Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 inayounganisha Tanzania na Mozambique mpaka sasa bado haijajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa na kuanza ujenzi huo kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii katika suala la usanifu na upembuzi wakina sasa hivi limechukua miaka nane. Sasa swali langu ni kwa nini Serikali inachukua muda mrefu kiasi hiki kwa ajili ya kufanya tu usanifu na upembuzi wa kina?

(b) Barabara hii imebeba uzito mkubwa sana katika kuharakisha shughuli za kiuchumi ili tuweze kufikia uchumi wa kati itakapofika mwaka 2025. Lakini kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba upembuzi yakinifu unaendelea na usanifu mpaka inakapofika Juni, 2020 ninapata mashaka kwamba huenda hii barabara ikaendelea kuchelewa ziadi.

Je, Serikali haioni kwamba kutoleta maendeleo au kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami ambayo inapita katika kata zifuatazo zinazoendelea kujishughulikisha katika shughuli za uchumi ikiwa pamoja na makaa ya mawe yanayochimbwa huko? Lakini pia shamba kubwa la miwa linaloenda kuanzishwa huko. Na kata hizo ningependa nizitaje, ni kata ya Likuyufusi, Litapwasi, Ndogosi, Muhukulu lilayi na Muhukulu barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa serikali itakwenda kuanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nitumie nafasi hii nishukuru kwa swali nzuri lakini niseme tu, eneo hili la Likuyufusi barabara hii ya Likuyufusi Mkenda ni barabara ambayo inagusa majimbo mawili; Jimbo la Peramiho kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama, lakini pia inawahudumia kwa kiasi kikubwa wananchi wa jimbo la Nyasa. Ambapo kuna kazi kubwa imefanyika kwa sababu barabara hii ina wapunguzia adha wananchi wa kata hii ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa juhudi ambazo zinafanyika na kwa ushirikiano mkubwa kwa Mheshimiwa Jacqueline na Wabunge wa majimbo inayofanyika, barabara hii ipo katika ubora kwa kuzingatia mahitaji ambayo nimeyata. Tunatambua kwamba ili tuweze kujenga uchumi ni lazima miundombinu iwe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembelea na nimejionea namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge hawa akinamama, na niseme Wabunge wakinamama kazi nzuri wanafanya. Nimekwenda kule nimeona kule Mitomoni kuna MV Stella inasaidia wananchi wale kuvuka ili watumie barabara hii ambayo kwa kiasi kikubwa tumeiboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga vizuri. Wakati harakati za kujenga barabara ya lami zinafanyika, tunazingatia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha barabara hii inakuwa bora. Yako maeneo ambayo tumeweka madaraja ya chuma, yako maeneo tumeelekeza ili wakati huu tunafanya harakati za kuhuisha kujua gharama halisi za ujenzi wa barabara za lami, barabara hii inakuwa bora na makaa ya mawe yanabebwa, hata mwekezaji anaendelea na harakati zake za uwekezaji wa kiwanda cha sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga vizuri, tutawa-support wananchi wa maeneo haya ya Peramiho, wananchi wa Kata alizozitaja ili nao waende katika harakati; hatupendi tukifika uchumi wa kati wawe chini ya mstari ule wa wastani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga vizuri kwenda kuiboresha barabara hii. Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo; Mheshimiwa Mhagama na Mheshimiwa Manyanya, tumejipanga vizuri, vuteni subira, muwe comfortable, tutaenda kuijenga barabara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda Mkenda nimeona pia kuna soko zuri, nimeona wananchi wa kule Msumbiji wana mahitaji makubwa ya mahindi ambayo yanazalishwa upande wa Peramiho. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu huo wa kufanya maboresho ili wananchi hawa waweze kupata manufaa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.