Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ussi Salum Pondeza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chumbuni
Primary Question
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:- Wananchi wa Kisakasaka, Mkoani Mjini Magharibi Unguja wamekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na Kambi ya Jeshi la Wananchi na hivyo kuathiri shughuli zao za kiuchumi:- (a) Je, Serikali imechukua hatua gani kumaliza mgogoro huo? (b) Je, ni sababu gani zimesababisha mgogoro huo kudumu zaidi ya miaka 40? (c) Je, ni lini Taasisi husika za Serikali zitakaa pamoja na kumaliza mgogoro huo?
Supplementary Question 1
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina swali moja dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upimaji wa pili wa mipaka uliofanywa mwaka 1985 uliingia mpaka katika maeneo ya wananchi ambapo wamechukua eneo kubwa la wananchi. Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa ile mipaka mipya imeingia ndani ya maeneo ya wananchi ambao walikuwepo pale tangu miaka 1960 tofuati na ile mipaka ya mwaka 1978. Je, Serikali ipo tayari kuwaachia maeneo yao yale ya mwanzo kwa mipaka ile ya mwaka 1978 kwa sababu mipaka ya mwaka 1985 imeingia katika makazi ya wananchi?. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutuhakikishia jambo hili ili migogoro hii iweze kuisha?
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri mimi mwenyewe nimetembelea eneo hilo la Kisakasaka na nilipata maelezo ya kina juu ya mgogoro huu. Kilichopo ni kwamba wananchi wanadai eneo ambalo wao wapo ni la kwao wakati Jeshi wanadai walikuwepo muda mrefu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kuna wakati CDF Mstaafu, Jenerali Mwamunyange, alikwenda pale; na katika kulimaliza tatizo hili, alitoa agizo la kurekebishwa kwa mipaka ili wananchi waliokuwa ndani ya Kambi ya Jeshi wawe nje. Kazi hiyo ilifanyika lakini bado wananchi wale hawajaridhika na utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyosema awali, tunaunda Kamati au Tume ndogo itakayopitia matatizo ya migogoro ya ardhi katika Zanzibar nzima, kwa sababu siyo hapa tu, kuna maeneo mengi yana migogoro; ili tuweze kupata ufumbuzi wa kudumu. Kwa wale wanaostahili fidia, watalipwa fidia na wale ambao hawana haki, basi watalazimika kuyaachia maeneo hayo ili Jeshi liweze kufanya shughuli zake.
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:- Wananchi wa Kisakasaka, Mkoani Mjini Magharibi Unguja wamekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na Kambi ya Jeshi la Wananchi na hivyo kuathiri shughuli zao za kiuchumi:- (a) Je, Serikali imechukua hatua gani kumaliza mgogoro huo? (b) Je, ni sababu gani zimesababisha mgogoro huo kudumu zaidi ya miaka 40? (c) Je, ni lini Taasisi husika za Serikali zitakaa pamoja na kumaliza mgogoro huo?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na wananchi, kama alivyosema ipo nchi nzima, lakini nimekuwa nikizungumzia utatuzi wa mgogoro kati ya Jeshi la Wananchi na Mtaa wa Bugosi na Kenyambi kule Tarime ambao umedumu kwa muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri anaelewa; ni lini sasa Serikali itaona kwamba imeshindwa kupata fedha za fidia kuwalipa hawa wananchi, ukizingatia Jeshi la Wananchi limetoka kwenye Kambi yao, limekuja kwenye makazi ya wananchi?
Mheshimiwa Spika, kama hakuna fedha, tunaomba warudishe hii ardhi kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao za maendeleo. Ni lini Serikali itawarudishia ardhi wananchi hawa wa Tarime?
Name
Dr. Hussein Ali Mwinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwahani
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna tatizo la mgogoro wa ardhi katika eneo hili la Tarime la muda mrefu, ninayo taarifa hii, tumeshazungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Mbunge. Wataalam wameshauri na tathmini ya fidia imefanyika, kinachosubiriwa ni fedha ili ziweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, katika mwaka huu wa fedha, bajeti yetu ilikuwa ni shilingi bilioni 20 katika kulipa fidia na upimaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali. Bahati mbaya sana tumepokea kama shilingi bilioni tatu ambazo tumeshazilipa kule Kilwa, lakini mwaka wa fedha haujaisha, tuna matumaini kwamba fedha zitapatikana na zikipatikana tutaendelea kulipa katika maeneo haya ambayo uhakiki umeshafanyika.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Esther avute subira, ajue kwamba Jeshi nalo lina umuhimu wa kuwepo maeneo haya. Katika ulinzi wa nchi lazima tuone umuhimu wa taasisi hii ya Jeshi kuwepo. Siyo vizuri au siyo rahisi tu kusema kwamba kila ambapo tunashindwa kulipa fidia kwa wakati, basi Jeshi liondoke wananchi warudishiwe ardhi; ulinzi utafanywa na nani? Kwa hiyo, naomba subira iendelee na bila shaka tutalimaliza tatizo hili kwa haraka iwezekanavyo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved