Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y MHE. KABWE Z. R. ZITTO) aliuliza:- Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanapata changamoto za huduma za uhamiaji kutokana na Balozi zetu takribani zote kutokuwa na Maafisa Uhamiaji. Je, ni lini Serikali itapeleka Maafisa Uhamiaji kuhudumu kwenye Balozi zetu ili kutoa huduma bora kwa raia wa Tanzania kwenye nchi hizo?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali imeteua maafisa watano; na tunajua kwa miaka mitano ya uongozi wa awamu hii maafisa wengi wamerejeshwa Tanzania na hivyo Balozi nyingi hazina maafisa kwa sababu ya hofu labda ambazo wanazijua ndani ya chama chenu. Sasa maafisa watano tu katika Balozi nyingi ambazo ziko kwenye nchi mbalimbali hamuoni kwamba mnawapatia Watanzania wanaoishi nje ya nchi matatizo ya kupata huduma ambayo ni ya kimsingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarehe 31 mwezi wa kwanza mwaka huu Serikali ilisitisha matumizi ya passport za zamani; na tunajua Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanahitaji passport ambayo ndiyo inawapa uwezo wa kuishi huko wanakoishi na kufanya shughuli zao. Ni lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaoishi huko wanapata huduma hii kwa haraka ili wasionekane kama wamekuwa-condemned kurudishwa huku kwa sababu hawana passport?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Heche kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina hofu, ni suala la utaratibu tu. Kwamba kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi, kwamba kwa kutambua upungufu huo wa Maafisa Uhamiaji ndiyo maana maafisa watano wako mbioni kupelekwa wakati wowote. Hata hivyo nataka nimhakikishie kwamba kutokuwa na Maafisa wa Uhamiaji katika kila Balozi hakumaanishi kwamba wananchi au wageni wanaotaka kupewa huduma hizo wanashindwa kupata; kwa sababu kwanza hivi sasa hivi tuna Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao nitauelezea kwa kifupi ili pamoja na mambo mengine utakuwa umeweza ku-cover lile swali lake la pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao unahusisha uhamiaji kwa maana ya e-passport, e-visa, e-permit pamoja na e-gate umerahisisha sana kutoa huduma kwa wananchi kwani sasa haihitaji mwananchi kwenda moja kwa moja kwenye Ofisi zetu na badala yake anaweza kwenda kwenye mtandao tu na kujaza fomu zake na kuweza kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo maafisa ambao wapo katika Balozi zetu wameshapata training juu ya matumizi haya ya uhamiaji mtandao, na pale ambapo wananchi ama wageni wanapohitaji huduma hizo kwa maeneo ambayo hakuna Maafisa Uhamiaji basi Maafisa wa Mambo ya Nje waliopo katika Balozi zetu huwa wanatoa msaada kwa wale ambao wanahitaji huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo kwa ufupi ni dhahiri kwamba uchache huo wa maafisa ambao ameuzungumzia Mheshimiwa Heche hauna madhara yoyote mpaka sasa hivi kwa huduma mbalimbali za raia na wageni ambao wanataka kuzipata katika Balozi zetu duniani.