Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Muhammed Amour Muhammed

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Bumbwini

Primary Question

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:- Suala la mafuta ni la Muungano na kumekuwepo na taratibu mbalimbali zinazofanywa ili kutafuta mafuta nchini:- Je, ni taratibu zipi zilizopaswa kufanyika ili kuthibitisha kwamba mafuta yanapatikana katika eneo husika?

Supplementary Question 1

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo yanaonekana kuchupachupa kwa baadhi ya mambo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni community based, kwa kuwa research ni suala la Muungano na 2018 ilifanywa research kule Zanzibar nzima, ndani ya harakati za wale vijana kufanya research waliwaharibia wananchi wetu mazao yao. Je, ukizingatia research ni suala la Muungano Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina namna gani ya kurejea nyuma angalau kuwapa mkono wa pole wale waliowaharibia mazao yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali imesema kwamba wamekubaliana mafuta na gesi kila upande ufanye kwa kutumia taasisi zake. Pamoja na Azimio ambalo limepitishwa na Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar lakini bado suala la mafuta linabaki ni la Muungano. Je, hatuoni sasa ni wakati mwafaka sheria hii ambayo imo ndani ya Katiba ya Muungano kwamba mafuta ni suala la Muungano tukalitoa sasa ili kurahisisha uwekezaji kule Zanzibar?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri. Swali lake la kwanza ameulizia namna gani Serikali ya Muungano inaweza ikawalipa fidia wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa wakati wa utafiti. Kama lilivyosema jibu langu la msingi, utafiti huu ulifanyika kwa ajili ya masuala ya mafuta au gesi; na kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar kwa nia njema ilipofika mwaka 2015 Bunge hili lilipitisha Sheria ya Mafuta na kifungu cha 2 kilianisha kabisa mamlaka ambazo zitatumika katika suala zima la utafutaji mafuta ni kwa pande zote mbali na ni kwa nia njema ya kupunguza urasimu. Kwa kuwa shughuli hizi za utafiti za mafuta na gesi zilifanyika upande wa Zanzibar ambao wana mamlaka na walipitisha Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 labda nilichukue na kwa sababu tuna ushirikiano mzuri tutawasiliano na Wizara ya upande wa pili wa Muungano Zanzibar kuona hili jambo wanalifanyia kazi vipi lakini nia ilikuwa njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza kwa kuwa suala hili lilifanyika kwa nia njema kwa nini lisifanyiwe marekebisho. Jambo la kufanya marekebisho katika Katiba limeundiwa utaratibu wake ndani ya Katiba hiyo hiyo lakini kwa sasa kwa nia njema Bunge hili hili liliridhia kupitisha Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 na Baraza la Wawakilishi wakapitisha Sheria yao ya Mafuta ya mwaka 2016 kwa sasa shughuli zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako walikuwa mashahidi tarehe 23 Oktaba, 2018, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ilitiliana saini mkataba wa kugawana faida itakayopatikana wakati wa kuchimba mafuta au gesi na Kampuni ya RAK Gas kutoka nchi ya Ras Al Khaimah. Kwa hiyo, ni wazi kwamba tangu waingie mkataba huo kazi inaendelea na hakujatokea mgongano. Hata hivyo, hili naomba niliachie mamlaka zingine na Bunge hili kama itaona inafaa. Ahsante sana.