Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Ingawa kuna tatizo la ajira Serikalini, lakini inasemekana kuwa ziko nafasi nyingi zilizo wazi katika ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya hata Vijiji:- (a) Je, ni kwa nini Serikali inalificha jambo hili na ni lini sasa itajaza nafasi za ajira zilizo wazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu katika sekta za Utawala kama vile VEO, WEO ambapo wananchi huwalipa watumishi wa kukaimu kwa fedha zao wenyewe kinyume na taratibu? (b) Je, ni kwa nini Serikali isipandishe mishahara ya kima cha chini kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya sasa?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili.
Kwanza, kwa kuwa mipango hii ya bajeti tunayoijadili sasa hivi katika Bunge letu inahitaji sana kada hizi za Watendaji na kwa kuwa nafasi nyingi katika kada hizi ziko wazi, je, ni kwa nini Serikali isione umuhimu mkubwa wa kutoa nafasi kwa wale vijana waliomaliza Vyuo vya Serikali za Mitaa na Vyuo vya Utawala, wakaanza kujitolea katika kipindi hiki cha mpito kutegemeana na makubaliano yao katika Serikali za Mitaa hususan kwenye maeneo yao, ili baadaye waweze kuingia katika mfumo wa ajira?
Pili, ni kwa nini sasa Serikali isione inapaswa kutenga fedha za kutosha katika kuwezesha ofisi za Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa sababu fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika ngazi za chini zinatumika kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uendeshaji katika ofisi hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issaay ambapo katika suala lake la kwanza alitaka kujua kwamba ni kwa nini Serikali isitoe fursa au nafasi kwa hawa WEO na VEO ambao wanajitolea katika kipindi hiki cha mpito.
Mheshimiwa Naibu Spika suala zima la kujitolea au la liko mikononi mwao katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Kwa hiyo, nitoe tu rai kwa Mheshimiwa Mbunge, mipango hiyo wanaweza wakaifanya na kuitekeleza huko chini kabisa katika Mamlaka zao za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika kama ambavyo nimesisitiza, ni kutokana tu na ufinyu wa nafasi na wigo wa kibajeti, katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo nilieleza tumepanga kuajiri ajira mpya, nafasi 71,496 na katika nafasi hizo kwa ujumla wake katika WEO na VEO na nafasi zinginezo kwa upande wa Mbulu watapata nafasi 466, vile vile tutawapandisha vyeo katika promotion nafasi 1066. Kwa hiyo, nimwombe tu waendelee kuwa wavumilivu kipindi hiki na kama nilivyoeleza mwezi huu wa Tano ajira hizo zitaanza kutekelezwa na ni imani yangu watatekeleza kwa wakati, ili nafasi hizo ziweze kuzibwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kwa nini sasa Serikali isiweze kutenga fedha za kutosha kuziwezesha Kata hizi ziweze kufanya kwa ukamilifu niseme tu kwamba, mipango ya kibajeti kutokana na uwezo tulionao, Halmashauri zenyewe zinashirikishwa katika mpango mzima wa maandalizi ya bajeti. Kwa hiyo, niwaombe tu wahakikishe kwamba wanapokuwa wanapanga mipango yao wanaweka vipaumbele katika kuziwezesha Kata hizi kuwa na fedha ambazo zitaweza kufanya majukumu yao ya msingi, lakini kwa sasa inawezekana zisitoshe kabisa na ni kutokana na wigo wa bajeti.