Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Martha Jachi Umbulla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:- Changamoto ya fedha za mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya kwa makundi ya wanawake na vijana nchini ni urejeshaji hafifu pamoja na kutorejeshwa kwa fedha hizo kabisa; kuna taasisi za fedha hapa nchini zinatoa mikopo kwa makundi tajwa hapo juu kwa ufanisi mkubwa na kwa uzoefu wa muda mrefu:- Je, kwa nini Serikali isipitishe utoaji wa mikopo hiyo kwenye taasisi hizo zenye ufanisi wa muda mrefu na watalaam wa kutosha kama WEDAC ili kuepusha upotevu wa fedha za Serikali na mikopo kuwafikia walengwa?
Supplementary Question 1
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa walengwa wa mikopo hii ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri zetu wanapewa kwa makusudi ya kufanya biashara ili waweze kuzirejesha baada ya kupata faida. Je, walengwa hawa ambao ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wametayarishwa kwa kiasi gani ili waweze kuelewa masharti ya mikopo hiyo, aina ya biashara wanazopaswa kufanya, lakini zaidi sana elimu ya ujasiriamali kwa sababu mwishowe watahitajika kurejesha kwa faida? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kutokana na majibu ya Naibu Waziri kwamba malengo ya kutoa mikopo hii ni kuwapa watu wa hali ya chini sana katika nchi yetu; na kwa kuwa kuna baadhi ya kaya maskini hapa nchini ambazo zinaongozwa na wanaume pia ambao wanahitaji msaada, je, Serikali ina kauli gani kuhusu kaya hizo ambazo zinaongozwa na wanaume ambao wanahitaji pia kupata msaada kutokana na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zetu?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la elimu, ni ukweli usiopingika, maana wanasema kwamba, ‘mali bila daftari hupotea bila taarifa,. Ni wajibu wa Maafisa Ushirika na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata elimu juu ya kuanzisha biashara na namna nzuri ya kuweza ku-keep record ili wajue hicho kiasi ambacho wanakopa kinatumikaje ili waweze kurejesha kwa wakati kitumike kwa wengine.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba elimu inatolewa. Si elimu tu peke yake lakini amekuwa akisimamia mfuko ambao umekuwa ukifanya vizuri katika eneo la Mkoa wa Manyara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili, ni imani yetu kwamba pale ambapo unamwezesha mama unaiwezesha familia. Ni matarajio yetu kwamba akina mama katika mikopo hii wanayopata hawawaachi waume zao pembeni, kwa hiyo tunakuwa tunaiwezesha familia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba pale ambapo kuna ushirikiano kati ya baba na mama hakika familia hiyo husimama. Ni matarajio yetu kwamba baada ya kuwatosheleza akinama tutatizama pia upande wa akina baba kama haja itakuwepo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved