Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, ni lini kiwanda cha Saruji cha Dangote kitapewa gesi asilia na TPDC?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kutimiza ahadi yake kupeleka gesi kwenye Kiwanda chetu cha Saruji cha Dangote. Pamoja na pongezi hizi, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na kupeleka gesi kwenye Kiwanda chetu cha Dangote, kuna viwanda vingine Mkoani Mtwara hususan viwanda vya kubangua korosho. Je, Serikali imejipangaje kupeleka gesi kwenye viwanda hivyo ili itumike katika shughuli za uzalishaji katika viwanda hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kuhusu usambazaji wa gesi majumbani kwa sababu gesi inayozalishwa ni nyingi lakini matumizi ni kidogo. Je, Serikali imejipangaje kuongeza idadi ya watu watakaotumia gesi majumbani kwa Wilaya ya Nanyamba, Newala, Masasi na Mikoa mingine ili tutumie gesi yetu ipasavyo?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee pongezi zake kwa niaba ya Wizara baada ya kukamilisha ahadi yetu ya kumpelekea gesi Kiwanda hiki kikubwa cha Dangote kinachozalisha saruji. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Chikota kwa kazi nzuri anayofanya katika kufuatalia matumizi ya gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake mawili ya nyongeza anauliza ni lini Serikali itasambaza gesi katika viwanda ambavyo viko Mkoani Mtwara ikiwemo vya kubangua korosho. Napenda nimtaarifu Serikali yetu inatambua umuhimu wa gesi katika kuwezesha viwanda kuzalisha malighafi kwa kutumia gesi na ina mpango kabambe wa kusambaza gesi katika maeneo ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tuna viwanda zaidi ya 27 ambavyo vinatumia gesi na sasa hivi kuna mradi ambao unatekelezwa wa kusambaza gesi majumbani na viwandani na hasa maeneo ya Mtwara na Mkuranga. Hivi ninavyozungumza tayari TPDC imeshakamilisha mazungumzo na mkataba wa mauziano ya gesi ya viwanda vya KNAUF Gypsum Mkuranga na Lodhia Mkuranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye viwanda vya kubangua korosho, naomba niwataarifu wawekezaji wetu wote wenye viwanda katika ukanda huo ambao bomba la gesi limepita kutoka Mtwara kwamba fursa hiyo ipo, waje tu tuzungumze na TPDC. Serikali imejipanga katika uwekezaji huo na hata katika Mpango wa Matumizi ya Gesi kiasi cha trilioni 8 cubic fit zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya viwanda tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili alikuwa anauliza ni lini usambazaji wa gesi asilia majumbani utafanyika. Nataka nimtaarifu sasa hivi hata Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani alizindua Mradi wa Usambazaji wa Gesi Asilia katika Mkoa Mtwara na Dar es Salaam. Kazi inayoendelea ni ununuzi wa vifaa mbalimbali na mpaka sasa vimeshanunuliwa vifungashio, vifaa vya kupunguza mgandamizo wa gesi, vifaa vya kupimia gesi majumbani. Vifaa vyote hivi vitakamilika ifikapo Mei, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kazi ya kusambaza gesi katika Mikao ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam inaendelea. Ahsante sana.