Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:- Miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha wanawake na watoto kuporwa mali zao na ndugu za waume zao ni kukosekana kwa wosia, jambo ambalo jamii haijaona umuhimu huo wakiamini kuwa kuandika wosia ni kujitakia kifo:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani endelevu wa kukabiliana na kadhia hii? (b) Je, Serikali itakuwa tayari kuielimisha jamii umuhimu wa kuandika wosia kama njia mojawapo ya kulikabili tatizo hili ambalo ni kubwa katika jamii?
Supplementary Question 1
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Sika, wosia wa mdomo au wa matamshi una changamoto nyingi. Kwa kuwa mazingira ya ndugu au mashuhuda huweza kubadili wosia kwa mtoa wosia, sasa hivi tuko kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia, je, kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kurekodi wosia wa mdomo na kuhifadhi RITA ili wanawake na watoto wasipoteze haki zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa mujibu wa gharama za RITA kutunza wosia unatunza kulingana na mali aliyonayo mweka wosia ambayo ni kuanzia Sh.5,000 hadi Sh.50,000. Je, Serikali haioni umefikia wakati wa kufanya marejeo ya gharama hizo? Ahsante sana.
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maswali ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumefikia kipindi cha utaalam wa kisayansi, nakubaliana na yeyee kwamba wosia usiwe tu wa mdomo, lakini tutumie njia ya kurekodi wosia huo kutoka kwa wazazi, kutoka kwa jamii. Pia nataka kumhakikishia kwamba Ofisi za RITA ziko katika kila Wilaya kwenye Ofisi ya DAS na tutajitahidi kama Serikali kuweza kuziwezesha kuwa na mashine za kurekodi wosia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kumhakikishia kwamba kuna Mashirika mengi Yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa yanafanya kazi na jamii mbalimbali, kwanza kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuweka wosia na pili jinsi ya kuandika wosia. Kwa hivyo Serikali yetu kwa kutumia sheria iliyopitishwa mwaka 2017 ya Misaada ya Sheria tutafanya pamoja ili kuhakikisha kwamba tunaboresha uandikaji wa wosia kwa wahusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, amesema sawa kwamba gharama kuanzia milioni 50, gharama ni Sh.5,000, kuanzia milioni 51 mpaka millioni 200 gharama za uandikishaji ni Sh.20,000. Kuanzia milioni 201 mpaka milioni 500 ni shilingi 30,000 na kuanzia hapo na kwenda juu ni shilingi 50,000. Ukitazama gharama hizi kwa kweli sio kubwa sana na kama tutapata mawazo kama uliyoyatoa hapo na kutoka kwa wananchi na kutoka kwenye ofisi zetu tunaweza tukatazama upya gharama hizi kulingana na mahitaji yatakavyojitokeza ili iwe ni motisha kwa wazazi, kwa ndugu kuweza kujiandikisha na kutumia huduma hii ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved