Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. NAGHENJWA L. KABOYOKA) aliuliza:- Umeme wa maji unaonekana kuwa wa bei nafuu, na Same kuna maporomoko ya Mto Hingilili yanayoangukia Kata ya Maore na ya Mto Yongoma yanayoangukia Kata ya Ndungu; na Chuo cha Ufundi Arusha wameonesha utaalamu mkubwa wa kutengeneza umeme kwa kutumia maji hayo:- Je, Serikali ipo tayari kukiwezesha Chuo hicho ili kiweze kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa maji Kata za Maore na Ndungu?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Waziri kwa namna anavyojibu maswali hapa pamoja na kazi yake. Nafanya hivi sina hiyana kwa sababu imekuwa ni desturi ya Mawaziri kuwasifia Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na sisi huku kukaa kimya na mimi nichukue nafasi hii kujisifu, nafanya kazi nzuri jimboni kwangu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maswali, swali la kwanza, swali hili limekuja ni mara ya pili sasa na Chuo cha Ufundi Arusha kimeonesha nia ya kutaka kufanya kazi hii. Kwa nini kuchukua mzunguko mrefu kuwapa TANESCO kufanya upembuzi yakinifu wasiachie tu hiki chuo kikafanya hii kazi kikamaliza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama nilivyosema nafanya kazi nzuri sana kwenye Jimbo lango, kuna Kata za Reha, Nanjara, Kitirima, Kingachi, Mrao Keryo, Katangara Mrere ambako kuna vijiji umeme haujafika na kuna nguzo ambazo ziko chini. Ukweli ni kwamba kuna matatizo makubwa ya nguzo jimboni kwangu. Je, Waziri sasa yuko tayari kutoa maagizo maalum ili TANESCO kule Rombo wasiniharibie kazi yangu nzuri nayofanya ili kazi hii ikafanyika mara moja?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Baba Paroko, Mbunge wa Jimbo la Rombo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tupokee pongezi zake lakini na sisi tunakiri kweli mara kwa mara amekuwa akifuatilia changamoto mbalimbali za jimbo lake kwenye sekta ya nishati na hata kupitia ziara zetu tumekuwa tukishirikiana naye vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake ya nyongeza mawili ameuliza kwamba kwa nini inachukua mzunguko mrefu kuihusisha TANESCO. Kwa mujibu wa sheria kwa kweli mwenye mamlaka na masuala mazima ya sekta ya nishati, hususani masuala ya umeme, ni TANESCO ambaye ndiyo mzalishaji, msafirishaji na msambazaji. Kwa hiyo, labda nilichukue hili ili tuone namna gani tutafanya uharaka kati ya TANESCO na hicho Chuo cha Ufundi Arusha kwa ajili ya kuona huu upembuzi yakinifu unaotarajiwa kufanyika ufanyike kwa haraka ili tuone fursa zilizopo wakati wa kutekeleza ule mradi, aina ya maporomoko ya maji na uwezo wa kuzalisha hizo megawati, kwa hiyo, nilichukue hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la nyongeza kuna kata amezitaka ikiwemo Nanjara akiainisha kwamba kuna nguzo ziko chini na vijiji vingine kazi ya kusambaza umeme haijamalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimtaarifu, kwenye Jimbo lake la Rombo ni vijiji nane tu ambavyo havina umeme. Mkoa wa Kilimanjaro mzima una Kata 148 zote zina umeme na vijiji 519 ni Vijiji 453 vina umeme. Kwa hiyo, bado vijiji 66 tu. Kazi iliyopo, tuna matarajio Mkandarasi ambaye yupo, ni kweli alikuwa na changamoto, lakini tumekaa naye Dodoma hapa kutaka kujua mpango kazi wake. Tuna matarajio mpaka Desemba vijiji 35 vitakuwa vimekamilika, vitabakia Vijiji ambavyo kwa kweli kama Vijiji 26 ambavyo naomba niwathibitishie wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro vitakuwa vimekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo Kilimanjaro, wanahitaji ujazilizi na kwa awamu ya pili ya ujazilizi inayoendelea Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa Mikoa tisa. Kwa hiyo, maeneo ambayo ni ya Vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mbunge yataingia kwenye ujazilizi, vitongoji na maeneo kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata message nyingi sana za wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo na Wilaya yako na Rombo na kazi nzuri pia inayofanywa pale na Mkuu wa Wilaya ya Rombo. Kwa hiyo, nataka nikuthubitishie kwamba tutashirikiana ili ujazilizi ukidhi mahitaji kwamba tumalize Mkoa wa Kilimanjaro wote kwamba uwe umewekewa umeme kwa miradi inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyemiti, ahsante sana.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. NAGHENJWA L. KABOYOKA) aliuliza:- Umeme wa maji unaonekana kuwa wa bei nafuu, na Same kuna maporomoko ya Mto Hingilili yanayoangukia Kata ya Maore na ya Mto Yongoma yanayoangukia Kata ya Ndungu; na Chuo cha Ufundi Arusha wameonesha utaalamu mkubwa wa kutengeneza umeme kwa kutumia maji hayo:- Je, Serikali ipo tayari kukiwezesha Chuo hicho ili kiweze kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa maji Kata za Maore na Ndungu?

Supplementary Question 2

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nchi yetu ya Tanzania tumebahatika kuwa na vyanzo vingi vya umeme ikiwemo umeme wa upepo, Joto ardhi, maji, solar na vinginevyo. Sasa Serikali ina mkakati gani shirikishi na endelevu ifikapo mwaka 2030 kutekeleza kikamilifu lengo la saba la malengo endelevu ya dunia la kuwa na affordable and clean energy?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali zuri la nyongeza la Mheshimiwa Mbatia akiuliza mkakati wa Kiserikali ambapo kufikia mwaka 2020 inaweza ikatekeleza lengo la millennium ambalo amelitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mkakati wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano tulivyojipanga ifikapo mwaka 2025 tuna matarajio ya kuzalisha megawatts 10,000. Megawatts 10,000 hizi zitatokana na vyanzo mbalimbali ambavyo amevitaja ikiwemo maji, gesi, nishati jadidifu, joto ardhi, solar na masuala ya upepo. Hivi tunavyozungumza, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na energy mix ya uhakika ambapo kuzalisha umeme kutokana na vyanzo mbalimbali kupitia TANESCO, Serikali imetangaza tenda kwa ajili ya kuzalisha megawatts 950 ikiwemo megawatts 600 ya Makaa ya Mawe, megawatts 200 kupitia upepo na megawatts 150 kupitia jua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuhusu masuala ya joto ardhi, Serikali kupitia tafiti mbalimbali na Taasisi yake ya joto ardhi, imetambua uwepo wa vyanzo vya kuweza kuzalisha umeme kupitia joto ardhi na sasa mpango unaoendelea, tunaishukuru Wizara ya Fedha imeiwezesha Tasisi ya joto ardhi kiasi cha pesa takribani shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ununzi wa mashine za kuchoronga visima kwa ajili ya utafiti unaoendelea. Matarajio yetu, tutaanza kuzalisha megawatts 30 kutoka kwenye joto ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbatia kwamba kwa kweli Serikali inatambua na kuona umuhimu wa kuwa na energy mix ya kutosha kupitia vyanzo mbalimbali na ndiyo maana imejielekeza kwenye umeme wa maji, imejielekeza kwenye umeme wa gesi na miradi mbalimbali inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba tulivyojipanga, hilo lengo la millennium litafikiwa na tutakuwa na umeme wa kutosha ambao utaiwezesha nchi yetu pia kusaidia nchi za jirani, nchi za ukanda wa SADC na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. Tumejipanga sasa hivi ujenzi wa njia za kusafirisha umeme unaendelea vizuri katika maeneo hayo ili kuweza kuuza umeme katika nchi za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)