Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:- Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Charles Kitwanga alikaririwa na vyombo vya habari mwezi Desemba, 2015, akiliagiza Jeshi la Polisi kumkabidhi majina ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ambazo ongezeko lake nchini lina athari hasi dhidi ya vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa:- (a) Je, ni hatua gani zimechukuliwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani katika kuwabaini, kuwachunguza na hatimaye kuwafikisha Mahakamani wale wote waliobainika kujihusisha na mtandao wa biashara za dawa za kulevya? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wanaojiingiza kwenye dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya nchini? (c) Je, ni vijana wangapi kwa nchi nzima ambao kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita wamepatiwa tiba kusaidiwa kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya?

Supplementary Question 1

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwanza ningependa kutambua jitihada kubwa sana zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli katika vita dhidi ya madawa ya kulevya na ningependa kuwatia moyo na waweze kuendelea na jitihada hizi. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuweka katika mitaala ya elimu ya msingi pamoja na sekondari mafunzo kuhusu athari ya dawa za kulevya?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, hawa vijana 3,000 waliopatiwa tiba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa kushirikiana na wadau, je Serikali inafahamu vijana hawa wako wapi katika muda huu, yaani kwa sasa na wanafanya nini?(Makofi)

Name

Prof. Joyce Lazaro Ndalichako

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Answer

WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ningependa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainab Katimba kuhusiana na kipengele cha mpango wa Serikali kuweka kwenye mitaala masuala ya madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Spika, ningependa kusema kwamba mitaala ya kuanzia shule za msingi, Sekondari pamoja na masuala ya kitaaluma lakini pia inakuwa imebeba masuala mtambuka. Kwa hiyo, masuala yanayohusiana na masuala ya madawa ya kulevya, masuala ya jinsia, masuala ya UKIMWI yapo katika mitaala yetu na tutaendelea kuyaimarisha ili kuhakikisha kwamba tunaenda sambamba na azma ya Serikali ya kupambana na hili janga la madawa ya kulevya nchini. Ahsante.