Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Immaculate Sware Semesi
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:- Je, katika mwaka 2016/2017 na 2017/2018 Serikali ilikusanya kiasi gani cha kodi ya 18% (VAT) kwa taulo za kike (sanitary pads) zote zilizotengenezwa nchini na zile zilizoingizwa nchini kabla ya kodi hiyo kuondolewa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Upendo Peneza bado ana maswali mawili ya nyongeza kutokana na majibu ya Serikali. Swali la kwanza, nauliza kwamba, japokuwa Serikali imeondoa baadhi ya kodi katika uzalishaji wa taulo za kike lakini bado bei ya taulo hizo iko juu sana. Sasa Serikali ina mkakati gani wa kusimamia bei hii kushuka ili kufikia wale walengwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza, sasa kama Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei za hizi taulo japokuwa wameondoa baadhi ya kodi, je, haioni kwamba iendeleze tu kodi zile za awali lakini kodi hii ikusanywe na iwe ringfenced ili kuweza kununulia hizi taulo za kike na kuzigawa bure shuleni?
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Sware Semesi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nianze na swali lake la pili ambapo amesema kama Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei; naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taifa letu kwa ujumla tupo katika soko huru kwa bidhaa zote, kwa hiyo sio kwamba Serikali imeshindwa kusimamia kushuka kwa bei, hapana, haijashindwa na ndiyo maana sasa hivi baada ya kuondoa kodi ile kwenye bidhaa hii Serikali imeendelea kupokea maoni mbalimbali ya wananchi wetu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuweka bidhaa hii kuwa ringfenced Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali, lakini kuna changamoto ya kusema kwamba kodi inayotozwa specific kwenye bidhaa hii iwekwe kwa ajili ya wanafunzi hawa kwa sababu yapo makundi mengine ambayo kodi zinatozwa kwenye bidhaa zinazotumika specifically na makundi kadhaa, kwa hiyo tutatengeneza ombwe la kila kundi kuja kuomba kodi inayotozwa kwenye makundi hayo waweze kupewa wao.
Mheshimiwa Spika, Serikali kama nilivyosema inaendelea kufanya utafiti, tumekwenda nchini Afrika Kusini, Botswana na Kenya kujifunza nini wanafanya. Wenzetu waliondoa kodi hizi na wakagundua kwamba haiwezi kuleta matokeo chanya kama ambavyo yamekuwa ni majibu ya Serikali yetu ndani ya Bunge lako Tukufu. Kinachotakiwa kufanyika ni kubuni njia nyingine ya kuhakikisha watoto wetu wa kike wanapatiwa bidhaa hizi lakini bila kui-attach na kodi au tozo zozote zinazotozwa kwenye bidhaa hii kwa sababu tumejiridhisha kwamba unapoondoa kodi wanaonufaika ni wazalishaji kwa sababu tuko kwenye soko huria.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, kwamba ni mkakati gani kama Serikali tunaweka; nimesema sasa hivi tunaendelea kufanya tafiti mbalimbali ambapo tutakapojiridhisha na options ambazo zitaleta matokeo chanya kwa pande zote mbili watoto wetu wa kike na Serikali yetu, basi tutakuja na option hiyo ndani ya Bunge lako Tukufu ili tuweze kuwasaidia watoto wetu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved