Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Primary Question

MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:- Gereza la Wilaya ya Kibondo – Nyamisati limekuwa na ongezeko kubwa sana la wafungwa na mahabusu kwa sababu ya uwepo wa wakimbizi. Je, Serikali haioni sasa ni wakati unaofaa kupeleka mradi mkubwa wa maji kwenye gereza hilo ili kulinda afya za raia na askari walioko kwenye gereza hilo?

Supplementary Question 1

MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu kwanza nimpe taarifa tu kwamba maji yalitoka ndani ya miezi sita tu kama na siku nane halafu mpaka sasa hivi toka 2010 lile gereza halina maji ya uhakika na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati huu mradi unatengenezwa kipindi kile tulikuwa hatuna wakimbizi sasa hivi ninapoongea 2015 tumepokea wakimbizi 120,000 na kati ya hao kuna wahalifu mbalimbali ambao nao wanatumia gereza hilo hilo ambalo kipindi hicho kulikuwa na upungufu wa lita 39,000. Tunapozungumzia kwamba maji ni uhai na kwa kuwa na idadi ya wafungwa sasa imeongezeka, Serikali ina mpango gani wa dharura hata wa kuwashirikisha UNHCR ambao ndiyo wana dhamana ya wakimbizi katika kutatua tatizo hilo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sheria inawapa kinga wafungwa wa kisiasa na wafungwa wengi ambao wanatoka kwa wakimbizi siyo wa kisiasa, ni wafungwa wa makosa ya kawaida na kwa kuwa sasa wameanza kurudishwa makwao, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuwarudisha wale wafungwa ambao wako kwenye gereza ili kupunguza idadi ya wafungwa? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ushauri wake wa kulichukulia kwa uzito unaostahili tatizo hilo ambalo yeye kwa kuwa ni Mbunge amekuwa karibu na gereza na ameona shida hiyo inaathiri vilevile wananchi la kuhusisha UNHCR ni wazo zuri na tutalichukua. Tumekuwa tukishirikiana na UNHCR kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika maeneo ambayo wilaya/majimbo/vijiji vilivyopo karibu na maeneo ya wakimbizi ikiwemo maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuoni kwa nini tusichukue na hili jambo tukaliingiza katika mpango huu hasa ukitilia maanani ni juzi tu Mheshimiwa Makamu wa Rais amezindua mpango kabambe ambao utaweza kuwanufaisha zaidi wananchi wanaohusika katika maeneo ambayo wakimbizi wanaishi. Kwa hiyo, ni wazo zuri ambalo tumelichukua kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake ya wafungwa ambao wamefungwa kwenye magereza, tuna utaratibu wa kubadilishana wafungwa katika nchi mbalimbali ambao upo kabisa kisheria na kupitia utaratibu huo hilo jambo linafanyika. Kwa hiyo, siyo jambo geni limekuwa likifanyika miaka yote tu.