Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Immaculate Sware Semesi
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:- Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”; lakini kumekuwa na kiwango cha juu cha matukio na kesi zinazohusu kuvunjwa kwa haki za kiraia kwa kufanywa na vyombo vya dola:- (a) Je, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015 ni kesi ngapi zimefunguliwa Mahakamani kuhusu madhara yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia, na huchukua muda gani hadi kutolewa hukumu? (b) Je, kesi hizo zimekuwa zikigharamiwa kwa kiasi gani kutoka Mfuko wa Fedha za Umma tangu mwaka 2010 – 2015? (c) Je, Serikali inafanya jitihada gani kuhakikisha wananchi wake pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majibu niliyoletewa na Serikali ni dhahiri kuwa suala hili bado halijawekewa mkazo na bado wananchi wanapata shida wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola. Sasa Serikali haioni ni wakati sasa wa kujifanyia tathmini mahususi na kuja na mikakati thabiti ili wananchi wa Taifa hili wapate kuwa na kusimamia haki zao? Ahsante.
Name
Dr. Augustine Philip Mahiga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tathmini ni muhimu na ni endelevu. Wizara yangu inaendelea kufanya hivyo na kusisitiza kwamba Tume ya Haki za Binadamu inafanya hiyo. Pia ninapenda kusisitiza kwamba suala la haki za binadamu lazima iwe ni sehemu ya utamaduni wa Taifa; na kuifanya ni sehemu ya utamaduni wa Taifa itabidi tutengeneze mkakati wa somo la Haki za Binadamu liingie katika mitaala ya shule zetu zote na katika ngazi zote. Somo la Haki za Binadamu na Utawala Bora liwe ni sehemu ya lazima kwa mafunzo yote ya vyombo vyetu vya usalama. Kama ni ulinzi, kama ni Polisi, Usalama wa Taifa au Uhamiaji, iwe ni sehemu muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Askari wetu wanaoshiriki katika vikosi vya kulinda amani duniani huwa wanapewa kozi ya haki za binadamu kwa wiki sita na Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa na Taasisi mbalimbali za Kimataifa ziko tayari kuisaidia Tanzania kuweka Chuo cha Haki za Binadamu ambacho kitatengeneza mitaala katika shule mbalimbali. Hiyo nimehakikishiwa na ninadhani inaweza kutokea tukishachukua maamuzi. Watu wako tayari kutusaidia ili haki za binadamu na utawala bora iwe ni sehemu ya utamaduni wa Taifa hili.
Name
Frank George Mwakajoka
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:- Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”; lakini kumekuwa na kiwango cha juu cha matukio na kesi zinazohusu kuvunjwa kwa haki za kiraia kwa kufanywa na vyombo vya dola:- (a) Je, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015 ni kesi ngapi zimefunguliwa Mahakamani kuhusu madhara yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia, na huchukua muda gani hadi kutolewa hukumu? (b) Je, kesi hizo zimekuwa zikigharamiwa kwa kiasi gani kutoka Mfuko wa Fedha za Umma tangu mwaka 2010 – 2015? (c) Je, Serikali inafanya jitihada gani kuhakikisha wananchi wake pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia?
Supplementary Question 2
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kila mwananchi wa Tanzania ana haki ya kulindwa na Serikali yake na sasa hivi kumetokea wimbi kubwa sana kwenye Nchi ya Afrika Kusini, wageni wanauawa, wanatekwa, wanachomwa moto na wanateswa sana. Je, Serikali ya Tanzania imechukua hatua gani kuwalinda Watanzania wote ambao wako Nchini Afrika Kusini kwa kipindi hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Name
Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema, suala hilo ni la Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni suala ambalo limekuja mahali pasipokuwa pake kwa sababu bado ipo siku ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na linaweza kuwa ni swali ambalo linajitegemea. Hata hivyo, msizoze, acha kuzoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwanza ninapenda kusema kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika ya Kusini zina mahusiano mazuri sana ya kindugu na ya muda mrefu. Ndiyo maana nichukue fursa hii pia kumpongeza Cyril Ramaphosa kuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini; na inshallah tukijaliwa tutahudhuria kuapishwa kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la usalama wa Watanzania siyo wa Afrika ya Kusini tu, usalama wa raia wa Tanzania popote walipo ni jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha Watanzania popote walipo wapo salama. Kwa hiyo, suala hilo linafuatiliwa na Serikali ya Afrika Kusini yenyewe imeziandikia Nchi zote za Afrika; moja, kuomba radhi kwa yale yote yanayotokea nchini mwao ambayo yanaonekana kuwa ni ya ubaguzi na yanayoifanya Afrika ya Kusini ionekane ni nchi ambayo haikumbuki ilivyosaidiwa na Waafrika wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali ya Afrika ya Kusini yenyewe imetuletea andiko kupitia Ofisi ya Ubalozi kuomba radhi kwa yale ambayo yanatokea. Nasi tunachukua hatua moja ya kuhakikisha raia wote waliko Afrika Kusini wako salama; na wale ambao watapata matatizo tumewaambia watoe ripoti kwenye balozi zetu ili hatua za kuwalinda na usalama wao kuwepo zichukuliwe. Kwa hiyo, hilo ndilo jibu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved