Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Njalu Daudi Silanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Itilima
Primary Question
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:- Shirika la Nyumba lilianzishwa kwa ajili ya kusaidia watumishi wa umma pamoja na wananchi wenye maisha ya chini na Mkoa wa Simiyu ni mpya ambapo tayari kuna watumishi wengi ambao hawana nyumba za kuishi ikiwemo Wilaya za Itilima na Busega:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba katika Mkoa mpya wa Simiyu pamoja na wilaya zake kwa kutumia Shirika la Nyumba?
Supplementary Question 1
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kulingana na uchache Halmashauri ya Wilaya ya Itilima haukuweza kupata shilingi milioni 400 kwa wakati. Tuliweza kujenga nyumba nne kwa kutumia utaratibu kwa kutumia mikataba ya halmashauri na Naibu Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Kandege alikuja kufungua hizo nyumba. Je Waziri atakubaliana nami kuangalia utaratibu mpya na wa masharti ya ujenzi wa nyumba za watumishi hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miji mingi nchini imekuwa ikikua kwa kasi bila mpangilio. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na halmashauri hapa nchini ili kuweka upimaji ikiwemo Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla?
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Njalu tukutane huko nje tufahamishane namna gani mahitaji yake namna gani anaweza tukajenga hizo nyumba, lakini ajue Shirika la Nyumba limewekwa kwa mujibu wa sheria lazima lifanye biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tulivyokubaliana kwamba wangekuwa wanatenga pesa halafu tunawajengea nyumba. Shirika la Nyumba ujenzi wake wa gharama za ujenzi ni nafuu kuliko contractor yoyote, Shirika la Nyumba ni contractor wa daraja la kwanza. Hata hivyo, kwa kujua ni Shirika la Nyumba la Serikali gharama za ujenzi ni nafuu na ubora wa nyumba zake ni mzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, labda tujadiliane huko nje kitu gani wamekwama badala ya kujenga nyumba 13 wanataka wajenge ngapi halafu tujue namna ya kushirikiana. Kwa kweli hatuwezi kujenga nyumba bila kupewa pesa Shirika la Nyumba haliwezi kwa sababu itabidi likope fedha benki liende kujenga nyumba zao. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Njalu kwa hili la nyumba tuwasiliane baadaye ili tuone jambo gani wamekwama, tuweze kushirikiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili upimaji kabla ya kupima Mji wa Itilima lazima ifanywe master plan na bahati nzuri Bariadi wameshafanya master plan. Kama tatizo ni utaalam, sisi tuko tayari kuwaazima Wataalam wa Mipango Miji wawasaidie Itilima namna ya kuandaa master plan, halafu baada ya master plan then sasa lije zoezi lingine la upimaji na upangaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kama halmashauri yoyote haina Wataalam wa Serikali wa upangaji na upimaji wasipate tatizo. Serikali imeshasajili makampuni ya upangaji na ya upimaji ya Wataalam wabobezi ambao tumewasajili na tumewapa ruksa ya kufanya kazi hizi kama wenzao wa ujenzi wanavyofanya kazi nyingine za ujenzi wa barabara na majengo.
Mheshimiwa Naibu Spka, kwa hiyo, halmashauri kama haina Wataalam isikae ikisubiri Wataalam wa Serikali tunayo makampuni ambayo yanaweza kuwasaida wananchi wa Itilima kupanga mji wao, kupima hadi umilikishaji. Kwa hiyo, tunaweza tukawasaidia Wataalam, lakini pia halmashauri inaweza ku-engage Wataalam binafsi kampuni binafsi wakafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, yote mawili yanawezakana kufanywa kwa Itilima.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved