Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Zuberi Mohamedi Kuchauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Primary Question
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:- Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana unaohusu eneo lenye ukubwa wa ekari 357.5 Boko Dovya – Kawe – Kinondoni baina ya wananchi na watu wanaojitambulisha kuwa wamiliki halali wa eneo hilo maarufu kama SOMJI; wananchi katika hatua mbalimbali wamepeleka malalamiko Serikalini kuanzia ngazi ya Wilaya, Wizara ya Ardhi na hata kwa Waziri Mkuu lakini mpaka sasa hakuna utatuzi uliofanyika. Je, hatua gani zimeanza kuchukuliwa ili kero hiyo ya muda mrefu imalizike?
Supplementary Question 1
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nataka kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kuridhisha.
Lakini kwa niaba ya wananchi wa Dar es Salaam na hasa wa hili eneo la Kawe, huu mgogoro ni wa muda mrefu sana. Kama ambavyo Naibu Waziri anasema anataka kushirikisha sasa jamii kuona namna ya kuwapa fidia wale wamiliki wa mwanzo mimi naomba kwamba ushughulikiaji wa suala hili Mheshimiwa Naibu Waziri bado ni mdogo sana. Sasa nataka tu nipate majibu ya uhakika kwamba Mheshimiwa Naibu Wziri unawahakikishia nini watu wa Kawe juu ya upatikanaji wa ardhi ili waweze kuondokana na adha hii ya upatikanaji wa ardhi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili la migogoro ya ardhi Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hii alishawahi kutuletea taarifa Wabunge hapa Bungeni kwamba tuorodheshe migogoro mingi kwenye majimbo yetu, lakini asilimia kubwa ya migogoro ile bado haijashughulikiwa, nini kauli ya Serikali juu ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza tunawahakikishia nini wananchi hawa ili kuwapa maeneo mengine waweze kuwa na makazi. Nadhani kwenye jibu la msingi nimeeleza wazi, kwa sababu eneo lile walilivamia na kulikuwa na mashauri mahakamani na bado wananchi wale wakaonekana ni wavamizi. Hata hivyo kwa busara ya Serikali, kwa sababu tulishaona eneo lile limevamiwa kwa kiasi kikubwa, Wizara ikaamua kuwarasimishia, kwa hiyo walitakiwa kurasimishiwa ili waendelee kuwepo pale na wamiliki maeneo yale, lakini wale wananchi hawako tayari kurasimishiwa. Na tukumbuke eneo lile kisheria si la kwao, ni wavamizi na mahakama ilishatamka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama wao hawatakuwa tayari kwa zoezi ambalo Serikali imetaka kuwasaidia ili warasimishwe pale basi utaratibu mwingine Serikali haitasita kuchukua kwa sababu mahakama ilishatoa maamuzi na Serikali imeona iwasaidie kwa kuwarasimishia na wao wakae pale kihalali. Kwa hiyo, hatutakuwa na mpango mwingine nje ya pale waliponapo, kwa hiyo kama ni maeneo mengine itabidi wagharamie wenyewe kwenda kununua na waweze ku-settle kama ambavyo tunatoa viwanja kwa watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anaongelea habari ya migogoro; ni kweli tuliorodhesha migogoro mingi na iliundwa Kamati ya Wizara zaidi ya tano na migogoro ile imekuwa ikishughulikiwa katika kila Wizara na migogoro ambayo ilikuwa inaelekea kule, lakini tayari kuna ushauri ambapo kuna kamati iliundwa kwa ajili ya kutoa ushauri wa namna ya kuwa na ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ile na tayari Kamati ile ilishamaliza kazi yake, italetwa mtaona namna ambavyo tunakwenda kushughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa migogoro mingine yote ambayo ilikuwa ndani ya uwezo wa Wizara husika, moja wapo ikiwa ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Maliasili na Utalii; wote tumeshiriki pamoja na wenzetu ambao walikuwa wameandaliwa kufanya kazi hiyo.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Wizara inafanyia kazi na muda si mrefu mtapata ufumbuzi wa kudumu ambao umepangwa kwa ajili ya kuondokana na migogoro hiyo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved