Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mashimba Mashauri Ndaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Primary Question
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:- Wilaya ya Itilima ni mpya na ina eneo kubwa linalovutia kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha miundombinu ya barabara ya Migato, Nkuyu, Longalombogo, Laini, Bulombeshi na Bumera ili kuvutia watu kufanya biashara za mazao katika maeneo hayo?
Supplementary Question 1
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na barabara hizi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuna madaraja makubwa matatu kwenye barabara hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezitaja na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imekuwa ikileta bajeti yake ili iweze kuyajenga madaraja haya matatu lakini TAMISEMI wanapunguza bajeti hiyo kiasi kwamba Halmashauri imeshindwa kujenga haya madaraja matatu. Je, Serikali inasema nini juu ya madaraja haya kwa sababu yasipojengwa ni kikwazo kikubwa kwa usafiri kwa wananchi wa Wilaya ya Itilima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga daraja la Mwabasabi, ni ya mwaka juzi. Serikali inasema nini juu ya ujenzi wa daraja hilo?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakati mwingine bajeti zinakuja lakini kutokana na ukomo wa bajeti mapendekezo mengine ya Halmashauri yanakuwa yamekwama. Katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu tulivyokuwa tukipitisha hapa, tuliona ni jinsi gani Ofisi ya Rais, TAMISEMI itahakikisha inaangalia vipaumbele katika maeneo korofi hasa kuondoa vikwazo na ndiyo maana tumepitisha bajeti ya shilingi bilioni 247.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi kuangalia katika mpango wetu wa kuondoa vikwazo maeneo mbalimbali pale ambapo kuna vikwazo vya msingi katika ujenzi wa madaraja tutatoa kipaumbele. Naomba niwasihi wataalam wetu kule site waanze kufanya designing na needs assessment katika maeneo mbalimbali ili kuonyesha ni gharama kiasi gani zinahitajika katika ujenzi wa madaraja haya ambayo yatahusika. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba kama Serikali tunalichukua hili lakini katika mpango wetu wa kuondoa vikwazo tutatoa kipaumbele katika maeneo haya. Lakini suala la ahadi ya Mheshimiwa Rais, naomba niwahakikishie lengo kubwa la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba ahadi hizi zote zinatekelezeka. Naomba nimhakikishie kwamba katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani 2015 - 2020 daraja hili ni miongoni mwa maeneo ambayo tunaenda kuyajenga, lengo kubwa ni ili ahadi ya Mheshimiwa Rais iweze kutekeleza katika maeneo hayo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved