Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Magdalena Hamis Sakaya
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Primary Question
MHE. JOHN P. KADUTU (K.n.y. MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:- Serikali ilianzisha Wakala wa Misitu (TFS) kwa lengo la kuhifadhi misitu, kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali ya misitu:- Je, ni kwa kiasi gani Maafisa wa Misitu walioko Mikoani, Wilayani wameweza kuokoa misitu inayozidi kuteketea hapa nchini?
Supplementary Question 1
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa; Serikali imetoa matangazo na kuweka vibao kuhalalisha masoko ya mazao ya misitu maeneo ambayo hakuna mashamba ya misitu, wakijua kabisa kwamba misitu inayovunwa wale wavunaji wanavuna visivyo halali. Kwa mfano, ukitoka Dodoma ukiwa unaelekea Morogoro kuna vibao kwamba kuna masoko halali, lakini wale watu kule hakuna mashamba ya misitu, wanavuna kwenye maeneo ambayo siyo halali na hawana namna nyingine, hawajaelimishwa namna gani wapande misitu ili wavune mazao ya misitu kwenye maeneo ambayo yamepandwa. Je, Serikali haioni kwamba, kuweka masoko ya mazao ya misitu maeneo ambayo hakuna mashamba ya misitu ni kuhalalisha kuendelea kuhakikisha kwamba misitu iliyopo ya asili inateketea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la la pili; kwa kuwa kwenye majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri anasema kwamba misitu imepandwa. Kuna baadhi ya misitu ya uoto wa asili imepandwa lakini tumeshuhudia kazi wanayofanya Maafisa Misitu maeneo yetu, ikiwepo Kaliua ni kupiga mihuri magogo, kupiga mihuri mbao na kutoa vibali kwa ajili ya uvunaji usio halali kiasi kwamba speed ya kuvuna misitu baada ya kuwepo kwa TFS imeongezeka tofauti ya ilivyokuwa mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, je, Serikali haioni kwamba kuna sababu ya kukaa na Maafisa wao wa Misitu ili sasa waanze kazi ya uhakika ya kurejesha uoto wa asili ikiwepo maeneo mbalimbali kwa sababu Kaliua kuna misitu mingi lakini hakujapandwa mti hata mmoja kuhakikisha kwamba tunarejesha uoto wa asili maeneo ambayo yameharibika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nikiri kabisa kwamba kweli kumekuwa na matumizi mabaya ya misitu yetu katika maeneo mengi na vituo vingi vipo katika maeneo ambayo kwa kweli hakuna misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuwepo kwa sehemu ya kituo hata kama hakuna msitu siyo tatizo, tatizo ni kwamba ule mkaa unaouzwa katika lile eneo je, una kibali na umepatikana katika taratibu zilizowekwa. Kama haujapatikana kwa mujibu wa utaratibu hilo ndilo linakuwa tatizo kubwa lakini kama vibali vipo na mkaa umesafirishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine maadam una vibali hilo linakuwa siyo tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo tutaendelea kulifuatilia pale ambapo watu wanafungua vituo wanaweka masoko bila vibali maalum Serikali itachukua hatua zile zinazostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu hawa Maafisa Misitu ambao wapo maeneo mengi na wamekuwa hawatekelezi labda majukumu yao sawasawa na kama ulivyosema wamekuwa labda wanagonga mihuri tu zile mbao, kwa kweli naomba nitumie nafasi hii kuwaagiza Maafisa Misitu wote kuhakikisha wanasimamia hifadhi zetu zote zilizoko katika maeneo yao, mihuri inayotakiwa kutolewa ni pale ambapo wale wavunaji wamevuna katika ile misitu wanayoisimamia, kwa mujibu wa taratibu kwa mujibu wa sheria na kanuni tulizojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wakiwa wamefuata hizo taratibu na wakigonga haina shida, shida inakuwa pale wanapopita njiani humu halafu wanagonga hiyo mihuri wakati wao wenyewe hawajui hizo mbao zimetoka sehemu gani. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua zinazostahili, kwa wale ambao watakuwa wanakiuka hizi taratibu ili kusudi hifadhi zetu ziendelee kuwepo hapa nchini. (Makofi)
Name
Munde Abdallah Tambwe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOHN P. KADUTU (K.n.y. MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:- Serikali ilianzisha Wakala wa Misitu (TFS) kwa lengo la kuhifadhi misitu, kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali ya misitu:- Je, ni kwa kiasi gani Maafisa wa Misitu walioko Mikoani, Wilayani wameweza kuokoa misitu inayozidi kuteketea hapa nchini?
Supplementary Question 2
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, katika Mkoa wa Tabora kumekuwa na kero kubwa ya kuwapiga, kuwanyang’anya baiskeli zao, kuwajeruhi, kuwanyang’anya simu zao na pesa walizonazo mfukoni wanaobeba mkaa kutoa vijijini kuleta mjini. Je, Mheshimiwa Waziri ni haki mtu anapofanya kosa kuchukuliwa hatua kupigwa hapo hapo bila kupelekwa kwenye vyombo vya sheria? (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Answer
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto hizo, katika maeneo mengi nchini, watu wamekuwa wakinunua mkaa na wamekuwa wakisafirisha kwa baiskeli, wamekuwa wakisafirisha kwenye bodaboda na vyombo vingine ambavyo kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani haviruhusiwi kufanya hivyo. Pale ambapo wanakuwa wamekiuka hizo taratibu wanatakiwa wakamatwe, wapelekwe katika vituo, wapelekwe katika mikondo ya sheria siyo kuwapiga. Wale ambao wanaowapiga wananchi bila ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, ni ukiukaji wa taratibu na ukiukaji wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaombe watendaji wote kokote waliko nchini wahakikishe wanazingatia sheria na kanuni na miongozo iliyopo na wahakikishe wanawatendea haki wananchi ili kusudi wasinyanyaswe na kupigwa. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved