Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Philipo Augustino Mulugo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songwe
Primary Question
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:- Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Songwe yapo Mbozi na hakuna barabara ya kuunganisha Wilaya mpya ya Songwe kufika mkoani hadi upitie Mbeya:- Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza barabara ya mkato toka Songwe kupitia Kata ya Magamba kwenda Mbozi Makao Makuu ya Mkoa ili kuwarahisishia usafiri wananchi wa Wilaya ya Songwe?
Supplementary Question 1
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ninayoiombea ni ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya kwenda mkoani, Wilaya ya Songwe ni mpya kabisa, kwa hiyo hatuna barabara inayounganisha wilaya na mkoa, kwa hiyo ningependa Serikali ifanye uharaka zaidi kwa sababu wale wananchi wanapitia Mbalizi ambako ni mbali sana. Kama itakuwa inatenga milioni 63 kila mwaka maana yake itachukua miaka sita kuja kupata hii barabara, nataka Serikali angalau iniongezee fedha kutoka milioni 63 mpaka milioni 300 ili tuweze kumaliza hii barabara kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais alipokuja Wilaya ya Songwe tulimwomba kilometa nne kwa ajili ya kufanya Mji wa Mkwajuni, Makao Makuu ya Wilaya yawe salama na yawe safi. Sasa ni lini Serikali itatupa fedha kwa ajili ya kilometa nne za lami pale Mji wa Mkwajuni?
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mulugo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa majibu kwenye majibu yangu ya msingi, yeye mwenyewe anakiri kwamba ameona nia ya Serikali ya kuhakikisha kwamba kwanza tunatambua kwamba tunataka tutumie kilometa ili wananchi wasiendelee kuzunguka na tumeanza kujenga hayo madaraja. Katika majibu yangu ya msingi nimemhakikishia kwamba ni vizuri tukawa na tathmini kujua gharama halisi ili hata hicho kiasi cha fedha kinavyotafutwa tuwe tunajua tunatafuta kwa ajili ya kazi gani ambayo inatakiwa ifanyike. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali tunatambua iko haja ya kuhakikisha kwamba wanafika Makao Makuu ya mkoa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anasema iko ahadi ya kilometa kwa ajili ya lami ili na wao katika makao makuu ya wilaya wafanane na makao makuu ya wilaya zingine. Naomba nimhakikishie Mhesimiwa Mbunge; ahadi zote za Viongozi wa Kitaifa tunazitekeleza na kwa Mkoa wa Songwe tumeanzia Makao Makuu kwa maana ya Momba, tunaanza kuweka kilometa moja, lakini pia na Mbozi. Naomba hatua kwa hatua, hakika ahadi zote za Viongozi wa Kitaifa sisi tutakwenda kuzitekeleza.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved