Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y. MHE. GOODLUCK A. MLINGA) aliuliza:- Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kuwapatia wananchi wa Kata za Lupiro, Iragua, Milola na Minepa eneo la ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero kwa ajili ya makazi na kilimo pindi tu atakapoingia madarakani. Je, utekelezaji wa ahadi hiyo imefikia wapi?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa mchakato ambao unaendelea katika maeneo yale.
Swali la kwanza, kupitia huo Mradi wa KILORWEMP, wadau tulikaa mwezi Oktoba, 2016 katika Mji Mdogo wa Mikumi. Tulichokubaliana ni kwamba urejeshaji upya wa mipaka ile utazingatia ushirikishi wa wananchi. Serikali wamefanya hilo lakini changamoto hapa, tunapojadiliana, tunapokubaliana katika urekebishaji wa ile mipaka lakini wakienda site watumishi/wataalam wale wa Serikali wanagoma, wanaelekeza kuweka mipaka kama wanavyotaka wao. Kwa mazingira hayo bado wataendeleza mgogoro. Kwa nini sasa makubaliano yale na wananchi na wadau kwenye kijiji hayatekelezwi wanapokwenda kuweka upya ile mipaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali sasa mnafanya zoezi la kuondoa mifugo kwenye hifadhi kwa maeneo yale ya lile Bonde la Ardhi Oevu la Kilombero. Mifugo ile itakapotoka kule inakuja kwenye ardhi ya vijiji, ardhi ya vijiji ndiyo yenye vyanzo vya maji katika bonde lile la Kilombero. Je, Serikali mnavisaidiaje vijiji hivi kukabiliana na msukosuko huo wa ile mifugo itakapotoka kule kwenye lile bonde kuja kwenye ardhi ya vijiji? (Makofi)

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: MheshimiwaSpika, swali lake la kwanza linasisitiza juu ya umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi jambo ambalo kwenye majibu yangu ya msingi nimelifafanua kirefu kwamba kwa mujibu wa mipango ya Serikali ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kufanya uhifadhi uweze kuwa endelevu na kuweza kutimiza masharti ya sheria, kanuni na taratibu bado utekelezaji wake unaendelea kusisitizwa na kwamba Serikali itaendelea kuona umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi. Katika mradi huu wa KILORWEMP tayari tunao mpango huishi unaoitwa intergrated management plan ambao kwa mujibu wa Kanuni za Mkataba za RAMSAR Convention tunapaswa kuuzingatia.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nipokee maelezo yake ambayo nayasikia kwa mara ya kwanza hapa kwamba makubaliano yanayofikiwa katika vikao mbalimbali vilevile vya ushirikishwaji wa wananchi wakati wa kwenda kuyatekeleza kule site yanakuwa yana kasoro au yana upungufu. Hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa niaba ya Serikali tunalipokea ili tuweze kufika kule kwenye maeneo yanayohusika tuweze kuona pengine katika utekelezaji, utendaji unakuwa una kasoro. Kwa hiyo, tukifika kule tutakwenda kushirikiana kuona namna gani tunaweza kuondoa hizo kasoro ndogo ndogo zinazoweza kukwamisha dhamira kuu ya Serikali ya kuweza kufanya uhifadhi uwe na mafanikio.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili linalohusiana na uondoaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na changamoto zake, anataka kujua kwamba uondoaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa na mahsusi katika suala hili ni suala la Bonde la Mto Kilombero kwamba mifugo ile hasa ng’ombe wanapokwenda katika maeneo ya vijiji wanakwenda kusababisha changamoto nyingine ambazo na zenyewe zinakuwa ni kubwa vilevile pengine ni kubwa zaidi kuliko wanapokuwa wako kwenye hifadhi kwa mujibu wa maelezo yake.
Napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba na hili nalo ni suala vilevile la ushirikishaji wa pande zote mbili kwamba Serikali na wananchi kwa pamoja tunapaswa kufanya kazi hizi kwa pamoja kwa kushirikishana ili kila mmoja atambue umuhimu wa uhifadhi lakini katika kusimamia uhifadhi, changamoto tunazokutana nazo wakati wa kusimamia tuweze kuzitatua kwa pamoja. Kwa hiyo, katika safari hiyohiyo ninayosema tutakuja tuweze kuona nini kiko site, tutaweza kuliangalia tatizo hili la mifugo inayoondoka katika maeneo ya hifadhi ya Mto Kilombero ili tuweze kuona namna ya kutatua changamoto hizo katika maeneo ya vijiji wanamoishi wananchi.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y. MHE. GOODLUCK A. MLINGA) aliuliza:- Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kuwapatia wananchi wa Kata za Lupiro, Iragua, Milola na Minepa eneo la ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero kwa ajili ya makazi na kilimo pindi tu atakapoingia madarakani. Je, utekelezaji wa ahadi hiyo imefikia wapi?

Supplementary Question 2

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro wa Hifadhi ya Kazimzumbwi kati ya Ukonga na Kisarawe na nimshukuru Mheshimiwa wa Maliasili na Waziri wa Ardhi na Mheshimiwa Waziri Mkuu tulishakutana tukafanya mazungumzo na kulikuwa na kesi Mahakamani ambayo imekwisha. Sasa wataalam wale wa Maliasili wameenda Kazimzumbwi, wamevunja nyumba za watu, wanapiga watu, wanaharibu mali za watu katika eneo hilo. Swali langu, hawa Waheshimiwa Mawaziri wawili, wapo tayari twende pale Kazimzumbwi au hapahapa Dodoma nipo tayari kuwaita wale wahusika tukae pamoja tukubaliane kumaliza mgogoro ule ili usilete maafa katika aneo lile? Ni hilo tu.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, swali lake linafanana na maswali yaliyoulizwa na muuliza swali la msingi hapo awali, ni changamoto za utekelezaji wa usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwamba wananchi wamekuwa wakilalamika juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohakikishia Serikali kwamba tunasimamia maeneo yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Spika, changamoto moja inayojitokeza hapa ni kwamba, kwa sababu suala hili linahusisha pande mbili; upande mmoja ni Serikali ambayo inasimamia sheria, kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu yako masuala ambayo ni lazima yatekelezwe ili kuhakikisha kwamba uhifadhi unafanikiwa lakini upande wa pili ni wananchi ambao kwa maoni yao wanadhani katika kutekeleza shughuli mbalimbali za usimamizi wa hizo hifadhi upo utekelezaji ambao una kasoro kwa sababu unaleta athari kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, sasa hapa haiwezekani kupata uhalisia, ukweli na uhakika bila kwenda kwenye uhalisia wenyewe. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameuliza Mawaziri hao wanaweza kuongozana naye kwenda kuona hali ilivyo huko au wale wananchi labda kupitia viongozi wao kama wanaweza kupata fursa ya kuja Dodoma na kuweza kuonana na Waziri mwenye dhamana na Msaidizi wake wanaosimamia Maliasili.
Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwa kifupi kwamba hii ya pili itakuwa ni nyepesi zaidi kwa sababu ahadi zetu za kufika kwenye maeneo mbalimbali ambayo yana changamoto zinazohusiana na maliasili na utalii zinakuwa ni nyingi na muda unakuwa hautoshi. Kwa hiyo, kama hili la pili Mheshimiwa Mbunge anaweza kulitekeleza kwa urahisi zaidi ni jepesi zaidi. Hebu tupate viongozi kutoka huko, waje hapa na kile ambacho wanaona kwamba ni sahihi kwa upande wao halafu tutakuja hapa kuzungumza masuala haya kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa sababu suala hili la Kazimzumbwi limeshawekwa vizuri kwa mujibu wa sheria lakini kama zipo changamoto basi ni utaratibu tu wa Serikali sikivu kuweza kusikiliza wananchi wanasema nini.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hebu fanya utaratibu wa kuweza kupata viongozi wanaotoka kwenye maeneo haya wakija hapa basi mimi na Mheshimiwa Waziri tutaweza kuona namna bora zaidi ya kuweza kuwasikiliza halafu tutaweza kuona namna ya kuweza kushughulikia matatizo yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.