Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yahaya Omary Massare
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Primary Question
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:- Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi kusaidia kupunguza gharama kubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, pia kulipa mishahara yote ya watumishi, mgao wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), vifaa tiba na kuongeza Madaktari Bingwa:- • Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? • Je, Serikali haioni kuwa kwa sasa ni bora kujenga hospitali ya Serikali katika Halmashauri mpya ya Itigi?
Supplementary Question 1
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Nishukuru majibu mazuri ya Serikali yenye dhamira ya kuona sasa wananchi wanapatiwa huduma ambazo zinakidhi. Kwa kuwa, Serikali imeona busara hii na kutoa ruzuku kwa Hospitali hii ya Mtakatifu Gaspar lakini gharama zake ni juu sana na sasa Serikali imeona ni vizuri ianze kujenga hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Itigi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika kutekeleza Ilani ya CCM tunazo changamoto ambapo Serikali imetuletea pesa za kujenga kituo cha afya lakini gari la Kituo cha Afya ni dogo, wakati huo huo kuna Kituo cha Afya cha Mitundu ambacho ni kilometa zaidi ya 100 kutoka kituo cha afya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Manyoni iliyopo sasa. Je, Serikali iko tayari kutoa gari la wagonjwa kusaidia kituo kile ili kupunguza gharama za wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kituo cha Afya Rungwa ambacho kiko zaidi ya kilometa 200 kimeshakamilika. Je, Serikali iko tayari sasa kukifungua kituo hiki?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anaongelea juu ya suala zima la upungufu wa magari kwa maana ya ambulance kwa ajili ya kituo cha afya alichokitaja ambacho anasema kipo karibia kilometa 100. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba inapunguza adha kwa wananchi hasa wagonjwa, ndiyo maana gari zinapopatikana zimekuwa zikitolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale magari yatakapokuwa yamepatikana tutaanza kupeleka maeneo yenye uhitaji mkubwa hasa yale ambayo yanahitaji kutembea umbali mrefu. Naamini na hicho alichosema Mheshimiwa Mbunge nasi pia tutazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaulizia juu ya utayari wa Serikali kufungua kituo cha afya kilichokamilika. Essence ya kujenga kituo cha afya ni ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi. Serikali kama mambo yote yamekamilika tuko tayari kuzindua kituo hicho cha afya. (Makofi)
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:- Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi kusaidia kupunguza gharama kubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, pia kulipa mishahara yote ya watumishi, mgao wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), vifaa tiba na kuongeza Madaktari Bingwa:- • Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? • Je, Serikali haioni kuwa kwa sasa ni bora kujenga hospitali ya Serikali katika Halmashauri mpya ya Itigi?
Supplementary Question 2
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itazuia wagombea Urais kutoa ahadi ambazo zinachukua muda mrefu kutekelezeka ikiwepo suala la zahanati na barabara? (Makofi/Kicheko)
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, wagombea nafasi za Urais wanaenda kuuza sera kwa wananchi ili kwa sera hizo waweze kuchaguliwa. CCM ambao ndiyo tulichaguliwa na wananchi baada ya kuuza sera na ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais na katika kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais mkataba wake na wananchi waliompa kura ni miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shuhuda, tumekuwa tukipata fursa ya kujibu maswali juu ya maeneo mbalimbali ambayo ahadi za Mheshimiwa Rais zilishatekelezwa. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuzuia ahadi hizo kwa sababu zimekuwa zikitekelezwa. (Makofi/Kicheko)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved