Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Masoud Abdalla Salim
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtambile
Primary Question
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:- Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2019:- Je, Serikali inasema nini juu ya ushirikishwaji wa Vyama vya Siasa katika mkakati wa kutoa elimu ili kufikia lengo la uchaguzi huru na haki?
Supplementary Question 1
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kutakuwepo na uchaguzi wa huru na haki. Nataka nimwambie tu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 3(1) inasema, “Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na malalamiko kila kona juu ya tabia mbaya iliyoonekana, kuhusu kuondolewa kwa Wagombea wa Upinzani hasa katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa unaofanyika tarehe 24 kwa vyama vya ACT Wazalendo, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi. Imeonekana huu ni mkakati maalum wa Serikali katika kudhoofisha upinzani hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri utuambie, mna makakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba tabia hii mbaya, chafu iliyofanywa makusudi na Serikali kwamba wagombea hawa wa upinzani wanarejeshwa na wanashiriki uchaguzi tarehe 24 mwaka huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili,…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Masoud, hilo siyo swali.
MBUNGE FULANI: Ni swali.
MWENYEKITI: Endelea swali lingine.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri mhusika, Mheshimiwa Jafo alisema, wasimamizi wa uchaguzi na wote waliohusika kuwaondoa Wagombea wa Upinzani, wasilikilize malalamiko hayo na baadaye kutoa haki ambayo italeta tija katika uchaguzi huu ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uniambie, pamoja na kauli ya Waziri ambapo hadi sasa baadhi ya watendaji hawa, wasimamizi wanakimbia katika ofisi: Je, mna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba maandalizi haya yataweza kufanikisha uchaguzi huu na ukawa wa haki na huru?
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Hili swali ni muhimu kwa ajili ya uelewa. Nalitumia jukwaa lako ili uniruhusu nitoe elimu pia kwa wale wote ambao hawajaelewa utaratibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kwamba Waheshimiwa Wabunge wamelalamika sana kwenye Bunge hili, naomba niwaarifu kwamba Wabunge hawana haki ya kuweka pingamizi wala kulalamikia uchaguzi kama wametendewa haki ama lah! Wenye haki ya kulalamika ni wale watu wote ambao walijaza fomu na kusema wameondolewa. Utaratibu umeainishwa vizuri kwenye Kanuni yetu na Waheshimiwa Wabunge na Vyama vya Siasa wamepewa Kanuni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, muda wa vipingamizi haujaisha. Kanuni imeeleza, baada ya uteuzi, kuanzia tarehe 5 mpaka tarehe 6 ambayo ilikuwa ni jana, wale wote ambao wamekuwa hawajaridhika na uteuzi au kuondolewa ama kuteuliwa kugombea walipaswa wapeleke pingamizi kwenye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi. Kama hawajaridhika na maamuzi hayo, pia wanayo fursa mpaka tarehe 9 kwenda kupeleka pingamizi kwenye Kamati ya Rufaa.
Pia kama hawataridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa ambayo inapatikana kwenye ngazi ya Wilaya, wanayofursa ndani ya siku 30 kwenda kwenye Mahakama yoyote kuanzia na wilaya kwenda kuweka pingamizi kuweza kupata haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hayupo hapa Bungeni leo, lakini jana alikuwa Singida. Yanayozungumzwa Bungeni na kule site hali ni tofauti sana. Ameenda Manyara na sasa hivi ninavyozungumza yuko Iringa, ataenda Njombe. Tumetuma watu kule Liwale na Moshi. Mazungumzo mengi ya Waheshimiwa Wabunge humu ndani yanatofautiana sana na hali halisi kule site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, yaliyozungumzwa hapa kuna Wabunge wamechukua clip wameweka kwenye mtandao. Nimeuliza kwa mfano Tarime Mjini, Mheshimiwa Mbunge alitoa taarifa hapa kwenye clip akisema wagombea wote wameondolewa, siyo kweli. Taarifa za leo asubuhi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa nchi ni kwamba, Kanuni inaelekeza, yule ambaye hajaridhika na uteuzi wake apeleke pingamizi kwenye vyombo vile na asiporidhika ndiyo aseme. (Makofi/ Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwatie moyo Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Watanzania, utaratibu unaeleweka, lazima ufuatwe…
MBUNGE FULANI: Wamefunga Ofisi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SRIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …na uchaguzi huu utakuwa ni huru na haki kwa wale ambao watazingatia taratibu na sheria za uchaguzi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved