Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hassan Elias Masala
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha jengo la Mahakama Wilayani Nachingwea?
Supplementary Question 1
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kabisa kwamba jengo lile halihitaji tu kufanyiwa marekebisho isipokuwa kujengwa; na kuwa kuwa pia tathmini imeshafanyika toka mwaka 2017/2018, kuna sababu gani sasa za kutenga fedha au kulipeleka jengo hili kwenye mpango wa kujengwa 2020/2021 badala ya mwaka 2019/ 2020?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba kujua nini mpango wa Wizara ya Katiba na Sheria katika kuongeza idadi ya watumishi katika Mahakama zetu hasa Mahakama za Mwanzo? Nachingwea tuna kituo pale kinaitwa Ndomoni, kwa muda mrefu sasa kimefungwa na wananchi hawapati huduma pale. Hivyo, wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda Nachingwea Mjini kufuata huduma ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Mahakama wa Miaka Mitano wa Kuboresha Huduma za Mahakama hapa Nchini, imeweka pia vipaumbele vya ujenzi. Baada ya taratibu zote hizo kukamilika, limetengenezwa jedwali ambalo ndiyo linaipelekea Mahakama hii kuanza kujenga hizi Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pande wa Nachingwea, kwa sababu tathmini ilikuwa inaendelea kufanyika katika jedwali letu, Nachingwea wenyewe ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha 2020/2021 hasa kutokana na kwamba ilikuwa lazima taarifa hizo zikamilike na tayari kuna baadhi ya Mahakama ilikuwa imeshaingia katika mpango wa ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunatambua changamoto hiyo lakini kwa sasa kwa sababu Wizara tumeingia makubaliano na Baraza la Ujenzi wa Taifa katika ujenzi wa Mahakama kupitia teknolojia mpya na bei nafuu ya Moladi naamini kabisa kwamba pindi fedha itakapopatikana tutaanza ujenzi wa Mahakama ya Nachingwea ili kuwaondolea usumbufu wananchi wa Wilaya ya Nachingwea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika swali lake la pili la kuhusu watumishi, ni kweli tuna changamoto katika baadhi ya maeneo, lakini nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi kwa maana ya kuajiri watumishi wengine ambapo tunaenda kupata kibali toka utumishi. Kwa hiyo, pindi ajira hizi zitakapotangazwa na kupatikana, pia Wilaya ya Nachingwea itaangaliwa katika kutatua changamoto hii ya ukosefu wa watumishi katika eneo hilo ili wananchi wa Nachingwea waweze kupata huduma za Mahakama kwa ukaribu lakini na kwa ufanisi zaidi.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved