Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Nassor Suleiman Omar
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Ziwani
Primary Question
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR aliuliza:- Utamaduni katika kila nchi ni utambulisho wa Taifa; na kwa kuwa kuna upotevu mkubwa wa utamaduni wa asili kwenye makabila yetu nchini:- Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kufufua utamaduni wa asili wa makabila yetu?
Supplementary Question 1
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Utamaduni una maana pana ikiwemo mazishi na mavazi. Je, ni lini Serikali itatangaza rasmi vazi la Taifa? (Makofi)
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuridhika na majibu ambayo yametolewa na Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la msingi ambapo ametaka kujua ni lini sasa Serikali itakuja rasmi na mchakato wa kutangaza vazi rasmi la Taifa, mara nyingi tumekuwa tukijibu swali hili ndani ya Bunge na sisi kama Wizara ambao ndiyo tunasimamia masuala mazima ya utamaduni ikiwemo lugha pamoja na vazi la Taifa, tupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba tunaleta vazi la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato unaoendelea sasa hivi ndani ya Wizara ni kuhakikisha kwamba tunakusanya mavazi yote kutoka kwenye mikoa kwa sababu tunajua kabisa vazi la Taifa siyo kitu ambacho tunaweza kukipata kutoka kwenye jamii moja. Tunachotaka kukifanya sasa hivi ni kuhakikisha mikoa na wilaya zote na wadau wote wa sanaa pamoja na wabunifu wa mavazi wanashiriki kwenye mchakato huu wa kupata vazi la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi mchakato huo utakapokamilika sisi kama Wizara tutakuja rasmi na vazi la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR aliuliza:- Utamaduni katika kila nchi ni utambulisho wa Taifa; na kwa kuwa kuna upotevu mkubwa wa utamaduni wa asili kwenye makabila yetu nchini:- Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kufufua utamaduni wa asili wa makabila yetu?
Supplementary Question 2
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Chakula pia ni moja ya utamaduni. Je, Serikali inasema nini juu ya vyakula vinayotoka nje ya nchi ambavyo ni kinyume na utamaduni wetu wa chakula cha asili ambacho tulikuwa tunakitumia? Nataka kujua tunatoa tamko gani kuzuia vyakula ambavyo siyo vya utamaduni wetu na vinaathiri afya za Watanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya maswali yaliyotangulia. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali alilouliza ni mtambuka linalohusu biashara ya nje na sekta mbalimbali ambapo Wizara yangu haiwezi kulitolea tamko hapa kwamba kuanzia sasa vyakula ambavyo siyo vya utamaduni visiingie nchini. Hili ni suala pana ambalo hata Bunge lako Tukufu lina mamlaka ya kuweza kulijadili kwa upana zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Name
Masoud Abdalla Salim
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtambile
Primary Question
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR aliuliza:- Utamaduni katika kila nchi ni utambulisho wa Taifa; na kwa kuwa kuna upotevu mkubwa wa utamaduni wa asili kwenye makabila yetu nchini:- Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kufufua utamaduni wa asili wa makabila yetu?
Supplementary Question 3
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alituambia kwamba yuko katika mkakati na mchakato wa kuendeleza Kiswahili nje ya nchi lakini inaonekana kwamba Kiswahili kinachofundishwa nje ya nchi siyo standard Swahili, siyo lugha sanifu ndani ya Tanzania ni Kiswahili cha nchi jirani. Je, wana mkakati gani wa ziada kuhakikisha Kiswahili chetu cha Tanzania ambacho ni Kiswahili sanifu (standard Swahili) ndicho ambacho kinatumika nje ya nchi na siyo Kiswahili cha nchi ya jirani?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud, Kiswahili si ni lugha, sijaelewa unamaanisha lafudhi au lugha, hebu uliza swali lako vizuri.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, standard Swahili (Kiswahili sanifu) ndicho ambacho kinaongelewa au kinaandikwa hapa Tanzania lakini katika nchi nyingine, unapokwenda huko duniani katika nchi za Ulaya Kiswahili ambacho kinafundishwa ni cha nchi jirani siyo cha Tanzania.
MBUNGE FULANI: Kweli.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kweli na ndiyo uhalisia. Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie …
NAIBU SPIKA: Sawa, umeeleweka Mheshimiwa.
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika matumizi ya lugha yoyote duniani kuna kitu kinaitwa standardization, kila mtu lazima atumie lugha ambayo ni sanifu. Ndiyo maana Jumuiya ya Afrika Mashariki imeunda Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yako Zanzibar na moja ya kazi yake kubwa ni kufanya lugha ya Kiswahili iwe na urari wa aina moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, tuna kazi pia kubwa ya kufanya kati ya sisi upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar kuoanisha baadhi ya misemo na maneno ili tusiwe na lugha mbili. Kwa mfano, jana nimeona Kamusi kutoka Zanzibar inaitwa ‘Kamusi Sanifu la Kiswahili’ wakati sisi huku Bara Kamusi haiwezi kuwa ‘likamusi’ ni ‘Kamusi ya Kiswahili’. Sasa sisi wenyewe tuna matatizo ndiyo maana inabidi tukae, Baraza la Kiswahili la Zanzibar na Baraza la Kiswahili la Tanzania wakae pamoja kwanza tuwe na lugha ya aina moja ili tuweze kuwashawishi wenzetu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved