Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:- Matatizo ya migogoro ya ardhi na Mipango Miji ni suala nyeti sana linalohitaji kutazamwa sana katika zama hizi; na hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam lakini zoezi hilo halikufanikiwa kutokana na kukosa mkakati ulioambatana na matumizi ya ramani hizo:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ramani hizo zinapatikana kwa nchi nzima ili kusaidia kuongoza matumizi ya ardhi katika miji mingi nchini? (b) Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema Serikali ingeuza Government Bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huo; Je, agizo hili limefikia hatua gani katika utekelezaji?

Supplementary Question 1

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Wizara ya Ardhi lakini bado uhitaji wa suala hili la uandaaji ramani ningeendelea kupendekeza kwamba lifanywe na Wizara ya Ardhi badala kurudishwa kwa Halmashauri kwa sababu bado Halmashauri zetu zina mbinyo mkubwa sana wa bajeti.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mipango maalum kupitia Wizara ya Ardhi kuhakikisha kwamba ramani za Mipango Miji ya jumla kwa maana ya master plan zinapatikana nchi nzima na kuacha zile detailed plan ndiyo zifanywe na Halmashauri?
Swali la pili, kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba ameacha Halmashauri zishirikiane na sekta binafsi kwa ajili ya kuandaa hizi ramani za Mipango Miji. Sitaki kukubaliana na ningependa nieleze tu bayana kwamba katika kuliachia Halmashauri zetu suala hili linafungulia mianya ya rushwa na wananchi wengine kushindwa kumudu gharama, kwa sababu sasa hivi ukipeleka mchoro wako binafsi au kuomba mchoro binafsi unaambiwa wewe mwenyewe ndiyo uugharamie mpaka na kikao cha Halmashauri kikae kwa gharama ya mwombaji kupimiwa eneo la ardhi. Je, Serikali haioni kwamba inafungua mianya rushwa na kuwafanya wananchi washindwe kabisa kupata huduma hii kwa ufanisi?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba nakubaliana naye katika swali lake jinsi alivyouliza, kwa sababu taratibu zinazoendelea mpaka sasa suala zima la upangaji miji ni jukumu la Halmashauri zenyewe. Napingana naye kwenye suala la kusema kwamba Wizara ifanye kazi hii. Wizara kazi yetu ni kusimamia sera na tunaposimamia sera maana yake tunafanya ufuatiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukumbuke mwaka 2016 Waziri alitoa ramani kama kuleta chachu kwenye Halmashauri zetu zote ili waweze kufanya jukumu hilo ambalo ni la kwao kama mamlaka za upangaji miji. Mara nyingi kama wananchi kule na hasa kwenye maeneo ya vijiji Wenyeviti wa Mitaa kama hawatambui maeneo yao migogoro inakuwa mingi. Kwa hiyo, nitoe rai tu kwa Halmashauri kuendelea kutekeleza jukumu lao la kuandaa zile ramani na baadaye kuzishusha mpaka kwenye maeneo ya vijiji na mitaa kule ili wale wenye dhamana kule waweze kuchukua jukumu lao la kuelimisha watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zoezi linaloendelea la urasimishaji kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 37 (d)(4) ambapo urasimishaji unaendelea, bado zoezi la kugawa linatakiwa liendelee katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge akubaliane kwamba Wizara haiwezi kupora mamlaka ya Halmashauri isipokuwa tutaendelea kuwakumbusha ili watimize wajibu wao. (Makofi)

Name

Joyce John Mukya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:- Matatizo ya migogoro ya ardhi na Mipango Miji ni suala nyeti sana linalohitaji kutazamwa sana katika zama hizi; na hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aligawa ramani za maeneo ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam lakini zoezi hilo halikufanikiwa kutokana na kukosa mkakati ulioambatana na matumizi ya ramani hizo:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ramani hizo zinapatikana kwa nchi nzima ili kusaidia kuongoza matumizi ya ardhi katika miji mingi nchini? (b) Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema Serikali ingeuza Government Bond ili kupata fedha za kugharamia mradi huo; Je, agizo hili limefikia hatua gani katika utekelezaji?

Supplementary Question 2

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarehe 31Januari, 2018 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dokta Kigwangala alitoa ilani kwenye kiwanja Namba 4091 kilichopo eneo la Njiro Mkoa wa Arusha kwamba wale watu ni wavamizi, wamejenga eneo la Serikali la kiwanja kinachoitwa kwa jina la Tanzania Tourist Corporation.
Swali langu, kwa nini Mheshimiwa Kigwangalla Waziri wa Maliasili na Utalii asikutane na watu hawa kwa sababu watu hawa pia ni wamiliki halali eneo lile kwa sababu wana hati pia na licha ya hivyo haoni kama huu ni uzembe wa Serikali yenyewe na je, kwa nini wasimtafute aliyehusika kufanya ili kabla hajawahukumu wananchi waliojenga katika eneo lile?(Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ametoa hilo tamko ametoa siku 30 kwa wale watu waliovamia wajisalimishe waje zile documents halali ili kusudi Serikali iweze kutathmini na kuangalia kama kweli hayo maeneo wameyapata kihalali. Kwa hiyo, siku 30 baada ya hapo ndipo tutafanya uamuzi unaostahili.(Makofi)