Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Je, kwa nini Serikali inatenga na kutumia fedha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji?
Supplementary Question 1
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa taarifa tu ni kwamba na mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa hiyo, hiki nilichokuwa nakiuliza nahitaji Wenyeviti wengine wapate ufafanuzi wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali inatenga fedha nyingi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Majibu ya Naibu Waziri amenukuu Katiba, Ibara ya 146, wanasema madhumuni ya kuanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kuharakisha maendeleo ambapo kuchaguliwa huku na sisi Wabunge, Madiwani pamoja na Rais tunachaguliwa hivyohivyo lakini sisi tunalipwa posho na mshahara. Kama Serikali inaweza kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi, kwa nini haitengi fedha kwa ajili ya kuwalipa Wenyeviti hawa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa na Vijiji kuna Watendaji wa Vijiji na wa Serikali za Mitaa ambao wanalipwa na Serikali, wanaofanya kazi saa tisa lakini Wenyeviti wanaochaguliwa na wananchi wanafanya kazi saa 24 hawalipwi. Serikali haioni sasa kwa kuwa mpaka sasa haijawalipa Wenyeviti wala hakuna sheria yoyote iliyoletwa kwa ajili ya kuwalipa, kwa nini isiufute Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wabaki hawa wanaolipwa na Serikali?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimjibu Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, maswali yake ya nyongeza mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuhusu posho za Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Mimi pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kabla ya kuwa Mbunge tangu 2014 mpaka 2017. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba haya ni maswali ya uchonganishi na naomba niwaambie Wenyeviti wa Mitaa kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inawapenda sana na ndiyo maana inataka kuwaeleza ukweli na naomba wanisikilize.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kwenda kugombea kunakuwa na maelezo na kanuni zimetaja sifa za nani anapaswa kuwa Mwenyekiti wa Mtaa. Sifa mojawapo muhimu sana ni kuwa na kipato cha kumfanya aweze ku- sustain maisha yake binafsi. Kwa hiyo, mtu yeyote anapoenda kuchukua fomu na bahati nzuri mwaka huu mwezi Novemba tunafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kila anayetaka kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au Mjumbe wa Serikali ya Mtaa au Kijiji, Kitongoji, anapaswa asome sifa, ajiridhishe ndiyo achukue fomu, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Wenyeviti wa Mitaa kwa mujibu wa maelezo ya Serikali watalipwa kwa viwango mbalimbali kulingana na uwezo wa Halmshauri yao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anapouliza swali ningetaka aseme kwenye Halmashauri yao wamejipangaje kuwalipa posho Wenyeviti wa Halmashauri kwa sababu pesa ziko kule na miradi iko kule wanaisimamia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa uwezekano wa Serikali kulipa posho za Wenyeviti wa Mitaa kwa maelekezo tuliyotoa makusanyo yakipatikana kinachotakiwa kirudishwe kwenye Halmashauri asilimia 20 walipwe. Ni muhimu kuzingatia Mheshimiwa Diwani anapochukua fomu anafahamu mimi sina mshahara nitalipwa posho, anajiridhisha Sh.350,000 kwa mwezi inatosha.
Mheshimiwa Spika, tunaomba watenganishe kati ya kazi na posho. Wafanye kazi kwa weledi lakini wasiache kuwahudumia wananchi kwa sababu hawajalipwa posho, kwa sababu hayo ni makubaliano na wameridhika kabla ya kugombea. Serikali ikipata uwezo wa kutosha itapeleka posho kwa Wenyeviti wa Mitaa, kwa sasa uwezo haujapatikana, tunawaomba waendelee kufanya kazi kwa weledi, wanafanya kazi kubwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ipo pamoja na Wenyeviti wa Mitaa kinyume na hapo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba kwa sababu Wenyeviti wa Mitaa hawalipwi posho na Watendaji wa Mitaa na Vijiji wanalipwa kwa hiyo tufute wabakie wanaolipwa. Hawa Watendaji wa Mitaa, Kata na Vijiji ni watumishi wa Serikali, wanatajwa kwenye orodha ya watumishi wa umma.
Kwa hiyo, huyu ni mtumishi na ndiyo maana anapotaka kupata nafasi hii tunatangaza nafasi kwa uwezo wa Halmashauri na Serikali Kuu, analeta vyeti, anakuwa- vetted, anakaguliwa, anapewa mkataba wa kazi yake na huyu anapaswa kufanya kazi kwa niaba ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwenye ngazi ya Kijiji na Mtaa huyu Mtendaji ndiyo Mkurugenzi wa Halmashauri na kama kuna jambo lolote hawa wanawajibika. Kwa hiyo, naomba tutofautishe huyu ni mtumishi wa Serikali na huyu ni mtumishi wa wananchi kwa kazi ya kujitolea na wote ni watu muhimu sana katika eneo hili. Huyu Mtendaji na watu wengine watapata kile ambacho kinastahiki kwa kadiri ambavyo tumekubaliana. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved