Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stephen Julius Masele
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Primary Question
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:- Wananchi wakazi wa Kijiji cha Ishokelahela, Misungwi, Mwanza, wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kihalifu, kinyama na kikatili na Vyombo vya Dola kuwaondoa katika makazi yao na kuacha kuchimba dhahabu ili eneo hilo libaki kwa Mwekezaji anayetaka kuwaondoa kwa nguvu kinyume cha sheria:- i. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu vitendo hivyo wanavyofanyiwa wananchi hao? ii. Je, Serikali iko tayari kuunda timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mgogoro huo na kuchukua hatua stahiki ambazo zitamaliza kabisa mgogoro na kuwawajibisha wote ambao wamesababisha hali iliyopo sasa?
Supplementary Question 1
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mwezi wa Kwanza mwaka huu wakati Serikali ikijibu swali langu kuhusu wachimbaji hawa wadogo ilisema kwamba inatambua vikundi ambavyo nilikuwa nimewahamasisha wachimbaji hawa kuviunda na itawapatia maeneo ya kuchimba. Hata hivyo, baada ya mwezi mmoja Serikali hii hii ilienda kuwazuia wasichimbe na sasa Waziri ananiambia kwamba tena nihamasishe kwamba waunde vikundi vingine, ni vikundi gani tena hivyo? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kutatua hii migogoro kwa sababu naona kama wanakwepa kwepa na wamekuwa na ndimi mbili mbili kuhusu huu mgogoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, malalamiko ya wananchi ni kuhusu huyu mwekezaji ambaye anamiliki eneo kubwa ambalo lina ukubwa wa ekari 2,250, lakini ameshindwa kuliendeleza na wananchi hawa wana nia njema kabisa ya kuliendeleza na Serikali ilikiri mbele ya wananchi kwamba mwekezaji huyu ameshindwa kuliendeleza eneo hili. Je, Serikali itatekeleza lini hii ahadi yake ambapo ilisema kwamba ingemnyang’anya huyu mwekezaji hiyo leseni na kuwapatia wananchi na si kutumia nguvu kwa ajili ya kutatua migogoro? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba maswali ya Mheshimiwa Mbunge yana logic, lakini niseme tu kitu kimoja kwamba kuunda kikundi ni hatua moja lakini kumiliki kihalali ni hatua nyingine. Kwa hiyo kile ambacho Mheshimiwa Mbunge alishauriwa na ambacho ndicho msimamo wa Serikali ni kwamba hao vijana wakishakaa kwenye vikundi wanatakiwa pia wafanye zile taratibu za kuweza kumilikishwa kihalali na wakishamilikishwa ndio watakuwa wamekamilisha utaratibu wa kuweza kuchimba kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu mwekezaji anayesema anamiliki eneo kubwa, nalo hilo lina taratibu zake naamini Wizara husika watakapokuwa wamejiridhisha na taratibu zile kukamilika kwenye maelekezo waliyokuwa wameyatoa basi wanaweza wakachukua hizo hatua.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa majibu mazuri. Nimwombe tu ndugu yangu Mheshimiwa Susanne Maselle tuweze kuonana ili kuweza kulipata suala hili kwa kina na kuona namna gani tunaweza tukalitatua. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved