Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Primary Question

MHE. SAADA MKUYA SALUM (K.n.y MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:- Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri kiuchumi, kiafya na kisiasa na Jamhuriya Muungano wa Watu wa Cuba, lakini Tanzania haina Ubalozi katika nchi hiyo:- (a) Je, ni lini Tanzania itafungua ubalozi wake nchini Cuba hasa ikizingatiwa kuwa Cuba tayari wana Ubalozi nchini muda mrefu? (b) Je, Serikali inajua kwamba kutokana na Tanzania kutofunga Ubalozi nchini Cuba, imesababisha sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyeree kutowekwa katika uwanja wa Viongozi muhimu wa Afrika katika Jiji la Havana?

Supplementary Question 1

MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mipango inaendelea kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kufungua Ubalozi. Hata hivyo, tunaomba tu awaambie Watanzania hii mipango imefikia hatua gani ili na wao wapate confidence kwamba Ubalozi huu utafunguliwa karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa upande wa mashirikiano, Zanzibar inashirikiana kwa karibu sana na Cuba hasa katika nyanja ya afya na imekuwa ikipeleka wanafunzi mbalimbali kwa ajili ya masomo ya muda mfupi na mrefu. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuchelewa kufungua Balozi hii katika Mji wa Havana kunawapa maisha magumu wanafunzi wale kwa maana wanakuwa hawajui wanapopata matatizo wakimbilie wapi? (Makofi)

Name

Dr. Susan Alphonce Kolimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Saada Mkuya akitaka kujua hatua iliyofikiwa kwa sasa hivi. Naweza kumwambia tu utaratibu wa mwanzo huwa tunafanya kutafiti kutengeneza gharama za kuanzisha Balozi, uanzishwe wapi, watu wangapi wapelekwe, lakini mwisho kabisa ni lazima tuwe tumejiandaa kwamba tuna pesa ya kutosha na imewekwa kwenye bajeti ndipo hapo Ubalozi unaweza ukafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa pia anajua kwamba tuna Balozi nyingine sita ambazo zimefunguliwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambazo bado tunataka tuhakikishe kwamba tumekamilisha mambo yote yanayohusiana na staffing, gharama za nyumba na uendeshaji. Hatuwezi tu tukafungua kwa sababu tumesema, tukishakuwa tumejiandaa tutaweza kusema ni lini. Hata hivyo, utaratibu wa kuangalia aina ya watu watakaopelekwa na gharama za uendeshaji zimekwishakamilika, tunasubiria kwanza zile ambazo zimepangwa zikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili tunatambua kwamba mahusiano baina ya Tanzania na Cuba ni mazuri na Zanzibar kama yeye anavyojua kwamba ni sehemu pia ya Tanzania. Nataka kumhakikishia kwamba wale wanafunzi ambao wanasoma kule Cuba kwa kozi za muda mrefu na mfupi watakuwa wanaendelea kusimamiwa na Balozi yetu ya Canada maana ndiyo wanaosimamia wanafunzi au wafanyakazi wote wa Tanzania walioko Cuba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimwambie mahusiano hayo hayako mazuri tu kwa upande wa Zanzibar ni mazuri kwa Tanzania nzima. Kwa kumpa tu taarifa mwaka jana Manesi 16 pamoja na Madaktari kwa mkataba wa miaka miwili wa kutoka Cuba watakuwa wanafanya kazi katika Hospitali yetu ya Muhimbili na Waziri wa Afya yuko hapa anaweza kukiri hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mahusiano mazuri kwenye suala la elimu, kuna Madaktari na Wataalam wa afya ambao wanatoa mihadhara katika vyuo vyetu vikuu. Kwa hiyo, nataka kumhakikishia kwamba wale wanafunzi ambao wamepelekwa kutoka Zanzibar wataendelea kuhudumiwa na Balozi yetu ya Canada.