Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sabreena Hamza Sungura
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:- Je, ni muda gani mchakato wa kuandaa hatimiliki unatakiwa kukamilika kwa mujibu wa sera na taratibu?
Supplementary Question 1
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wazaramu wana msemo wao unaosema kwamba: “Zilongwa mbali, zitendwa mbali”. Ukiangalia majibu haya na uhalisia kwa wananchi ni vitu viwili tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa suala zima la watu kupatiwa Hatimiliki Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana alitangaza kwamba wananchi waache kutumia offer na waingie kwenye mfumo huo rasmi wa kutumia Hatimiliki na wananchi walifanya maombi kwa muda mrefu sana. Katika Kanda mbalimbali kumekuwa kuna unreasonable delay ya kutolewa kwa vitu hivi ambavyo wanajua ni vya msingi na vinawafaa sana wananchi wetu na vinatakiwa vitolewe kwa wakati. Je, Wizara sasa iko tayari kuunda tume kuchunguza maafisa wa Serikali ambao wanaharibu mpango huu mzuri wa Serikali kwa makusudi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunaelewa kabisa kwamba sasa hivi kama nchi inajipanga irudi kuendesha bajeti zake kwa kutumia vyanzo vyetu vya ndani na Serikali imekuwa ikipata mapato kupitia urasimishaji wa Hatimiliki na vilevile hata pale inapofanya transfer au sale, imekuwa ikipata mapato kama capital gain tax ambayo ni 10%, stamp duty, registration fee na kadhalika. Je, kwa kuchelewesha kuwapa huduma hizi kwa wakati muafaka kutokana na majibu haya ndani ya siku saba mpaka mwezi mmoja hawaoni kwamba wanaisababishia Serikali hasara hasa ikizingatiwa umuhimu wa Wizara hii ambapo kikatiba majukumu haya amepewa Mheshimiwa Rais na yeye ameyagawa kwa Makamishna wa Wizara ili waweze kumsaidia?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sabreena, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameongelea habari ya ucheleweshaji, pengine watumishi hawafanyi kazi zao vizuri kiasi cha kuchelewesha Hati kutoka na hivyo kuwanyima haki wananchi. Naomba nimthibitishie tu kwamba katika zoezi zima la utoaji Hati toka tumebadili muundo ndani ya Wizara katika kufuatilia kwa karibu mpaka sasa baadhi ya Kanda zina Hati zaidi ya maelfu ambazo hazijachukuliwa, kwa mfano, Dar es Salaam (7,000), Tabora (12,000) na Mwanza (7,000). Kwa hiyo, kasi ya utoaji Hati ni kubwa lakini pia wananchi hawazichukui.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tu kwamba wazifuate Hati zao ili waweze kuwa na umiliki ulio na salama zaidi. Watumishi sasa hivi wamebadilika siyo kama ilivyokuwa zamani. Nikiri mwanzo kidogo kulikuwa na ucheleweshaji lakini baada ya kuwa na mkataba kwa mteja kazi inaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la siku saba au thelathini ni kwamba hatutaki kumsumbua mwananchi. Kwa mfano, katika ile njia ya elektroniki ambayo inatumika Dar es Salaam Hati inaweza ikatoka ndani ya siku mbili au siku moja lakini hatutaki kumcheleweshea kwa sababu kunakuwa pengine na mlolongo wa watu ambao wako pale kuliko asubiri pengine amekuja asubuhi itatoka saa nane, basi tunampa siku ili apate muda wa kuja kuchukua. Kwa kutumia njia ya elektroniki Hati inaweza ikatoka kwa siku moja kama taratibu zote zimezingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anaongelea habari ya mapato, ni kweli mapato yanaongezeka kadri ambavyo utoaji hati unafanyika. Hata hivyo, napenda kumthibitishia tu kwamba katika usajili wa Hati mbalimbali ambazo zinafanyika, Wizara imekuwa ikifanya usajili katika nyaraka mbalimbali. Ukiangalia kuanzia Julai, 2018 mpaka Juni, 2019, Hati za kumiliki ardhi zilizotolewa ni 49,892 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Pia ukiangalia milki zilizofanyiwa transfer nazo ni 2,998. Vilevile kuna hizo nyaraka ambazo ameziongelea pale wanapokuwa wana-surrender nazo tumeshasajili 2,632.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna mlolongo mrefu ambao tumefanya ambapo unaingizia mapato Serikali. Sasa hivi wananchi wamekuwa makini katika kufuata taratibu, hawafanyi tofauti na kile ambacho wanaelekezwa na wengi wanakuja ofisini. Kwa hiyo, niseme mapato yameongezeka na wananchi sasa wanatumia ofisi zetu vizuri tofauti na walivyokuwa wakifanya awali.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved