Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:- Je, ni hatua zipi zimechukuliwa hadi sasa kumaliza mgogoro wa mipaka kati ya Ranchi ya Missenyi na Vijiji vinavyopakana na Ranchi?

Supplementary Question 1

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri na nichukue nafasi hii kumpongeza pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa uteuzi alioupata na kwa kazi nzuri ambayo anaifanya toka ameteuliwa. Pamoja na hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ukiangalia majibu yanayoonyesha kwamba NARCO walipewa ramani tarehe 20 Oktoba, 1969, yanathibitisha ukweli kwamba vijiji vya maeneo hayo vilikuwepo kabla ya ranchi. Kwa kuwa tulipokuwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa wa Kagera wa wakati huo na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, alioneshwa ramani ya NARCO ambayo ilionesha unapovuka Mto Kagera ukaenda mpaka wa Uganda hakuna kijiji, eneo lote ni la NARCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alishtuka na akaelekeza ramani hiyo siyo sahihi na akasema yeye alipokuwa askari alipigana vita na vijiji vilikuwepo na akaelekeza ramani hiyo irejeshwe kwake ili aweze kuipitia na ifutwe kwa sababu haitambui uwepo wa vijiji na toka wakati huo ramani hiyo imekuwa siri kubwa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kunionesha nakala ya NARCO wanayoitumia kugawa maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili, pamoja na majibu mazuri kwamba hekta 21,571 zimetolewa lakini nakuwa na wasiwasi kwa sababu katika eneo hilo inaonekana kuna viongozi wanaolipwa ili wasione na kwa kuwa bado wapo maamuzi haya mazuri huenda yasilete tija. Je, yuko tayari kuniambia haya maeneo yaliyoongezwa ni yaleyale yaliyokuwa ya vijiji au ni maeneo yaliyokuwa ya NARCO sasa vijiji vimeongezewa? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Kamala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaozunguka mashamba ya NARCO katika Wilaya ya Misenyi wamekuwa na mgogoro na Serikali na NARCO kwa muda mrefu. Hatua zilizochukuliwa sasa ni kwamba mchakato wa kupitia upya mgongano wa ramani hizi umeshaanza katika ngazi ya wilaya na unaendelea katika ngazi ya mkoa. Wataalam kutoka TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi sasa hivi wameanza kupitia mipaka ili kuondoa tatizo hili la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Balozi Dkt. Kamala achukue hatua tu kuwasilisha haya mawazo yake aliyoyasema na namna gani tunaweza kumaliza jambo hili kimaandishi Serikalini ili na yeye awe part ya mchakato huu wa kumaliza mgogoro wa mipaka katika vijiji hivi.