Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rev. Peter Simon Msigwa
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:- Ili kuharakisha upimaji na urasimishaji wa ardhi na makazi, Serikali iliruhusu kampuni binafsi kufanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali. (a) Je, ni lini kampuni zinazofanya kazi hiyo zitatoa hati za ardhi au leseni za makazi kwa wananchi? (b) Je, ni vikwazo gani vinakabili zoezi hilo na Serikali inachukua hatua gani kuviondoa ili kuzisaidia kampuni hizo kumaliza kazi hiyo kwa haraka? (c) Je, ni lini Serikali itakamilisha mpango kabambe (masterplan) mpya ya Jiji la Dar es Salaam ili uwe dira katika upangaji, upimaji na urasimishaji?
Supplementary Question 1
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Sugu alivyosema mnasema hatupongezi lakini katika hili nimpongeze Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu atleast wamefika maeneo mengi kufanya kazi yao vizuri. Kwa hiyo, kwa mazuri yanayofanyika sisi tunapongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ni mawili. La kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kwa sasa hakuna changamoto, nakubaliana kwa sehemu zimeondoka lakini malalamiko makubwa ya kampuni binafsi ni kwamba hawapati ushirikiano kwa watendaji wa Serikali kwa sababu wanaona kwamba wanachukua kazi zao. Kwa hiyo, wanapotoa taarifa kuomba vibali wale watendaji wakati mwingine wanawazunguka wanakwenda kuchukua kazi zao kwa sababu wanakuwa kama intruders kwenye kazi zao, Serikali itatatuaje tatizo hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, Mheshimiwa Lukuvi mwaka juzi alizindua masterplan katika Manispaa ya Iringa na tulikuwa Manispaa ya kwanza kuzindua masterplan jambo ambalo ni jema, nimesema nalipongeza na tumeendelea kufanya kazi vizuri. Hata hivyo, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa ametangaza katika Manispaa ya Iringa watu wajenge wanavyotaka hata kuingilia maeneo ya CBD. Je, Serikali inasemaje? Tumsikilize nani kati ya Waziri au Mkuu wa Mkoa? Bado niseme nawapongeza ningeomba nipate majibu ya Serikali kuhusiana na jambo kama hili.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amezungumzia habari ya wapimaji binafsi ambao hawapati ushirikiano. Tatizo hilo hatujalipata kama Wizara na lengo la kuwaweka wao ni kuhakikisha kwamba upimaji unaongezeka. Sasa kama suala ni kuongeza kasi halafu wanapata vikwazo, tunahitaji tupate uthibitisho wa hayo ili tuweze kuyafanyia kazi lakini kwa sasa hatujapata malalamiko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la masterplan na Mheshimiwa RC kuingilia kazi hiyo, naomba kusema kwamba hilo pia nalo hatujalipata lakini masterplan ndiyo kiongozi wa kupanga miji kama ilivyo na Iringa kweli mmekuwa wa kwanza. Kwa hiyo, tunachosema masterplan ikishapitishwa inahitaji kutekelezwa kama ilivyo na siyo vinginevyo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved