Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stephen Hillary Ngonyani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Primary Question
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:- Katika Jimbo la Korogwe Vijijini yako mashamba ambayo tangu yabinafsishwe hayajaendelezwa:- (a) Je, ni lini mashamba hayo yatagawiwa kwa wananchi kwa sababu hayaendelezwi? (b) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuyatoa kwa wananchi mashamba ambayo hayaendelezwi ili kuwapa fursa ya kuyatumia kwa shughuli za kilimo?
Supplementary Question 1
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye maana. Mwaka jana mwezi wa Sita niliomba Serikali iende mpaka Korogwe ikaangalie maeneo ambayo hayaendelezwi na Serikali iliniahidi kwamba ingekwenda kule na kukagua mashamba ambayo hayaendelezwi ili ufanywe utafiti wa kuwagawia wananchi, hadi leo hii na mimi nilienda kwenye mikutano ya hadhara na kuwaambia wananchi kwamba Naibu Waziri atakuja kuangalia mashamba ambayo hayaendelezwi na watu wakakipa sana kura Chama cha Mapinduzi kwa kujua kwamba viongozi wanafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hawajafika na badala yake nasikitika sana baadhi ya Watumishi wa Halmashauri wanaleta habari ambazo siyo njema, zisizoweza kumsaidia mtu wa aina yeyote. Naomba Waziri, ni lini mimi na wewe tutakwenda mpaka Korogwe Vijijini ukaone huku kudanganywa kwamba ni shamba moja katika mashamba 17 yanayozunguka Jimbo langu hayajapatiwa ufumbuzi.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niseme kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitia swali la Mheshimiwa Ngonyani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa kama kila Mbunge atataka Waziri afike kwenye eneo lake na kufanya utambuzi wa mashamba zoezi la ukaguzi wa mashamba haya yasiyoendelezwa halitafikia ukomo. Hata hivyo, najua wazi kwamba ni jukumu la Halmashauri zetu husika ambapo na Wabunge ni Wajumbe kuweza kuyatambua hayo mashamba na Wizara inapofika pale, inakuja baada ya kuwa imepata taarifa ili kujihakikishia kwamba kilicholetwa ni sahihi, tutafika pia kukagua, lakini hatuwezi kufanya ile kazi ya mwanzo, unakwenda kila eneo kukagua halafu ndiyo uweze kuchukua hatua, maana utashindwa kuchukua maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Halmashauri husika ilete mapendekezo halafu Mheshimiwa Waziri apeleke kwa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya ubatilisho. Maamuzi ya matumizi yanafanyika ndani ya Halmashauri kwa sababu ndiyo wenye mamlaka pia ya kugawa mashamba hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu zoezi hili Mheshimiwa Waziri alishalitolea maelekezo na alitoa barua katika maeneo yote, ni jukumu letu sasa kuanza kukagua yale mashamba tuliyonayo ambayo Halmashauri zetu imeyatoa. Hivyo, Wizara inarahisisha kazi baada ya kuwa imeshapata kutoka kwenu, sisi tutakuja kutambua ili sheria zisikiukwe na kuleta malalamiko kwa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Ngonyani iwapo itabidi, basi tutafika, lakini kazi hii ni kazi ya Halmashauri.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved