Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Zuberi Mohamedi Kuchauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Primary Question
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:- Mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha utalii wa picha badala ya utalii wa uwindaji kwenye Mapori yetu ya Akiba nchini: - Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na lango la utalii wa picha kwenye Pori la Akiba la Selous kwenye Ukanda wa Kusini kwenye Wilaya za Tunduru na Liwale?
Supplementary Question 1
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote, niishukuru Serikali kwa kuliona hili na kupandisha hadhi Hifadhi ya Selous, lakini baada ya kupandisha hadhi au baada ya Serikali kuimarisha uhifadhi katika hifadhi zetu suala la wanyamapori limekuwa ni shida sasa hivi, hasa wanyama kama tembo. Wanyama hawa sasa hivi wanasumbua kwenye maeneo yetu na niliuliza swali hapa kuhusiana na Serikali kuleta Muswada pengine kupata fidia wakasema haiwezekani, lakini bado suala la kifuta machozi hakipatikani. Je, Serikali ipo tayari kutupatia fedha hizi mapema iwezekanavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili inapozungumzia utalii Kanda ya Kusini, bado napata changamoto. Mwaka jana tumepata fedha kuendeleza utalii Kanda ya Kusini, lakini Wizara hii inapozungumzia Kanda Kusini wanazungumzia Morogoro, Mbeya na Iringa, lakini Mkoa wa Lindi, Mtwara na Songea hautajwi. Je, Serikali kwa upande wake inapozungumzia kukuza utalii ukanda wa kusini unaamanisha mikoa ipi? Ahsante sana.
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akifuatia haki za wananchi wake hasa wanaoathirika na matatizo ya kuharibiwa kwa mali zao na kuhatarisha usalama wao na wanyama waharibifu kama tembo. Nilifanya naye ziara kwenye jimbo lake na tulifanya mikutano takriban mitatu na tulizungumza na wananchi hasa kwenye mgogoro wao wa mpaka na Selous.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kweli kwamba tuliahidi hapa tutaleta marekebisho ya kanuni, kanuni zipo lakini Wizara yetu inazipitia upya ili kanuni hizo zinapokwenda kulipa fidia hiyo fidia iwe angalau na thamani kulingana na uharibifu uliofanywa kwa sababu zimekuwa za muda mrefu. Kanuni hizo zimekuwa ziko tayari na Mheshimiwa Waziri hivi karibuni alikuwa amealika wadau kuzipitia na mara baada ya wadau kupitia, tutazitangaza na zitaanza kutumia. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge ni kweli awali zilikuwa malipo yake ni kidogo, lakini tumezipita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuchelewa kwa kifuta jasho suala hili linahusisha taratibu na taratibu zinaanzia kwenye halmashauri yenyewe kwenye vijiji. Wataalam wetu wa vijiji wa kilimo wanapaswa kulifanya suala hili kwa haraka kwa kulipeleka kwa Afisa Wanyamapori wa Wilaya na baadaye linafika kwenye level yetu ya Wizara na kwa sababu ni la nchi zima, mara nyingi tumekuwa tukiangalia first in, first out. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni suala la utalii kusini, ni kweli imekuwepo tafsiri kwamba unaposema utalii kusini unamaanisha Lindi, Ruvuma na Mtwara, lakini tunapozungumzia kwenye Mradi wa REGROW ni utalii wa Nyanda za Juu Kusini. Sasa hivi Wizara yetu ipo katika hatua za mwisho za kuandaa utaratibu ambao tutafanya mkutano tena kama tulivyofanya na watu wa Nyanda za Juu Kusini ili kufungua utalii wa kusini kwa maana ya Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge hatujasahau eneo hili, tunalifanyia kazi na Wizara inashirikisha wataalam kutoka vyuo vikuu mbalimbali katika kuangalia maeneo ambayo yanaweza kutuletea mafanikio ya haraka ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya mikoa hii yote ambayo inapakana na bahari na hasa katika maeneo ambayo tuna mali kale nyingi kama maeneo ya Mikindani na Kilwa. Nakushukuru sana.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuongezea majibu kwenye sehemu ya swali la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka kwamba tunapozungumzia utalii Kanda ya Kusini, hatuzungumzii utalii wa Kanda ya Kusini ambayo ipo kwenye nyanda ya juu peke yake, tunazungumzia kusini kwa ujumla wake. Mradi wa REGROW pamoja na ku-include na pori la Akiba la Selous la zamani na sasa Nyerere National Park ambayo ipo kusini proper huku lakini pia imejikita kutengeneza Mji wa Iringa kama kama hub ya utalii, lakini mradi huu upo kwenye awamu hii ya kwanza awamu ya pili utatanua maeneo zaidi kwenye upande wa Kanda ya Kusini upande huo wa akina Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kuna miradi mingine mikubwa inayoendelea kule ikiwepo Mradi wa SECAD lakini pia ikiwemo mradi wa kukifanya Kisiwa cha Kilwa Kisiwani ile malikale iliyopo pale kama kivutio cha kipekee. Pale tumewaelekeza TAWA ambao kwa sasa tumewapa dhamana ya kuwaendeleza utalii kwenye eneo hili Kilwa Kisiwani, wanunue boti ya kitalii ambayo itakuwa ya first class na business class, lakini pia wawekeze kwenye lodge ya kitalii ambayo itakuwepo katika eneo hilo la kisiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mradi mkubwa utakuja pale kama wananchi watatoa ushirikiano, kuna zaidi ya trilioni moja itawekezwa pale katika eneo la fukwe zilizopo pale kusini kuanzia Kilwa mpaka Msimbati na hivyo tunaamini utalii wa fukwe unaweza ukakua kwa kiasi kikubwa sana katika eneo lile kama wananchi watatoa ushirikiano ili tuweze kuilinganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na fukwe zilizopo pale kusini. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved