Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Primary Question

MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:- Sumbawanga ina Wilaya mbili ambazo ni Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini:- Je, kwa nini ina Mkuu wa Wilaya mmoja?

Supplementary Question 1

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi anavyomudu nafasi yake na anavyochanganua majibu mbalimbali. Hata hivyo, nataka kumshauri aiangalie sana ofisi yake inayotoa majibu ya maswali, ni jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameelekeza taratibu tunazotakiwa kuzifuata na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilishazifuata, Mikutano ya Vijiji, Mikutano ya Madiwani, Mikutano ya DCC, Mikutano ya RCC na vigezo vipo na Bunge linajua hivyo na tulishaomba. Nataka aniambie ni lini wananchi wale watapata Wilaya mpya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, haoni kwamba kitendo cha kuunganisha Wilaya, Sumbawanga Mji na Sumbawanga Vijijini ambazo jiografia zake ni ngumu kunamfanya Mkuu wa Wilaya asiweze kumudu nafasi yake na hatimaye wananchi wa Wilaya wa Sumbawanga Vijijini kucheleweshwa kimaendeleo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu zetu za kitakwimu zinatuonesha Halmashauri ya Wilaya hii ambayo anazungumzia Mheshimiwa Mbunge, ukiiachia Sumbawanga Mjini kwa vigezo vya kijiografia kwa ukubwa wake ina square meter 1,300 ambapo kwa Wilaya inatakiwa iwe na square meter 5,000 lakini halmashauti iliyobakia ina square meter 8,000. Kwa hiyo, ukizi-combine maana yake hapa unapata equivalent ya Wilaya mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naomba nikiri wazi, Wabunge wengi sana wanasema wengine wamewasilisha taarifa, ndiyo maana wiki mbili zilizopita nimeagiza, baada ya Mheshimiwa Shangazi kuja ofisini kwangu kwa ajili ya Jimbo lake la Mlalo kuhusiana na suala hili, nikasema nimewaagiza wataalam wangu kuniletea orodha za halmashauri na wilaya zote ambazo zimeleta mapendekezo yao. Nia yangu ni tuweze kubaini ni wilaya ngapi zilipeleka maombi ili kama hazijakidhi vigezo vile tuweze kuwapa marejesho ni mambo gani wanatakiwa kuyarekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Malocha aniamini kwa sababu amesema wameshawasilisha haya yote, nitakwenda kufuatilia kwenye orodha ambayo nimeagiza. Tukiona kwamba kila kitu kiko sawa au kama kuna marekebisho ambayo yanatakiwa yafanyike tutawasiliana kwa sababu wananchi lengo lao kubwa ni kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini suala hili litatekelezwa. Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tukishajua hatua iliyofikiwa, tutaona jinsi gani tutafanya kuhusiana na suala hili la Sumbawanga Mjini na Vijijini. Bahati nzuri ofisi yetu iko chini ya Mheshimiwa Rais mwenyewe, tutamshauri ipasavyo kwamba watu wa Sumbawanga kwa jiografia yao ilivyokuwa ngumu, Wabunge wanapata shida sana kutoa uwakilishi mzuri katika maeneo yao, basi Sumbawanga wapate maeneo ya kiutawala.

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:- Sumbawanga ina Wilaya mbili ambazo ni Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini:- Je, kwa nini ina Mkuu wa Wilaya mmoja?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa Naibu Waziri amejibu kwamba kuna uwezekano mkubwa kabisa wa kupata halmashauri ndani ya Wilaya moja na kwa kuwa mchakato wa wilaya ni mrefu kidogo na mchakato wa kupata halmashauri uko ndani ya uwezo wake na kwa kuwa Jimbo la Mlimba lina kata 16 na urefu wa kilometa 265 kutoka Jimboni mpaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, ni lini Wizara italipa hadhi ya kiwango cha halmashauri Jimbo la Mlimba ili angalau tuanze sasa kujitegemea wenyewe kwa sababu vigezo vyote tunavyo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumzia Jimbo la Mlimba nadhani akiwa na maana pamoja na Ifakara kwamba eneo lake ni kubwa. Kuanzisha halmashauri kwa mujibu wa vigezo vyetu lazima iwe na kata 15, hicho ndiyo kigezo cha kwanza. Kwa hiyo, kama mna kata 16 maana yake tulitarajia kwamba angalau kata ziongezeke. Tukiachia vigezo hivyo, kuna vigezo vingine vya jiografia maana kuna maeneo mengine kata zinaweza kuwa chache lakini mtawanyiko wa jiografia yake unakuwa ni mkubwa zaidi kama kwa akina Mheshimiwa Keissy kule ndiyo malalamiko ambayo kila siku wanayazungumza hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu ni kwamba, kama mtakuwa mmekidhi vigezo tutafanya mchakato, lakini mwisho wa siku, wataalam wetu lazima watakuja field ku-assess uhalisia wa maeneo hayo yakoje. Lengo letu ni nini kama Serikali? Lengo letu ni kwamba katika maeneo ambayo wananchi wanatakiwa wapate huduma waweze kupata huduma. Kwa hiyo, thibitisho langu kwako ni kwamba, kama mtakuwa mmekidhi vigezo na wataalam wakija ku-verify wakiona kwamba vigezo hivi vimetimizwa na matakwa ya kisheria na taratibu zote zikishakamilika, basi Ofisi ya Rais, TAMISEMI haitosita kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya wananchi wa Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hapo tu, kutokana na jiografia ya Mkoa wa Morogoro hata watu wa Morogoro Kaskazini wana-issue kama hiyo hiyo. Kwa hiyo, naamini kwamba maeneo yote ambayo yataonekana kwamba yana kila haja ya kugawanywa, basi Serikali itaangalia, lakini wakati huo huo tutaangalia suala zima la kibajeti jinsi gani Serikali itaweza kuzihudumia hizi mamlaka mpya ambazo tutakwenda kuzianzisha.