Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joyce Bitta Sokombi
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:- Mara ni mkoa ambao una makundi makubwa ya jamii ya wafugaji, wakulima na wavuvi lakini kwa sasa kuna shida kubwa ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji:- Je, ni lini wafugaji watapatiwa eneo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao?
Supplementary Question 1
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilitegemea swali hili lingejibiwa na Wizara ya Mifugo na Kilimo lakini limejibiwa na TAMISEMI, kwa vile Serikali ni moja naamini tatizo la Mkoa wa Mara linaenda kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu idadi ya ng’ombe nina mashaka nayo, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wafugaji wengi wageni toka sehemu mbalimbali wanaingia mkoani kwa ajili ya malisho kwa kufuata mbuga. Malisho ni shida sana katika Mkoa wa Mara, Mkoa umeelemewa na ndiyo sababu kubwa sana Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na wakulima na wafugaji kuna mgogoro mkubwa sana. Kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuweka sheria ya kuwasaidia wafugaji hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama, Bunda na Musoma Vijijini zimesahaulika ndio zenye wafugaji wengi sana na hakuna sehemu za malisho. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa elimu kwa wafugaji hawa ili wafuge ufugaji wa kisasa ili kuweza kujikwamua katika mahitaji yao ya kila siku?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joyce Sokombi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namuomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi kama alivyosema Serikali ni moja, ulipozungumza habari ya Halmashauri na vijiji unazungumza TAMISEMI lakini pia tunafanya kazi pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kwamba mambo yanaenda sawasawa. Kwa hiyo, swali lipo sehemu sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la msingi anasema idadi ya ng’ombe ina tatizo, sisi tumejiridhisha kwamba idadi hii ni kamili kwa sababu sensa imefanywa na Serikali na ni data kamili labda kama ana taarifa nyingine tofauti na hizi tutamkaribisha tu-compare notes.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli baada ya kuona kwamba kuna shida kubwa ya malisho na migogoro mingi ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima ameunda timu ya Mawaziri wanane wanaendelea na vikao vyao maeneo mahsusi yamependekezwa na wadau wameshirikishwa, Tarime, Serengeti, Bunda na maeneo mengine nchi nzima yatatengewa maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mpango huo kukamilika na taarifa kupewa Mheshimiwa Rais ataona itakavyofaa ili kuruhusu baadhi ya maeneo yawe kwa ajili ya wafugaji na wakulima na tunaamini baada ya zoezi hilo migorogoro ya wakulima na wafugaji itakuwa imefikia ukomo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anazungumzia kuhusu kutoa elimu, nimemsikiliza mara kadhaa hapa Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mpina na Mheshimiwa Ulega wametoa taarifa mara nyingi na mipango mbalimbali na ni kweli kwamba wafugaji wetu wanashauriwa kufuga kwa tija, afuge mifugo michache kulingana na eneo lake lakini yenye manufaa ya kusomesha na kupata kipato. Hiyo kazi inafanywa na Serikali na inaendelea kuleta tija kubwa sana. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved