Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Venance Methusalah Mwamoto
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza (a) Je, kuna wachezaji wangapi wa nje wanaoruhusiwa kucheza kwenye Ligi Kuu Tanzania? (b) Je, tulianza na wachezaji wangapi miaka ya nyuma na sasa wako wangapi? (c) Je, ni zipi sababu za kuongeza au kupunguza wachezaji na ni nini manufaa yake?
Supplementary Question 1
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda naomba usikilize vizuri kwa sababu ni kiwanda hicho. Kwa kuwa ligi bora duniani ni Uingereza na ndiyo ligi yenye wachezaji wengi wa kigeni kuliko ligi nyingine lakini timu ya Taifa ya Uingereza ni moja ya timu mbovu ambazo zinashindwa kufanya vizuri kwa kuwa ina wageni wengi. Ligi bora katika Afrika Mashariki ni Tanzania, lakini kwa kuwa inawachezaji wengi wa kigeni timu ya Taifa imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu. Kwa kuwa mwaka 2000 wakati tukiwa hatuna wachezaji wengi wa kigeni timu yetu ilifikia rank ya kimataifa ya 65 na leo tumeongeza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni tumefikia kwenye rank ya 139. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuendelea kuruhusu wachezaji wengi wa kigeni ni kuua timu yetu ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanuni za TTF ziko wazi ili timu ishiriki Ligi Kuu lazima iwe na kiwanja, ikate bima kwa ajili ya wachezaji wake na iwe na timu ya under 20 vyote hivyo vinakiukwa. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siwezi kupingana naye kwamba ongezeko kubwa la wachezaji wa nje linaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya soka ndani ya nchi. Katika jibu langu kwa swali la msingi nimesema kati ya mwaka 2010 mpaka 2015 tulikuwa tunaruhusu wachezaji watano wa nje na baadaye ndipo tumeruhusu wachezaji saba. Ukiangalia wenzetu Kenya wao walianza na saba na sasa hivi wanaruhusu watano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini uzoefu tulioupata katika msimu huu ni kwamba tulikuwa na timu 16 kwenye Ligi Kuu na timu zote kikanuni zinaruhusiwa kusajili wachezaji 30 na kati ya hao saba wanaweza kuwa wanatoka nje. Wadau wanasema kwa kweli hii saba ni ukomo tu na mara nyingi ukomo huo hatuufikii.
Vilevile kwa nchi ambayo tayari imekubali professional football huo wigo wa saba siyo mbaya hata kidogo. Ni kweli timu zote hizo 16 zingesajili wachezaji saba kwa mfano tungekuwa na wachezaji wa kulipwa nchini 112 lakini mwaka huu ni wachezaji 35 tu ambao ni asilimia saba ya wachezaji wote. Kwa sababu timu 16 mara wachezaji 30 kama 480 kwa hiyo ni asilimia saba tu ndiyo ambao waliweza kuajiriwa kutoka nje. Kwa hiyo, ni ukomo tu na usitutie wasiwasi hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, timu zilizofanya vizuri sana katika ligi hii Mheshimiwa Mwamoto unaelewa zilikuwa hazina wachezaji kutoka nje. Chukulia timu ya Kagera Sugar ambayo ilikuwa ya tatu ilikuwa haina mchezaji kutoka nje, chukulia Mtibwa ilikuwa namba tano ilikuwa haina mchezaji yeyote kutoka nje. Vilevile mimi mwenyewe nimehusika katika utoaji zawadi kwa ajili ya wachezaji waliokuwepo kwenye Vodacom Premier League, wachezaji waliofunga magoli kwa kiwango cha juu na kupata zawadi walikuwa ni wawili mmoja kutoka Ruvu Shooting Stars (Abdulrahman) na mwingine kutoka Yanga (Msuva) wote ni Watanzania, hakuna mchezaji wa nje. Kwa hiyo, nimshawishi Mheshimiwa Mwamoto akubali tu kuwa na wigo wa wachezaji saba ila tu tusiongeze wakawa wachezaji kumi na kuendelea huko, lakini hii idadi inatosha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, umeongelea kuhusu timu zinazoshiriki kwenye ligi yetu kuu kwamba zingine nadhani hazina vigezo kwa mfano kuwa na vijana wa under 20 na zingine hazina viwanja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kwamba timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu sharti lao lazima ziwe na timu za vijana chini ya umri wa miaka 18 siyo under 20 actually. Kwa sababu hawa wanaosajiliwa 30 ni umri wa miaka 18 na kuendelea lakini lazima uwe na timu ya vijana ya miaka 18 ambapo tunaruhusu vijana watano kushiriki kwenye Ligi Kuu. Vilevile naomba tu baadaye aniambie ni timu gani ambayo haina kiwanja inachezea barabarani kufanya mazoezi.
Name
Mussa Ramadhani Sima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza (a) Je, kuna wachezaji wangapi wa nje wanaoruhusiwa kucheza kwenye Ligi Kuu Tanzania? (b) Je, tulianza na wachezaji wangapi miaka ya nyuma na sasa wako wangapi? (c) Je, ni zipi sababu za kuongeza au kupunguza wachezaji na ni nini manufaa yake?
Supplementary Question 2
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwa kuwa Tanzania ina wachezaji wachache sana wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na kwa kuwa vijana wetu wa Serengeti Boys Under 17 walionesha kiwango kikubwa sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kwa vijana hawa ili tuwe na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba timu yetu ya Taifa ya Serengeti imefanya vizuri sana katika historia ya nchi yetu na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sima kwamba juhudi za Serikali sasa hivi ziko katika maeneo mawili. Moja ni kuhakikisha timu hii tunaendelea kuilea kwa sababu hawa ndiyo wawakilishi wetu katika michuano yetu ya olympiki mwaka 2020, kwa hiyo hatuwezi kuwaacha tunaendelea kuwalea kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nimhakikishie kwamba tuko kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali, tumepata watu wengi nje ambao sasa hivi tunashirikiana kwa karibu kama Sport Pesa na timu ya Everton FC ambayo iko Premier League ya Uingereza ambao tuna mahusiano mazuri, tumeanza kuongelea kuhusu uwezekano wa kuweza kuchukua baadhi ya vijana wetu. Hayo ni mazungumzo bado hatujapata guarantee nisije nikasikia kesho magazeti yakesema sasa wanakwenda huko, tuko kwenye mazungumzo na tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nikuhakikishie Mheshimiwa Sima katika kipindi changu cha uongozi wa Wizara hii sitaruhusu kijana yeyote kwenye timu ya Serengeti achukuliwe na timu ambayo ina historia ya uchovu uchovu kiweledi hata kipesa na mimi mwenyewe nitasimamia katika kuangalia mikataba yao. Niwahakikishie tunawaangalia vijana wetu na wataendelea kutusaidia katika kuinua jina letu kwenye ulimwengu wa soka. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved