Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi, uchakavu wa majengo, mifumo mibovu ya maji safi na maji taka ikiwemo na ukosefu wa gari la wagonjwa:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia hospitali hiyo watumishi wa kutosha hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hii ni tegemeo la watu wengi hasa akinamama wajawazito? (b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba na vitendea kazi vingine ikiwemo CT Scan na MRI?

Supplementary Question 1

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inahudumia zaidi ya wagonjwa 300 kwa siku na inatoa huduma katika maeneo mawili tofauti, ipo hospitali ya zamani, ambayo ipo katika Kata ya Ipembe na hospitali mpya ya Rufaa iliyopo katika Kata ya Mandewa. Je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha inapeleka fedha za kutosha ili kumaliza ujenzi katika hospitali mpya ya Rufaa ya Mandewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hospitali hii inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Madaktari Bingwa wakiwemo wa wanawake na watoto pia ina uhaba wa vifaa tiba kama Oxygen Concentrator, baby warmer na phototherapy machine. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mahitaji haya muhimu katika hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida? Nakushukuru.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aisharose Ndoghoi Matembe, amekuwa ni mfuatiliaji mkubwa sana wa maendeleo ya hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na amekuwa ni mdau mkubwa sana kwetu sisi Wizara ya Afya kufuatilia masuala mbalimbali, nataka kumpa pongezi hizo. Naomba sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aisharose Matembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumezipokea hizo hospitali za Rufaa za Mikoa na kusudio letu ni kuhakikisha kwamba tunaziboresha ili ziweze kutoa huduma za kibingwa kama zilivyokusudiwa na ni kweli kwa sasa Mkoa wa Singida una hospitali ya zamani ambayo inatumika kama hospitali ya Rufaa ya Mkoa, lakini kuna ujenzi wa hospitali mpya ambao unaendelea pale Mandawe na nilishaitembelea na kusudio la Serikali ni kuhakikisha kwamba sasa tunaikamilisha ile hospitali. Baada ya hapo ile hospitali ya zamani tuirudishe katika ngazi ya halmashauri iweze kutumika kama hospitali ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, tutaendelea kuboresha na kuongeza Madaktari kadri tutakavyokuwa tunaendelea kuzalisha. Mwaka jana tumesomesha Madaktari takriban 125, mwaka huu tena tumeshasomesha Madaktari Bingwa zaidi ya 100. Kwa hiyo, kadri wanapokuwa wanamaliza na sisi tutakuwa tunawapangia katika hospitali zetu za Rufaa za Mikoa. Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba zile huduma za msingi za magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto, magonjwa ya mifupa, magonjwa ya akinamama, wataalam wa radiolojia, wataalam wa magonjwa ya dharura, kila hospitali ya Rufaa za Mkoa iweze kuwa nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na masuala ya vifaa tutaendelea kuongeza vifaa hivi kadri tutakavyoweza lakini nitoe msisitizo kwa waganga Wakuu wote wa hospitali za Rufaa wote wa hospitali za mikoa, masuala mengine wala siyo kuhitaji kusubiri Serikali, fedha wanazo waweze kuagiza vile vifaa ambavyo wanaviona ni muhimu katika utoaji wa huduma zao za afya.

Name

Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi, uchakavu wa majengo, mifumo mibovu ya maji safi na maji taka ikiwemo na ukosefu wa gari la wagonjwa:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia hospitali hiyo watumishi wa kutosha hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hii ni tegemeo la watu wengi hasa akinamama wajawazito? (b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba na vitendea kazi vingine ikiwemo CT Scan na MRI?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru matatizo yaliyoko Singida ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Geita DC, Hospitali ya Wilaya ya Geita imepandishwa hadhi takriban miezi sita na tunaishukuru sana Serikali kwa sababu imetuletea vifaa vingi x-ray machine, Ultra sound, machine za meno, vitu vya theatre, lakini vitu hivi vyote viko store kwa sababu hatuna wataalam na hospitali ile inaendeshwa na AMO na Madaktari wetu wengi bado wako Geita Mjini wamekaa tu ofisini. Je, ni nini kauli ya Serikali kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa apeleke watu wenye hadhi ya kuendesha Hospitali ya Wilaya?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Joseph Musukuma kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kufuatilia Hospitali hii ya Nzela katika Wilaya ya Geita na nilipata fursa ya kutembelea hospitali hii na ni hospitali kubwa na iliyojengwa kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelekezo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhambi kubwa sana kama hospitali imekamilika na vifaa vipo na haitoi huduma zile zilizokusudiwa wakati sisi kama Serikali tulishapeleka wataalam. Nitumie fursa hii kumkumbusha Mganga Mkuu na kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba wale wataalam wote ambao Serikali imewapatia na wapo mjini hawako katika kituo cha kazi kuhakikisha kwamba mara moja wanafika kule na wanatoa huduma kwa wananchi.

Name

Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi, uchakavu wa majengo, mifumo mibovu ya maji safi na maji taka ikiwemo na ukosefu wa gari la wagonjwa:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia hospitali hiyo watumishi wa kutosha hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hii ni tegemeo la watu wengi hasa akinamama wajawazito? (b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba na vitendea kazi vingine ikiwemo CT Scan na MRI?

Supplementary Question 3

MHE. JAPHARY R. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Singida halitofautiani sana na tatizo la hospitali ya Mawenzi ya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo hospitali ile imezidiwa sana na wagonjwa.

Sasa swali langu kwa Serikali, wako tayari kusaidia kuongeza Madaktari katika hospitali ile ya Mawenzi ili iweze kutoa huduma inayoridhisha kwa wagonjwa katika hospitali ile?

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Japhary Michael, Mbunge wa Moshi, kama ifuatavyo:-

Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ni hospitali ya Mkoa katika Mkoa wa Kilimanjaro na bahati nzuri nimepata fursa ya kutembelea ile hospitali. Kwa maana ya kuwa na Madaktari tunao Madaktari wa kutosha, changamoto ambayo tunayo pale ni Madaktari Bingwa na hili tumeshaliona Mheshimiwa Mbunge. Juhudi ambazo tunazifanya sasa hivi ni kusomesha Madaktari wengi zaidi na kuanza kuwapanga katika idara mbalimbali ambazo nimezisema katika swali la msingi, kuhakikisha kwamba sasa zile huduma za kibingwa zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaboresha mnyororo wa rufaa kwa maana ya kuboresha vituo vya afya na ujenzi wa hospitali za wilaya mbili ambazo zinaendelea katika Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha sasa ule mzigo ambao ulikuwa unakwenda pale katika hospitali ya mkoa, uweze sasa kuchukuliwa na hivi vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya.