Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sabreena Hamza Sungura

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza mahabusu katika Magereza na Vituo vya Polisi nchini?

Supplementary Question 1

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Moja, kwa kuwa wananchi wengi sana wa Tanzania ambao wamekuwa wakipelekwa mahabusu, whether wana kesi za kujibu ama hawana, ama ni kesi zinazopata udhamini, wamekuwa wakiingia mahabusu bure, lakini kutoka ni hela; napenda kuuliza: Je, Serikali imewahi kufanya utafiti kwamba suala hili linatokea na ni hatua gani wanachukua? Kwa sababu siyo suala la kisheria kwamba mtu akiingia mahabusu kutoka lazima atoe hela ndiyo atolewe. Ni suala la practice, sisi tuliopo mitaani tunajua kwamba mtu anapelekwa mahabusu lakini siku ya kutoka wengi wao wanakuwa wanachajiwa. Je, Serikali inachukua hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kumekuwa kuna wimbi kubwa la kesi, hususan za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kwa vijana hasa vijana hawa kama akina Tito, Kabendera na wengine wengi ambao hatuwajui, wamekuwa wakikaa mahabusu kwa muda mrefu na kesi zao zikiendelea huko; inawezekana siku ya siku wakaja kukutwa na hatia ama wasikutwe na hatia; lakini kwa kuwa tulipitisha sheria hapa Bungeni ya pre-bargaining ambayo inamtaka mshtakiwa ama wakili wake ama mwendesha mashtaka kuomba mahakamani waweze kupata ili kupunguza ukubwa wa adhabu, kupunguza muda wa adhabu lakini kuondoa baadhi ya kesi; pia Mheshimiwa Rais kupitia maombi maalum ya barua alikuwa akiwahi kutoa msamaha; sasa Bunge halioni ni wakati muafaka sasa tuje tufanye mabadiliko ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ili kuweka flexibility kwa Majaji na Mahakimu ambao wamekuwa wakiendesha kesi hizi na wenyewe waweze kuangalia ukubwa wa kosa na kuweza kutoa dhamana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu Bunge tumetunga sheria, tumewafunga mikono kwamba hawawezi kutoa dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi. Hata hivyo, mtu anaweza akahujumu uchumi ama kufanya utakatishaji fedha kwa 20,000/=, mwingine shilingi bilioni moja, wote wananyimwa dhamana kitu ambacho kinasababisha mlundikano wa kesi.

Je, Bunge sasa halioni ni wakati muafaka wa kuleta mabadiliko ya sheria hii ili vijana ambao hawana hatia na wanateseka huko Magerezani waweze kupunguza idadi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anazungumzia kwamba kuna kauli ambayo inatapakaa katika jamii kwamba unaingia mahabusu bure na unatoka kwa pesa. Siwezi nikapingana na kauli hii kwa sababu mbali ya kazi kubwa na nzuri ambayo Askari wetu wamekuwa wakiifanya ya kusimamia usalama wa nchi hii na ndiyo maana nchi yetu iko salama, lakini tunakiri kwamba wako baadhi ya Askari ambao wamekuwa wakikiuka maadili na ndio hao ambao pengine wanatuhumiwa na mambo kama ambayo amezungumza Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tunabaini Askari yeyote anayekiuka maadili yake kwa kufanya utaratibu kama ambao ameueleza wa kuwatoza mahabusu fedha ama kuwabambikia ama kuwaonea, tumekuwa tukichukua hatua. Wapo Askari kadhaa ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali kila mwaka ingawa ni wachache mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mabadiliko ya sheria, nadhani ni mamlaka ya Bunge hili kutunga sheria na kubadilisha pale ambapo inaona inafaa. Naye ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni anazifahamu. Kama kuna utaratibu ambao Mheshimiwa Mbunge anadhani kuna haja ya kuleta hoja binafsi ama utaratibu mwingine ambao ataona unafaa, basi ni juu ya Mbunge yeyote kutumia haki yake ya Kikatiba na kikanuni.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza mahabusu katika Magereza na Vituo vya Polisi nchini?

Supplementary Question 2

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala hili la hadhi ya mahabusu wetu ni suala nyeti na pana; na kwa kuwa sisi wote humu ndani tunayo nafasi ya kufanya marekebisho katika sheria hizi ili haki ya aina yoyote ya mahabusu iweze ikatendeka; na tumemsikia Jaji Mkuu akisema kwamba pamoja na kuwepo kwa wingi wa mahabusu ni kutokana na kutokufanyika kwa upelelezi na kuukamilisha ndiyo mtu aweze kupelekwa Mahakamani:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali, au Serikali kama imesikia kilio cha Jaji Mkuu na ushauri wao, nasi ni Wabunge na tukitegemea tunayo nafasi ya kuweza kufanya mabadiliko ya sheria hizi sasa, maana huwezi kujua kesho, wote hapa ni wafungwa watarajiwa; iwe kwamba, kama ni miezi mitatu upelelezi haujakamilika, basi mfungwa au mahabusu aachiwe au vinginevyo kwa busara itakavyoelekeza sheria hii sasa ifanyiwe marekebisho mahabusu waweze kupata haja na haki zao za kimsingi.

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema kubwa na ndogo anazotujalia sote hata kufika siku hii ya leo. Vile vile nimshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbatia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hadi sasa jitihada hizi zinazofanyika kwa njia hizi tatu ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezijibu kwenye jibu la msingi ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alipotembelea Magereza likiwepo Gereza la Butimba na akatoa maelekezo kwamba hali ilivyo, Magereza yamezidiwa na mahabusu ndio wengi zaidi na ndiyo maana hatua zinaendelea kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, DPP amekuwa akifanya jitihada za kutembelea Magereza na kuongea na wafungwa. Pia nasi kama Wizara tumekuwa tukifanya hivyo na ninaamini kabisa kila baada ya muda tutakuwa tunapunguza baadhi ya mahabusu ambao wana kesi ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua kubwa zinafanyika, nami nadhani iko haja ya jitihada hizi zinazofanyika tukawa tunaleta taarifa hapa kwenye Kamati au kwa njia yoyote ambayo mtaona inafaa kwa sababu ni kweli jitihada zinafanyika. Isipokuwa mchakato wake kama mnavyofahamu, zipo haki za wafungwa, zipo haki za mahabusu na zipo pia haki za waliotendewa makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, usilichukulie jambo hili kama ni jepesi. Lazima lichujwe, liangaliwe na upo utaratibu wa kisheria wa kufanya mambo haya. Kwa hiyo, pia tusikimbilie kushabikia tu haki za hawa waliotenda makosa. Ni kweli wanazo, lakini zipo haki pia za waliotendewa makosa. Kwa hiyo jambo hili linahitaji tuli-balance vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kwa jibu hilo watakubaliana nami kwamba jitihada hizi kwa kweli ni kubwa na zimetokana na maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)