Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Naghenjwa Livingstone Kaboyoka
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:- Jimbo la Same Mashariki lina Kata 14 lakini lina Kituo kimoja cha Polisi kilichopo Kata ya Maore na vituo vidogo vilivyopo Kata ya Ndungu na Kihurio; vituo vyote hivyo vipo katika tarafa moja yenye kata tano, kata nyingine tisa ambazo zipo katika tarafa mbili zilizoko mlimani na zipo mbali sana na vituo hivyo vya Polisi zinapata shida sana kutoa ripoti za uhalifu. Kwa kuwa wananchi wa tarafa hizo mbili za mlimani tayari wametenga maeneo ya kuweka vituo vya Polisi:- (a) Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Vituo vya Polisi katika Tarafa ya Mamba/Vunta na Tarafa ya Gonja? (b) Kama Serikali ipo tayari kuanzisha Vituo hivyo vya Polisi, je, ni lini Polisi hao wataanza kazi?
Supplementary Question 1
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba Naibu Waziri aliombe Bunge lako Tukufu radhi kwa kulidanganya. Amesema Tarafa ya Gonja ina Kituo cha Polisi cha Daraja B, naomba afanye home work, tarafa hii mimi ndiyo natoka na hakuna hata Kituo cha Daraja C, sasa hicho cha Daraja B amekitoa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hata huko anakosema kipo Kituo cha Daraja C, iko nyumba haijawahi kuwekwa polisi hata siku moja. Naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri aeleze Bunge lako Tukufu kwa nini anatoa taarifa za uongo ambapo hata wananchi katika Jimbo langu watashangaa kwamba hicho kituo Daraja B, kiko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Waziri atakumbuka kwamba nimeshawaandikia Wizara yao barua mara mbili kuomba kituo hiki kilichopo Maore, Tarafa ya Ndungu ambacho kimejengwa mwaka 1959, kimechakaa ceiling board zimedondoka, vigae vilivyowekwa hata kabla ya Uhuru vimebomoka hata OCS hana mahali pa kukaa kufanyia kazi, aseme lini Serikali itaweza kukarabati kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili amesema Polisi wanafanya doria kwenye Jimbo hili, atajua kwamba Polisi wa Kituo cha Maore chenye Daraja B kama anavyosema kipo Tarafa ya Ndungu hawana hata matairi kwenye magari yao, usafiri wao ni wa shida, sasa hiyo doria wanaifanyaje? Ahsante.
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilichokieleza katika majibu yangu ya msingi, nilieleza kwamba kulingana na maeneo ambayo walileta maombi ya ujenzi wa vituo katika Tarafa ya Gonja kwamba kuna Kituo cha Daraja B sio C. Katika Tarafa ya Mamba nilichokisema ni kwamba wananchi wametoa eneo, kwa hiyo tupo katika mchakato wa ujenzi wa kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kituo cha Maore ni kweli Mheshimiwa Mbunge aliwahi kuwasilisha barua yake kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na ukarabati wa kituo hiki na barua yake tunaifanyia kazi na pale uwezo utaruhusu basi tutafanya marekebisho ya kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na ubovu wa magari kwa ajili ya doria, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba natarajia muda siyo mrefu kufanya ziara katika Jimbo lake nitamwomba na yeye kama atakuwa na nafasi tuambatane ili tukaone changamoto hizo. Tatizo la usafiri katika nchi yetu ni kubwa sana, kwa hiyo itategemea uzito tutakavyoona katika eneo hilo kulinganisha na maeneo mengine katika nchi nzima tuone uwezekano wa kusaidia usafiri ili waweze kufanya kazi zao vizuri hasa maeneo ya milimani ambapo hakuna mawasiliano mazuri ya usafiri.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved