Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Grace Victor Tendega
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Kuna uhaba wa nyumba za kuishi walimu licha ya juhudi za wananchi kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari; walimu hao pia wanahitaji kujenga nyumba zao wenyewe za kudumu. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kutoa mikopo kwa walimu ili wajenge nyumba zao binafsi?
Supplementary Question 1
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kabisa yanaonyesha jinsi ambavyo walimu wetu wamekuwa wakikosa nyumba za kuishi, walimu wa sekondari 52,000 hawana mahala pa kuishi na walimu 130,300 wa shule za msingi hawana nyumba za kuishi. Tumesema tunataka kuwa na elimu bora katika nchi yetu na hatufahamu walimu wanaishi wapi.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka sasa wa kuamuru Jeshi la Polisi liweze kujenga nyumba hizi za walimu kama walivyofanya kwa Mererani kuzuia ile migodi yetu, tatizo hili ili liweze kuisha kwa haraka?
Swali la pili, walimu wamekuwa wakikosa udhamini katika mabenki mbalimbali kwa kutokuwa na mali za kudhaminiwa na taasisi alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ni hizo ambazo huwezi kudhaminiwa kama huna dhamana ya vitu visivyohamishika kama viwanja, magari na vitu vingine na tunatambua hali za walimu wetu zilivyo.
Je, sasa Serikali haioni haja kwamba ni wakati muafaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iweze kuwa dhamana kwa walimu wetu wakati bado wakiwa kazini na siyo baada ya kustaafu? Ahsante. (Makofi)
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nisisitize kwamba katika jibu langu la msingi ile takwimu niliyoitaja kwa faida ya Bunge lako tukufu haikumaanisha kwamba walimu hao hawana makazi kabisa. Nimesema kwamba walimu hao wanaishi katika aidha, nyumba za kupanga au nyumba zao binafsi, hilo ndilo jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ya swali lake kwamba kwa nini Serikali isiamuru Jeshi la Polisi kujenga nyumba za walimu nchi nzima, hilo ninaomba sana majeshi yetu yana kazi zake maalum ambayo yamepewa kufanya na waliojenga ukuta wa Mererani siyo Jeshi la Polisi ni Kitengo cha Ujenzi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Tumekuwa tukiwapa kazi nyingi sana, SUMA JKT kujenga nyumba za walimu kujenga nyumba za walimu katika mahali pengi. Hata kwake kule Iringa tumewapa sehemu nyingi tu SUMA JKT kujenga nyumba na tutaendelea kuwapa mikataba ya kujenga nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwamba ujenzi wa nyumba ambao unafanywa na Serikali utaendelea kuwa kidogo kidogo kwa sababu unategemea sana bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, napenda nimuondoe wasiwasi kuhusu dhamana. Karibu mabenki yote na taasisi zote zinazokopesha hakuna dhamana zaidi ya mshahara wa mtumishi. Kinachotakiwa tu ni kwamba mtumishi asiwe anadaiwa mikopo mingine hilo ndiyo jambo la msingi, kama mtumishi hadaiwi mikopo mingine anao uwezo wa kukopa na ataamua mwenyewe, je, akope kwa kurejesha miaka mitatu au akope kwa kurejesha miaka 10 au akope kwa kurejesha miaka 25 ni yeye mwenyewe katika makubaliano ya fomu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuwasisitiza watumishi wote nchi nzima na Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wako chini yangu nataka niwaambie kwamba mikopo hiyo ya watumishi ipo, waingie makubaliano maalum na hizo taasisi na mabenki ili kusudi watumishi waweze kukopesha waweze kujenga nyumba zao binafsi. (Makofi)
Name
Eng. James Fransis Mbatia
Sex
Male
Party
NCCR-Mageuzi
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Kuna uhaba wa nyumba za kuishi walimu licha ya juhudi za wananchi kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari; walimu hao pia wanahitaji kujenga nyumba zao wenyewe za kudumu. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kutoa mikopo kwa walimu ili wajenge nyumba zao binafsi?
Supplementary Question 2
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa maendeleo ya Taifa lolote lile yanatokana na mifumo yake ya elimu inayojali utu wa binadamu; na kwa kuwa Walimu ni sehemu muhimu sana katika uzalishaji wa maendeleo endelevu katika Taifa letu.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga fungu maalum la fedha hata kama ni kukopa ili kuondoa kero hizi katika sekta ya elimu ikiweko nyumba za walimu? (Makofi)
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbatia ambaye ni mkereketwa mkubwa sana wa sekta ya elimu napenda nimhakikishie kwamba mawazo yake ni sawa tu na mawazo ya Serikali. Hivi karibuni tumekamilisha kukokotoa gharama zinazohitajika kuweza kukamilisha miundombinu inayohitajika katika sekta ya elimu ili tuanze utekelezaji kwa asilimia 100 wa Sera yetu ya Taifa ya Elimu ya mwaka 2014, hilo analoliongea ni mojawapo ya yale ambayo tumeyaingiza katika hizo gharama na gharama za awali katika rasimu inaonyesha wazi kwamba tunahitaji takribani trilioni 13 ili kuweza kukamilisha miundombinu yote inayohitajika.
Naomba Mheshimiwa Mbatia na Bunge lako Tukufu liweze kuwa na subira, tutakapokamilisha tutafanya majadiliano maalum ili tuweze kupata fedha zinazohitajika kwa sekta ya elimu. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved