Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:- Barabara kutoka Ifakara hadi Mlimba mpakani mwa Mkoa wa Njombe (Madeke) ni kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Mlimba:- Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu umeshafanyika kuanzia Ifakara mpaka Kihansi; na kwa kuwa barabara hiyo hakuna kabisa sehemu ambayo unaweza ukapata changarawe kwa sababu upande wa kulia ni bonde oevu na upande wa kushoto ni Udzungwa. Je, Waziri husika yupo tayari kuongea na Waziri mwenzake wa Maliasili ili wakandarasi hao wanaotengeneza hiyo barabara ingawaje kwa kiwango cha changarawe waweze kupata kifusi au moramu katika eneo ambalo watalitenga kwenye eneo la Udzungwa? Nasema hivyo kwa sababu ni udongo tupu na hii barabara inabomoka kwa muda mfupi sana na wananchi wanapata tabu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa pale Mlimba Mjini, TARURA kwa bajeti zao wanasema wataweka angalau kilometa 1 kiwango cha lami lakini kuna mita 500 za TANROADS zinazopita kwenda pale mjini. Je, TANROADS sasa wako tayari kwenye ile barabara yao pale Mlimba Mjini hizo mita 500 kuunganisha na ile lami ya Kihansi, Mlimba Mjini ili TARURA wanapofanya kazi yao kusiwepo na kipande kingine cha vumbi pale Mlimba Mjini, kwenye mji wa Mlimba?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Kiwanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu tulipata nafasi ya kutembelea barabara hii na changamoto ya kupata changarawe ili kuifanya barabara iwe bora zaidi tuliizungumza na tulikuwa tumefanya mazungumzo na wenzetu upande wa Maliasili. Hata hivyo, kwa vile amelisema tena hapa nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya mazungumzo ili tuweze kupata kibali cha kifusi ambacho kitafanya barabara hii matengenezo yake yawe imara.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la kipande cha mita 500, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nalichukua ili niweze kulielekeza upande wa wenzetu wa TANROADS, Mkoa wa Morogoro ili kilometa 1 itakayotengenezwa na TARURA iwe na muunganiko mzuri na hizi mita 500, hii nimelichukuwa.