Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Khatib Said Haji
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Fedha za kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF), zimekuwa msaada mkubwa katika kusaidia Maendeleo Majimboni. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza viwango vya fedha hizi ili kuleta ufanisi zaidi?
Supplementary Question 1
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kuna baadhi ya halmashauri hufanya matumizi ya fedha hizi bila kumshirikisha Mheshimiwa Mbunge, na hayo yako hasa kwa upande wa Zanzibar. Je, Serikali inatoa kauli gani ili waache tabia hiyo mbaya na kujua kama Mbunge ndiyo mhusika mkuu na msimamizi wa Mfuko huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sijui huku Bara lakini kwa upande wa Zanzibar Mheshimiwa Mbunge baada ya kupitisha matumizi ya fedha hizi, halmashauri inakuwa haimshirikishi katika suala lolote tena. Je, mamlaka ya Mbunge katika kusimamia fedha zile kwa upande wa Zanzibar ni ya halmashauri au ni Mbunge anahusika mwanzo hadi mwisho? Ahsante sana.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, anataka kujua kama fedha hii inaweza ikatumika bila Mbunge kuhusika. Kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi ni kwamba Mwenyekiti wa fedha hii ya Mfuko wa Jimbo ni Mbunge mwenyewe na wametajwa vizuri wajumbe wa Mfuko wa Jimbo, Madiwani wawili kwa kuzingatia jinsia, Watendaji wawili wa Kata au Viti Maalum lakini na mtu mmoja ambaye anakuwa ni kutokana na NG’O katika Jimbo husika, halafu anaongeza na Katibu wa Mfuko huu anakuwa ni Mchumi katika halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kuna fedha inataka kutumika, kwa vyovyote vile hata kama Mbunge hatakuwa Jimboni ni lazima Mkurugenzi wa halmashauri hiyo afanye consultation na Mbunge wa Jimbo kama Mwenyekiti na kama hatakuwepo maana yake Mbunge ataridhia labda Diwani miongoni mwa wale Madiwani kwa sababu shughuli haziwezi kusimama ili aweze kufanya kazi hiyo. Miradi inapopitishwa Mkurugenzi kazi yake ni kwenda kupitisha fedha ikatumike na siyo kupanga kwamba ongeza, punguza hiyo hairuhusiwi kabisa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linafanana na la kwanza, kama nilivyosema na naomba nirudie tumepata malalamiko kwa kweli karibu Wabunge wengi hapa wanalalamika. Wakurugenzi wa halmashauri hawana maamuzi katika fedha hizi, hizi fedha zinaenda kwenye vikao na Wabunge ambao ni Wenyeviti wenyewe wanajadili, na inawezekana Mbunge akaenda kwenye eneo A au Kijiji B akasikiliza kero za wananchi au Mwenyekiti wa Mtaa au Mheshimiwa Diwani au wananchi wa kawaida wakalalamika, Mbunge anaweza akasema napeleka shilingi laki tano hapa. Kwa hiyo Mkurugenzi hawezi kubadilisha haya maelekezo ya Mbunge kwa sababu ndiyo uwezo wake. Ndiyo maana inaitwa Fedha ya Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, kwa hiyo, wale Wakurugenzi ambao wana tabia ya kutumia fedha bila Mbunge tunaomba majina yao tutawashuhulikia kwa sababu Sheria imetaja vizuri namna ambavyo wanapaswa kufanya.
Mheshimiwa Spika, tumeelekeza, ukishapitisha fedha hizi kwenda kutumika ni lazima Kamati ya Mfuko wa Jimbo iende kufanya ziara ikakague hiyo miradi kama kweli ipo na kama imetekelezwa na anayetajwa pale ni Mbunge. Hii ni fedha ya Serikali, lazima isimamiwe vizuri na Sheria imeelekeza kwamba Mbunge inawezekana hana fedha mfukoni kutoa lakini kupitia Mfuko huu unaweza ukatamka neno kwa wananchi na roho za wananchi zikapona, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, makofi kwa majibu ya Serikali kutoka kwa Wabunge yanaashiria kwamba yako matatizo katika uendeshaji na matumizi na usimamizi wa Mfuko wa Jimbo ambao lengo lake mahsusi ni kuhakikisha kwamba Wabunge wanachochea shughuli za maendeleo katika Majimbo yao.
Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali sisi mtuachie pia twende tukashauriane na Waziri mwenye dhamana ikiwezekana Serikali itoe waraka wa maelekezo tena kusudi kila halmashauri iweze kusimamia utekelezaji wa kisheria wa mfuko huo, lakini vilevile tuwaombe Waheshimiwa Wabunge kama Wenyeviti wa Mifuko hiyo, waone kwamba wana wajibu pia wa kuhakikisha kwamba matumizi ya fedha ya Mfuko wa Jimbo yanafanyika kwa kuzingatia Sheria.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved