Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:- Wilaya ya Malinyi tangu mwaka 2014 mpaka sasa inakabiliwa na mlipuko wa panya wanaoshambulia mbegu za mazao ya Mpunga na Mahindi katika kipindi cha upandaji:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza sumu maalum ya kuua panya hao? (b) Kwa kuwa upatikanaji wa sumu ya panya una changamoto nyingi: Je, Serikali ina mkakati gani mbadala katika kukabiliana na panya hao waharibifu wa mazao shambani?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini angalizo langu la kwanza naomba uwe makini na uende kwa kina zaidi kwani hicho kitengo cha kudhibiti panya hakiko sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Serikali kupitia Chuo cha Utafiti cha Sokoine, wamefanya utafiti njia mbadala ya kudhibiti hao panya kwamba wamegundua mkojo bandia wa paka unaoweza kuwadhibiti panya hao bila madhara makubwa kama tunavyotumia sumu ya kawaida. Swali langu, ni kwa namna gani Serikali kwa haraka inaweza ikasambaza matokeo ya utafiti huu, maana yake huo mkojo bandia wa paka huweza kukabiliana na adha hiyo ya panya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hiyo hiyo Wilaya ya Malinyi takribani sasa ni mwaka wa tano tunasumbuliwa na ugonjwa wa virusi kwa ajili ya zao la mpunga, Kiingereza wanaita Rice Virus Disease ambapo kule kwetu jina maarufu Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi tunaita Kimyanga; unashambulia mpunga, kipindi ambacho karibu unataka kuzaa unakuwa na rangi ya njano baadaye unaathiri kabisa uzalishaji. Sasa Serikali mna utaratibu gani kusaidia wananchi hawa wakabiliane na huo ugonjwa wa Kimyanga ambao ni adha kubwa sana kwa wakulima wa mpunga kwa maeneo hayo?

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la Rice Virus Disease ambalo linaathiri Wilaya ya Malinyi, Wizara kupitia TARI, sasa hivi wataalam wetu wa TARI wanafanya special investigation kuweza kujua njia bora ya kuweza kudhibiti virus huyu asiweze kusambaa na hivi karibuni tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri ya Mkoa wa Morogoro kwa ujumla ili kuweza kuwapa mbinu mbadala za kuweza kupambana na virus huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili la Chuo cha Sokoine, kwa kuwa liko ndani ya docket yetu ya Wizara na sisi ni interested party, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua na tutalifanyia kazi. Hatua zozote ambazo zinaweza kutusaidia kupambana na changamoto ya panya, ingawa katika Mikoa ya Mtwara ni fursa kwao lakini tutahamasisha wenzetu wa Mtwara waje maeneo ya Malinyi kuweza kuwatega. Vilevile sisi kama Wizara tutashirikiana na SUA kuweza kutumia njia mbadala walioweza kugundua kuondoa hili tatizo.