Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Primary Question

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:- Zao la Korosho pamoja na kuingiza mapato makubwa Serikalini bado lina changamoto nyingi sana katika uuzaji wake kwa upande wa Wakulima:- Je, Serikali ipo tayari kuondoa changamoto hizo ili kuleta tija kwa Wakulima?

Supplementary Question 1

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna changamoto moja ameiacha katika Korosho ambayo ni changamoto ya malipo kwamba mpaka leo Serikali inasuasua kuwalipa Wakulima waliouza Korosho zao. Wapo Wakulima ambao wamepeleka Korosho zao ghalani lakini wamelipwa pesa ambayo haikidhi au hailingani na kiwango walichopeleka. Lakini pia wapo Wakulima ambao mabodi display zinaonesha kwamba wamelipwa tayari lakini wakienda benki pesa hizo hazipo, kwa hiyo kuna malipo hewa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kujua Serikali kwa nini haielezi ukweli juu ya malipo ya Korosho kwa Wakulima wa Korosho.

Mheshimiwa Spika, swali la pili nilikuwa naomba kujua kwamba Serikali imekusanya Korosho hizi zikawekwa kwenye maghala Mtwara na Lindi na maeneo mengine na Korosho zinahifadhiwa haizidi miezi mitatu, Korosho zimeanza kuota hivi sasa zingine. Je, Serikali haioni kwamba inalitia hasara Taifa hili kwa kuziweka Korosho hizi bila kuzibangua?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Nachuma. Kwanza sisi kama Serikali au Taasisi ya Serikali iliyopewa jukumu hili bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko tunalipa pesa kwa wakulima, na mpaka jana kiasi cha Korosho tulizokusanya ni zaidi ya tani laki mbili kumi na tatu na tumeshafanya uhakiki zaidi ya tani laki moja na ishirini na tisa na tani laki moja na kumi na sita ndizo tulizozilipa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ajue kufahamu kwamba malipo hatuwezi kuanza kulipa kabla ya kujiridhisha katika uhakiki na pesa hii niwahakikishie kwamba pesa zipo na mimi mwenyewe na Mheshimiwa Waziri Mkuu tumetoka juzi huko ambao kulikuwa kweli na changamoto hasa kwenye malipo ya daraja la pili ambao mwanzo pale tuliona mkazo kuanza daraja la kwanza lakini kuanzia jana wameanza kulipwa pia na Korosho daraja la pili hasa Mikoa ya Pwani na Mikoa ya Tanga.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazungumzia kuhusu hasara ambayo kwa kuweka Korosho muda mrefu, kwanza ni kweli Korosho sio kama zabibu kwa sababu zabibu ukiiweka muda mrefu ndio ukali wake unaongezeka lakini Korosho kila unavyoiweka ubora wake unazidi kushuka. Hilo tunalifahamu na ndio maana tumeshaingia mikataba na wabanguaji wa ndani wameshaanza kubangua na sasa hivi tuko kwenye mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kuuza tani zaidi ya laki mbili kwenye masoko ya Kimataifa muda sio mrefu Korosho zitaanza kusafirishwa nje ya nchi.

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:- Zao la Korosho pamoja na kuingiza mapato makubwa Serikalini bado lina changamoto nyingi sana katika uuzaji wake kwa upande wa Wakulima:- Je, Serikali ipo tayari kuondoa changamoto hizo ili kuleta tija kwa Wakulima?

Supplementary Question 2

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, asante nilitaka kuuliza swali la nyongeza, suala la ununuzi wa Korosho unaendana sambasamba na ulipaji wa wadau wanaoshiriki katika suala zima la Korosho, ununuzi unaoendelea mpaka sasa hivi halmashauri hazijapewa pesa yao ya ushuru hata senti tano. Nilitaka kuiuliza Serikali yangu, kwa kuwa Serikali imeamua kununua Korosho ni lini italipa ushuru wa halmashauri ili Bajeti zetu ziende kama tulivyozipanga?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Ghasia Mbunge wa Mtwara Vijijini, kwanza ni kweli kuna watoa huduma mbalimbali katika zao la Korosho, na sisi kama Serikali tuliona mwanzoni kutokana na mkanganyiko uliokuwepo tuliweka mkazo zaidi kulipa kwamba wakulima kabla ya watoa huduma.

Mheshimiwa Spika, na mpaka sasa tulishalipa wakulima zaidi ya asilimia 59 sasa hivi tumeshaanza kulipa na watoa hudma wengine wakiwemo hao watu wa halmashauri, mpaka jana tulishalipa zaidi ya bilioni nne kwa wasafirishaji lakini tumeshalipa watunza maghala zaidi bilioni sita na tushalipa pia watoa huduma wengine wasambazaji wa magunia zaidi ya bilioni nne nukta nane.

Kwa hiyo na hiyo ya Halmashauri tunaifahamu tushawaambia watu wa vyama vikuu na vyama vya msingi watunze rekodi zao vizuri wote tutawalipa kwa sababu halmashauri na Serikali kuu wote ni wadau katika hili, Serikali kuu export levy na hawa hizo fedha za halmashauri zote Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi zipo kwenye mikakati na tutazilipa. Lakini la mwisho, nitoe ufafanuzi katika hili, ni kweli Serikali tunanunua Korosho lakini sio kwamba Serikali yenyewe ndio inanunua Korosho ni Taasisi ya Serikali ya Bodi ile ya nafaka ya mazao mchanganyiko ndio inayonunua Korosho, kama zinavyofanya biashara Taasisi zingine kama TTCL na zingine sio Serikali kuu.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA aliuliza:- Zao la Korosho pamoja na kuingiza mapato makubwa Serikalini bado lina changamoto nyingi sana katika uuzaji wake kwa upande wa Wakulima:- Je, Serikali ipo tayari kuondoa changamoto hizo ili kuleta tija kwa Wakulima?

Supplementary Question 3

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza pamoja na maelezo mazuri ya Serikali itakumbukwa kwamba siku nne tano zilizopita Mheshimiwa Waziri Mkuu alikiri kwamba zoezi la uhakiki limegubikwa na vitendo vya rushwa. Sasa ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali kuwachukulia hatua wale ambao wameshiriki zoezi hili na kujihusisha na vitendo vya rushwa, ambayo kwa kweli kwa sehemu kubwa ndiyo imevuruga zoezi hili na kulikosesha maana na matokeo yake wakulima wameathirika sana.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kabla ya kujibu hili swali, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kwa kuniteua katika nafasi hii na kuniamini kwamba naweza kufanya kusaidia katika maendeleo.

Pia nichukue nafasi kuwashukuru viongozi wengine wote wanaomsaidia Mheshimiwa Rais lakini pia, wewe Mwenyewe Mheshimiwa Spika kwa malezi mazuri, ambayo ndiyo yamenifanya nifikie katika nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nimjibu Mheshimiwa Nape Nnauye kama ifuatavyo, ni kweli kabisa kwamba wakati tunaendelea na hili zoezi la uhakiki katika maeneo mengi kumekuwa na maneno katika baadhi ya maeneo kwamba baadhi ya viongozi na baadhi ya wafanyakazi ambao wako kwenye Kamati za uhakiki wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa. Sisi kama Wizara tuliposikia tu hatukusubiri tupate ushahidi, tuliposikia baadhi ya wafanyakazi wanashiriki kwenye rushwa tumechukua hatua na naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwenye upande wa Wizara na bodi zake.

Mheshimiwa Spika, wafanyakazi wanne tumeshawachukulia hatua tumeshawasimamisha na hivi sasa tunakusudia kuwapeleka Mahakamani kutokana na kudhihirika kwamba wamejihusisha na vitendo vya rushwa. Lakini pia kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wako TAMISEMI ambao tunawasiliana ndani ya Serikali ili nao waweze kuchukuliwa hatua zinazokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kusema kwamba Serikali haitavumilia wafanyakazi wote ambao watakuwa wanajihusisha na vitendo vya rushwa na pale ambapo Waheshimiwa Wabunge mnazo takwimu au mmepata taarifa kwamba mfanyakazi wetu yeyote anajihusisha na rushwa tunaomba mtupatie hizo taarifa na kama Serikali tutachukua hatua mara moja. Ahsante.