi na hali yake ni mbaya sana. Kwa hiyo, hii mikakati imeorodheshwa lakini katika mwaka 2016/2017 ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; namwomba Mheshimiwa Waziri tukiondoka Dodoma tufuatane, mguu kwa mguu twende katika Jimbo la Welezo tukatembelee kituo hiki cha afya, kipo katika hali mbaya na kinahudumia wananchi wengi na wengi wanakitegemea. Kwa hivyo, akienda akiona utajua sasa ni jinsi gani anaweza kukisaidia. (Makofi)

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikakati niliyoielezea kuna baadhi ambayo imeshaanza na kuna baadhi ambayo bado tunategemea itaanza siku za usoni. Lile la Bima ya Afya ambayo kwa kweli tunadhani ndio itakuwa mkombozi wa kuboresha huduma za afya, hilo bado halijaanza, tupo katika mchakato na ni matumaini yetu kwamba likianza fedha nyingi zitapatikana ili kuweza kuboresha vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yale yaliyoanza ni msaada uliotolewa na Serikali ya Marekani na Ujerumani. Tumeshafanya ukarabati na tumenunua vifaa, lakini tumeanza na ngazi za Hospitali za Rufaa za Jeshi. Kwa sababu hata kwenye Jeshi kuna vituo vya afya, hospitali na hospitali kuu. Kwa hivyo, kazi iliyofanyika kwa mfano katika Hospitali Kuu ya Lugalo, kazi zilizofanyika katika Ali Khamis Camp Pemba, kazi zilizofanyika Mwanza na kadhalika ni kubwa na tunajua kwamba kazi hii haijakamilika kwa sababu bado kuna vituo hatujavifikia ikiwemo hicho cha Welezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tutafika, tunakwenda kwa awamu ili na chenyewe tukiboreshe wananchi pamoja na Wanajeshi waweze kupata huduma nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kutembelea katika kituo hicho, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba nipo tayari, nitakapofanya ziara ya eneo la Unguja, basi moja ya kazi zangu itakuwa ni kufuatana naye kwenda kuangalia kituo hicho.

Name

Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SAADA MKUYA SALUM aliuliza:- Vituo vya Afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Wananchi vimekuwa vikitoa huduma za afya kwa wananchi wengi na kutokana na umadhubuti na umakini wa watendaji, wananchi wamejenga imani kubwa juu ya huduma zinazotolewa katika vituo hivyo; hata hivyo huduma hizo zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo mbalimbali vikiwemo uhaba wa dawa, Madaktari na vitendea kazi:- Je, Serikali imeweka mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kuwa vifaa tiba, dawa na Madaktari vinapatikana ili kutoa huduma bora?

Supplementary Question 2

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuwajengea wanajeshi kituo kizuri cha afya pale Ali Khamis Camp Jimbo la Wawi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vitu vingi vya afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna majokofu ya kuhifadhia maiti, hata kwa Askari wenyewe pale wanapofariki kwa sababu wengine wanakaa mbali sana na maeneo ya mikoa yao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka majokofu katika vituo tofauti vya Afya vya Jeshi ili Askari wenyewe wanapofariki waweze kuhifadhiwa vizuri?Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kuna umuhimu wa kuwa na majokofu ya kuhifadhia maiti katika vituo vyetu vya Jeshi, kwa sababu vingi sasa hivi vinatoa huduma ya rufaa na bila shaka ni muhimu kuwa na majokofu hayo endapo itatokea vifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, ni kwamba lazima twende kwa awamu. Tunaanza kwenye vituo vikubwa na kazi hii tumeshaifanya pale Lugalo ni matarajio yetu kwamba kila fedha zitakapokuwa zinapatikana, basi huduma hii tutaiendeleza katika vituo vya chini. Kwa hiyo, nataka nimtoe hofu, jambo hili tunalijua na tutalifanyia kazi ili hatimaye vituo hivyo vipate majokofu ya kuhifadhia maiti.